Ijumaa, Juni 17, 2022
Leo ni Ijumaa, tarehe 17 Dhul-Qaadah mwaka 1443 Hijria, inayosadifiana na 17 Juni mwaka 2022 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1264 iliyopita Imam Mussa al Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa Ahlubait wa Mtume wetu Muhammad (saw) alibaidishwa kutoka Madina na kupelekwa Iraq kwa amri ya mtawala dhalimu, Haroun Rashid. Mtukufu huyo aliwasili Iraq tarehe 7 Dhilhijja 179 Hijria na kufungwa katika jela ya mji huo. Kwa muda, Imam aliwekwa katika jela ya Issa bin Jaafar aliyekuwa mtawala wa Basra lakini mtawala huyo alimwandikia barua Haroun Rashid akimuomba amkabidhi Imam kwa mtu mwingine kwa sababu hakupata ushahidi wowote dhidi ya mtukufu huyo. Haroun Rashid alimpeleka tena uhamishoni Imam mjini Baghdad na akamtaka waziri wake, Fadhl bin Rabi'i amuue mjukuu huyo wa Mtume. Waziri huyo alikataa na hivyo Haroun alimtaka mtu aliyejulikana kwa jina la Yahya bin Khalid Barmaki atekeleze amri hiyo. Hatimaye Imam Kadhim (as) aliuuliwa shahidi na muovu huyo kwa amri ya mtawala Haroun Rashid.

##########
Siku kama ya leo miaka 88 iliyopita alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sheikh Abdulkarim Hairi Yazdi fakihi na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu ambaye aliasisi chuo kikuu cha kidini cha Qum. Alimu huyo alizaliwa katika mji wa Yazd katikati mwa Iran na baada ya kupata elimu ya mwanzo alielekea nchini Iraq ili kuendelea na masomo ambako alipata elimu na maarifa kutoka kwa maulamaa maarufu wa zama hizo na kufikia daraja ya juu ya ijitihad. Ayatullah Hairi Yazdi aliporejea Iran alihisi haja ya kuwepo chuo chenye nguvu cha elimu ya dini na kwa minajili hiyo mwaka 1340 Hijiria Shamsia alinzisha Hauza ya Qum ambayo ni chuo kikuu cha kidini katika mji mtakatifu wa Qum. Hauza ya Qum ilipanuka kwa kasi na hivi sasa ni miongoni mwa vituo muhimu vya elimu katika ulimwengu wa Kiislamu.
##########
Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita sawa na tarehe 17 Juni 1925, ulitiwa saini mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya silaha za vijidudu na kemikali mjini Geneva Uswisi. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utumiaji vitani wa aina yoyote ya silaha za vijidudu, gesi zinazoua, sumu za kemikali na nyinginezo kama hizo ulipigwa marufuku. Licha ya kufikiwa makubaliano hayo, lakini baadhi ya nchi bado ziliendelea kutumia silaha hizo zilizopigwa marufuku duniani. Ujerumani ilitumia silaha za kemikali katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Marekani katika vita vya Vietnam na utawala wa zamani wa Iraq kutumia silaha hizo wakati wa vita vyake vya kichokozi dhidi ya Iran.
##########
Na siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, wakazi wa kisiwa cha Iceland walifanikiwa kupata uhuru wao kutoka mikononi mwa Denmark. Kisiwa cha Iceland kiligunduliwa tarehe 10 Julai 874 Miladia na kuanzia wakati huo, ndipo wahajiri wa Norway, Scotland na Ireland wakaanza kuishi katika kisiwa hicho. Hadi kufikia karne ya 13 Miladia ilikuwa ni nchi huru hata hivyo muda baadaye iliunganishwa na Norway na kisha Denmark. Mwaka 1874 Denmark iliruhusu kuundwa baraza la watunga sheria (yaani bunge) katika kisiwa hicho cha Iceland. Aidha serikali ya ndani ya kisiwa hicho iliendelea kufuatilia haki zake zaidi ingawa bado kiliendelea kutambuliwa kuwa sehemu ya Denmark, hadi tarehe 17 Juni 1944 ambapo kulitangazwa kuvunjwa muungano huo baada ya kurejelewa maoni ya wakazi wa Iceland. Kuanzia wakati huo, wakakazi wa Iceland wanaitambua siku kama ya leo kuwa siku ya kitaifa.