Jun 15, 2022 23:23 UTC
  • Alkhamisi, Juni 16, 2022

Leo ni Alkhamisi, tarehe 16 Dhul-Qaadah mwaka 1443 Hijria, sawa na tarehe 16 Juni mwaka 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1117 iliyopita alizaliwa Sahib Ismail bin Ubbad, mwanafasihi maarufu na msomi wa Kiislamu wa kizazi cha Dailami katika familia ya Kiirani. Sahib alikuwa mwandishi hodari na mtu mwenye hadhi na mashuhuri sana katika zama zake. Licha ya kwamba alikuwa waziri katika serikali ya kizazi cha Dailami, lakini alikuwa mtu mnyenyekevu na mwema kwa watu wa chini yake. Sahib bin Ubbad ameandika vitabu vingi, na maarufu zaidi ni kile cha "al Muhiit" chenye juzuu saba.

Sahib Ismail bin Ubbad

 

##########

Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita Ayatullah Zainul Abidin Mazandarani mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kiirani aliaga dunia. Baada ya kuhitimu masomo ya awali, Ayatullah Mazandarani alielekea katika hauza ya kielimu ya Najaf huko Iraq ili kukamilisha masomo ya kidini. Akiwa huko mwanazuoni huyo alifunzwa na maustadhi wakubwa wa zama hizo wa hauza ya Najaf kama vile Sheikh Murtadha Ansari na kufikia daraja ya juu ya kielimu na kimaanawi.

Ayatullah Zainul Abidin Mazandarani

##########

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita wananchi wa Soweto huko Afrika Kusini walianza harakati za mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa makuburu. Katika kipindi hicho Afrika Kusini ilikuwa ikitawaliwa na wazungu wachache waliodhibiti kila kitu na sheria zilizokuwa dhidi ya binadamu. Juni 16 mwaka 1976 maelfu ya wanafunzi wazalendo walifanya maandamano makubwa kupinga sera za kibaguzi katika sekta ya elimu ambayo yalikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa utawala wa kibaguzi. Mamia ya raia waliuawa na wengine kujeruhiwa.

##########

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita sawa na tarehe 16 Juni 1963, Valentina Tereshkova mwanamke wa kwanza duniani mwanaanga kutoka Russia, alianza safari yake ya angani kwa kutumia safina ya anga iliyoitwa Vostok-6. Mwanake huyo alitua katika orbiti ya ardhi wakati ambao Valery Bykovsky mwanaanga mwingine wa Russia alipokuwa akijishughulisha pia kuzunguka dunia. Safari ya Tereshkova katika anga za juu ilifanyika miaka miwili baada ya safari ya Yuri Gagarin ambayo ilikuwa ya kwanza kufanywa na mwanadamu katika anga hizo. Katika muda wa masaa 70 na dakika 50 aliyokuwa katika anga za juu, Tereshkova alizunguka dunia mara 48.

Valentina Tereshkova

##########

Katika siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, yaani sawa na tarehe 16 Juni mwaka 1944, wanajeshi wa majini wa Marekani waliaza kushambulia kwa mabomu miji ya Japan sambamba na kuulenga mji wa Fokula ulioko kusini mwa nchi hiyo. Hayo yalijiri wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Aidha mashambulizi hayo yalifanyika kwa lengo la kuilazimisha Tokyo isalimu amri. Katika mashambulizi hayo makumi ya maelfu ya raia wa Japan waliuawa na kujeruhiwa, sambamba na kuangamizwa viwanda na mashamba ya nchi hiyo. Vita hivyo vilipelekea Marekani kushambulia kwa mabomu ya nyuklia miji miwili ya Japan ya Hiroshima na Nagasaki mwezi Oktoba mwaka 1945.

Hiroshima baada ya shambulizi la bomu la nyuklia

##########