Jumatano tarehe 16 Machi mwaka 2022
Leo ni Jumatano tarehe 13 Shaaban 143 Hijria sawa na Machi 16 mwaka 2022.
Katika siku kama ya leo miaka 163 iliyopita Alexander Stepanovich Popov, mvumbuzi na mwanafizikia wa Russia alizaliwa. Baada ya kuhitimu masomo katika taaluma ya fizikia, alianza kujishughulisha na ufundishaji katika vyuo vikuu vya nchi hiyo. Mbali na shughuli hiyo, Popov aliendelea mbele na utafiti wake katika nyanja mbalimbali za kielimu ambapo baadaye alifanikiwa kuvumbua chombo cha kunasia sauti. Aliaga dunia mwaka 1906.
Katika siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, Parvin I’tisami mwandishi na malenga mahiri wa Kiirani aliyekuwa na kipaji kikubwa alizaliwa katika mji wa Tabriz ulioko kaskazini magharibi mwa Iran. Mshairi huyu alizaliwa katika familia iliyosifika kwa fadhila na heshima. Baba yake ni Yusuf I’tisam al-Mulk aliyekuwa mmoja wa watarjumi na waandishi watajika katika zama zake. Parvin alijifunza fasihi ya Iran na ya Kiarabu kwa baba yake na alionyesha kipaji cha hali ya juu cha mashairi tangu akiwa mdogo. Katika kipindi chote cha masomo, Parvin I’tisami alikuwa mwanafunzi bora shuleni. Safari zote alizifanya akiwa pamoja na baba yake na kujifunza mambo mengi katika safari hizo.
Miaka 83 iliyopita katika siku kama ya leo, katika hali ambayo Vita vya Pili vya Dunia havikuwa vimeanza, nchi ya Czechoslovakia ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Ujerumani ya Kinazi. Kwa utaratibu huu, Jamhuri ya Czechoslovakia ikawa nchi ya pili baada ya Austria kukaliwa kwa mabavu na Adolph Hitler.
Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, alifariki dunia Bi Selma Lagerlof mwandishi wa Sweden. Lagerlof alizaliwa mwaka 1858 na baada ya kumaliza masomo yake akaanza kujishughulisha na ukufunzi na uandishi wa hadithi na hekaya. Lagerlof alikuwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fasihi mwaka 1909.
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, Kamal Fouad Jumblatt mwanasiasa mahiri wa Lebanon aliuawa. Alizaliwa Disemba 6 mwaka 1917 huko Moukhtara kusini mwa Beirut. Mwaka 1952 na kuendelea, Kamal Fouad Jumblatt alikuwa mwanasiasa wa mrengo wa upinzani na akafanikiwa kumuondoa madarakani Bechara El Khoury Rais wa muda wa wakati huo wa Lebanon. Hatimaye Kamal Fouad Jumblatt aliuawa na wapinzani wake katika siku ma ya leo akiwa na umri wa miaka 60.
Katika siku kama ya leo miaka 37 iliyopita Mahdi Bakeri mmoja wa makamanda mashujaa na wenye tadibiri katika kipindi cha kujihami kutakatifu wanananchi wa Iran mbele ya hujuma na mashambulio ya kichokozi ya jeshi la dikteta wa wakati huo wa Iraq Saddam Hussein alikufa shahidi. Alizaliwa katika mji wa Miandoab kaskazini magharibi mwa Iran na mama yake alifariki dunia wakati yeye akiwa mtoto mdogo. Kaka yake naye kutokana na kuonyesha upinzani dhidi ya utawala dhalimu wa Shah aliuawa na makachero wa utawala huo.
Na siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, utawala wa Baath nchini Iraq uliushambulia bila huruma na kwa mabomu ya kemikali za sumu mji wa Halabja wa wakazi wa Kikurdi huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kwa kutumia makumi ya ndege za kivita. Hujuma hiyo ilianza baada ya kushindwa kupambana na wapiganaji Waislamu wa Iran na wa Kikurdi wa huko Iraq, na katika upande wa pili wananchi Waislamu wa Halabja waliwakaribisha wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na dhulma na ukandamizaji usio na kipimo wa Saddam Hussein dhidi yao. Raia elfu tano wasio na hatia waliuawa kutokana na kuvuta gesi ya sumu huko Halabja. Hata hivyo nchi za Magharibi hazikuchukua hatua yoyote kwa jinai hiyo kubwa na ya kutisha. ***