Jumatatu tarehe 11 Aprili 2022
Leo ni Jumatatu tarehe 9 Ramadhani 1443 Hijria sawa na tarehe 11 Aprili 2022.
Siku kama ya leo miaka 162 iliyopita chombo cha kuzalisha baridi kilibuniwa na mwanakemia wa Kifaransa kwa jina la Ferdinand Carre. Kifaa hicho kilikuwa kikizalisha baridi kwa kutumia gesi ya ammonia. Ubunifu huo wa Carre ulikuwa hatua muhimu katika kuhifadhi vyakula ili visiharibike hususan katika maeneo yenye joto. Uvumbuzi wa msomi huyo hatimaye ulipelekea kutengenezwa kwa majokofu na vifaa vingine vikubwa vya kuzalisha baridi kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamadani. Ayatullah Bahari Hamadani alikuwa mmoja wa maulama wakubwa na mtaalamu mashuhuri wa elimu ya Irfan wa karne ya 13 na 14 Hijiria wa nchini Iran. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali, Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamadani alielekea Najaf, Iraq na baada ya kukamilisha masomo yake alijishughulisha na kazi ya ufundishaji. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Tadhkiratul-Muttaqiina.'
Miaka 37 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo aliaga dunia Enver Hoxha Rais wa zamani wa Albania. Hoxha alikuwa kiongozi wa wapiganaji wa mrengo wa kushoto baada ya Italia kuivamia na kuikalia kwa mabavu Albania mwaka 1939. Enver Hoxha alichukua madaraka ya nchi mwaka 1944 kwa kusaidiwa na jeshi la Urusi ya zamani baada ya kushindwa Italia katika Vita vya Pili vya Dunia. Rais huyo wa zamani wa Albania miaka miwili baadaye aliitangaza nchi hiyo kuwa ni Jamhuri ya Kikomonisti.
Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, siku moja tu baada ya mahakama moja ya Ujerumani kutoa hukumu dhidi ya viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ziliwaita nyumbani mabalozi wao kutoka mjini Tehran. Jaji wa mahakama hiyo iliyopata umaarufu kwa jina la Mykonos aliathiriwa mno na misimamo ya Kizayuni na kutangaza kuwa viongozi wa Iran walihusika katika mauaji ya mpinzani wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyekuwa akiishi Ujerumani. Iran ilikadhibisha madai hayo na ikajibu hatua ya nchi hizo kwa kuwaita nyumbani mabalozi wake wote katika nchi za Umoja wa Ulaya. Uamuzi wa mahakama ya Mykonos kwa hakika ulikuwa sehemu ya hujuma ya kisiasa ilikuwa ikiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Takribani miezi kumi baadaye mabalozi wa Umoja wa Ulaya walianza kurejea hapa Tehran mmoja baada ya mwingine.
