Apr 28, 2022 02:41 UTC
  • Alkhamisi, Aprili 28, 2022

Leo ni Alkhamisii tarehe 26 Ramadhani 1443 Hijria, sawa na Aprili 28 mwaka 2022 Milaadia.

Miaka 30 iliyopita katika siku kama ya leo, makundi ya Mujahidina wa Afghanistan hatimaye yalipata ushindi baada ya mapambano ya miaka 13 dhidi ya jeshi la Urusi ya zamani na serikali kibaraka ya nchi hiyo. Baada ya majeshi ya Urusi ya zamani kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa miaka 13, hatimaye mwezi Februari mwaka 1989 wanajeshi hao wa Urusi walilazimika kuondoka Afghanistan. Hata hivyo kutokana na makundi hayo ya Kiafghani kutokuwa na mikakati mizuri na pia kutopata misaada kutoka nje, vikosi vya serikali ya Afghanistan viliendelea kubakia madarakani chini ya hiyama na misaada ya kifedha na kijeshi wa Urusi ya zamani. Aprili 28 Mujahidina walifanikiwa kuuteka kikamilifu mji wa Kabul na kuiondoa madarakani serikali kibaraka ya Afghanistan.

Tarehe 8 Ordibehesht miaka 34 iliyopita watawala wa kizazi cha Aal Saud walikata uhusiano wa Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya utawala wa Saudia kufanya mauaji ya umati ya mahujaji Wairani wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu mjini Makka katika siku iliyopewa jina la "Ijumaa ya Damu" hapo tarehe 9 Mordad 1366 Hijria Shamsia, uhusiano wa Iran na nchi hiyo ulifika kiwango cha chini zaidi, na wanadiplomasia wa Iran nchini Saudia wakapunguzwa kwa kiasi kikubwa. Wanadiplomasia wa Saudia mjini Tehran walikuwa tayari wamekwishaondoka. Hatimaye uhusiano wa nchi hizi mbili ulikatwa kikamilifu tarehe 28 Aprili 1986. Safari za Wairani waliokuwa na hamu ya kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Makka na Harama tukufu ya Mtume Muhammad (saw) mjini Madina pia zilisimamishwa kwa kipindi cha miaka mitatu. Uhusiano wa nchi hizo mbili ulikatwa katika kipindi ambacho Saudi Arabia ilikuwa msaidizi mkubwa wa kifedha wa utawala wa Saddam Hussein katika vita vyake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hatua hiyo ilichukuliwa sambamba na siasa za Marekani za kubana na kuzidisha mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi dhidi ya Iran.

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita Marekani ililazimika kuondoka kwa madhila huko Vietnam baada ya kupata kipigo cha kuaibisha. Majeshi ya Marekani yaliingia Vietnam kwa shabaha eti ya kukabiliana na kasi ya kuenea ukomunisti na kukabiliwa na mapambano makali ya wapiganaji waliokuwa maarufu kwa jina la Viet Cong huko Vietnam ya Kaskazini. Katika vita hivyo Marekani ilitumia silaha zote zilizopigwa marufuku isipokuwa silaha za nyuklia. Wapiganaji hao wa mwituni walifanikiwa kutoa kipigo kikali kwa majeshi ya Marekani, na tarehe 28 Aprili mwaka 1975 Rais Richard Nixon wa Marekani aliwaamuru wanajeshi wa nchi hiyo kuondoka Vietnam.

Vita ya Vietnam

Na siku kama ya leo miaka 467 iliyopita, Kongamano la Augsburg lilifanyika katika mji wenye jina hilo huko nchini Ujerumani. Katika kongamano hilo, viongozi wa Kikatoliki chini ya uongozi wa Papa Paul IV (wa Nne) kwa mara ya kwanza waliunga mkono uhuru wa madhehebu ya Waprotestanti. Katika kongamano hilo pia ulichukuliwa uamuzi wa kurejeshwa mali za Waprotestanti walizokuwa wamenyang'anywa. Hata hivyo uamuzi huo haukutekelezwa na hilo lilizusha vita vya miaka kumi kati ya Waprotestanti na Wakatoliki katika nchi mbalimbali za Ulaya.

Augsburg