Alkhamisi tarehe 14 Aprili 2022
Leo ni Alkhamisi tarehe 12 Ramadhani 1443 Hijria sawa na Aprili 14 mwaka 2022.
Siku kama ya leo yaani tarehe 12 Ramadhani kwa mujibu wa wapokezi wengi wa kalenda ya Hijria Qamaria, ni siku ambayo Nabii Issa Ibn Maryam, Masih AS aliteremshiwa kitabu kitukufu cha Injili. Neno Injili ni la Kigiriki na lina maana ya bishara. Jina hilo limetajwa mara 12 katika Qur’ani Tukufu na kitabu hicho kinaitambua Injili kuwa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu SW chenye sheria na kanuni za mbinginu. Hata hivyo kitabu kinachojulikana hivi sasa kwa jina la Injili si kile kilichoteremshwa kwa Nabii Issa Masih bali ni riwaya na kumbukumbu zilizokusanywa na wanafunzi wake baada ya Yeye kupaa mbinguni.

Siku kama ya leo miaka 1442 iliyopita yaani tarehe 12 Ramadhani mwaka wa kwanza Hijria, muda mfupi baada ya Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) kuhama Makka na kuelekea Madina, aliunga udugu baina ya Muhajirina na Ansar. Muhajirina ni watu ambao walihama na Mtume (SAW) kutoka Makka kwenda Madina, na Ansar ni Waislamu wa Madina waliowakaribisha Muhajirina katika mji huo. Kwenye sherehe hiyo ya kuunga udugu bina ya Waislamu, Mtume (SAW) alimtangaza Ali bin Abi Talib (AS) kuwa ndugu yake hapa duniani na Akhera.

Siku kama ya leo miaka 896 iliyopita alizaliwa Ibn Rushd, mwanafalsafa na mwanafikra maarufu wa Waislamu mjini Andalusia (sehemu ya Uhispania ya sasa). Baba na babu wa Ibn Rushd, wote walikuwa makadhi mjini Andalusia. Akiwa kijana alipata kusoma elimu mbalimbali za zama zake, huku akitabahari zaidi katika elimu za hisabati, sayansi ya elimu asilia, nyota, mantiki, falsafa na udaktari. Kufuatia hali hiyo alipewa kipaumbele na watawala wa silsila ya Muwahhidun ambao walikuwa wakiitawala Andalusia wakati huo, kiasi cha kufikia kuteuliwa kuwa kadhi wa mji wa Córdoba, mji mkuu wa Andalusia. Hata hivyo mwishoni mwa umri wake alichukiwa na watawala na hatimaye akabaidishwa. Mielekeo ya Ibn Rushd ilielemea sana kwenye fikra za Aristotle. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na ‘Tahaafut al-Tuhafat’ ‘Kitabul-Kulliyyaat’ na ‘Faslul-Maqaala.’ Ibn Rushd alifariki dunia Disemba, 1198 Miladia sawa na mwezi Swafar 595 Hijiria.
Tarehe 12 Ramadhani miaka 846 iliyopita, alifariki dunia Ibn Jawzi, faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi katika karne ya 6 Hijria. Ibn Jawzi alizaliwa mwaka 510 Hijria na kufanya safari nyingi kwa ajili ya masomo. Mbali na kubobea katika masuala ya elimu ya fiq'hi na hadithi, alikuwa mtaalamu katika uwanja wa kutoa mawaidha na hata akaweza kuaminiwa na maulamaa wakubwa wa zama zake. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi na mashuhuri zaidi ni Al Muntadhim na Mawaidhul Muluk.

Siku kama ya leo miaka 176 iliyopita alizaliwa Friedrich Carl Andreas, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) na Iran huko nchini Ujerumani. Baada ya kufahamiana na mtaalamu mmoja wa masuala ya mashariki wa nchini Denmark, alivutiwa sana na utamaduni wa Iran ambapo alianza kufanya utafiti kwa kipindi cha miaka minne katika uwanja huo. Katika kukamilisha masomo yake aliamua kutembelea nchi za Iran na India sambamba na kujifunza lugha ya Kifarsi. Kwa karibu kipindi cha miaka 30 alikuwa mwalimu wa lugha ya Kifarsi katika Chuo Kikuu cha Göttingen nchini Ujerumani ambapo wanafunzi wake walipata kufahamu tamaduni za thamani za Iran. Mtaalamu huyo wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ujerumani alifariki dunia mwaka 1930.
Siku kama hii ya leo miaka 132 iliyopita muungano wa Pan American ambao baadaye ulibadili jina na kujulikana kama Jumuiya ya Nchi za Amerika uliasisiwa. Nchi wanachama wa jumuiya hiyo zilikuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali hadi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Hata hivyo baada ya vita hivyo kumalizika Jumuiya ya Nchi za Amerika iliundwa kutokana na kuweko haja ya kupanuliwa zaidi mashirikiano kati ya nchi hizo. Pamoja na hayo yote kitu kinachoitia wasiwasi jumuiya hiyo ni satwa na ushawishi mkubwa wa Marekani katika jumuiya hiyo na hatua yake ya kukitumia vibaya chombo hicho kwa maslahi yake ya kisiasa. Kwa sababu hiyo nchi wanachama zinafanya jitihada kubwa za kupunguza ushawishi wa Marekani katika jumuiya hiyo.

Katika siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sheikh Mahdi Khalisi, faqihi na mujtahidi mkubwa wa zama hizo. Ayatullah Khalisi alizaliwa huko Kadhimiya nchini Iraq mwaka 1277 Hijiria na akiwa kijana alijishughulisha na kuamrisha mema na kukataza maovu sambamba na kustahamili shida nyingi kipindi cha masomo na kutafuta elimu. Katika kipindi cha Vita vya Kwanza vya Dunia, msomi huyo akishirikiana na baadhi ya mujtahid wa Iraq, alianzisha mapambano dhidi ya uvamizi wa wakoloni Waingereza nchini humo. Baada ya muda alirejea nchini Iran na kujishughulisha na kazi ya ualimu na kufunza elimu za kidini. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo mkubwa ni Kifayatul Usuul na Anawinul Usul.
Tarehe 25 Farvardin miaka 34 iliyopita serikali ya wakati huo ya Iraq ilikiri kwamba ilitumia silaha za kemikali katika vita vyake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi chote cha miaka minane ya vita hivyo Iran iliwasilisha mashtaka katika jumuiya za kimataifa kwamba Iraq inatumia silaha za kemikali dhidi ya wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu. Wakati huo Iraq haikukiri wala kukadhibisha habari hiyo. Hata hivyo katika siku kama hii ya leo wakati vita vilipokuwa vimepamba moto, serikali ya Baghdad ilikiri kwamba inatumia silaha za kemikali zikiwemo za gesi ya sumu na hatari ya haradali dhidi ya malengo ya kijeshi na kiraia ya Iran.
Takwimu zimeonesha kwamba utawala wa Baath wa Iraq ulifanya mashambulizi 3,500 kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chote cha vita hivyo.

Miaka 20 iliyopita katika siku kama leo, Hugo Chavez rais wa zamani wa Venezuela alirejea nchini kwake na kushika hatamu za uongozi baada ya kufeli jaribio la mapinduzi ya kumuondoa madarakani. Chavez Aliingia madarakani mwaka 1999 na kufanya mabadiliko makubwa kwa maslahi ya tabaka la chini. Vilevile alichukua hatua za kusimamia mashirika ya mafuta ya Kimarekani yaliyokuwa yakichimba mafuta ya nchi hiyo. Siasa za kujitegemea za Chavez ziliikasirisha sana Washington. Ni kwa sababu hiyo, ndiyo maana Marekani ilipanga na kuratibu mapinduzi mnamo tarehe 12 Machi mwaka 2002. Licha ya mapinduzi hayo kupata mafanikio katika hatua za awali, lakini wananchi wa Venezuela waliokuwa wameridhishwa na mabadiliko ya Chavez, walipinga uingiliaji wa nchi za nje katika masuala ya ndani ya nchi yao. Hugo Chavez alifariki dunia Machi 5 mwaka 2013 kutokana na maradhi ya saratani akiwa na umri wa miaka 58.