Jun 27, 2022 22:13 UTC
  • Jumanne tarehe 28 Juni mwaka 2022

Leo ni Jumanne tarehe 28 Mfunguo Pili Dhulqaada 1443 Hijria sawa na Juni 28 mwaka 2022.

Tarehe 28 Dhilqaada miaka 1083 iliyopita mwanazuoni wa Kiislamu, Abul Qasim Tabarani, alifariki dunia katika mji wa kihistoria wa Isfahan nchini Iran. Tabarani alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Hadithi wa karne ya nne Hijria na alifanya safari katika nchi nyingi za Kiislamu kwa ajili ya kukusanya Hadithi za Mtume Muuhammad (saw). Alianza kufundisha na kulea wanafunzi wengi baada ya utafiti na uchunguzi wa miaka 33.

Tabarani ameandika vitabu vikubwa vitatu vya Hadithi kwa majina ya Al Muujamul Kabiir", al Muujamul Wasiit na al Muujamus Swaghir.

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, yaani tarehe 28 Juni mwaka 1957, Kituo cha Kiislamu mjini Washington, Marekani kilianzisha rasmi shughuli zake. Ujenzi wa kituo hicho ulianza mwaka 1949 kwa ushirikiano wa Waislamu wa nchi hiyo na baada ya kuanza ujenzi huo mwaka 1957 kiligeuka na kuwa alama yao ya kidini. Kituo cha Kiislamu cha Washington, mji mkuu wa Marekani kinajumuisha msikiti, shule, maktaba na kadhalika. Ratiba na shughuli mbalimbali za kidini zilizokuwa zikifanyika katika kituo hicho ni miongoni mwa mambo yaliyowafutia sana Waislamu na wasiokuwa Waislamu katika eneo hilo muhimu. Shughuli za kituo hicho zilipelekea viongozi wa serikali ya nchi hiyo, kupatwa na wahka na hivyo kusimamisha shughuli zake na hata kukifunga kabisa.

Kituo cha Kiislamu mjini Washington

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita mwafaka na tarehe 7 mwezi wa Tir mwaka 1360 Hijria Shamsiya, Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti aliuawa shahidi akiwa pamoja na watu wengine 72 waliokuwa miongoni mwa shakhsiya bora wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya kuripuliwa kwa bomu ofisi kuu ya chama cha Jamhuri ya Kiislamu. Ayatullah Beheshti pia alikuwa miongoni mwa shakhsiya wa awali waliotoa mchango mkubwa katika Mapinduzi ya Kiislamu. Dakta Beheshti pia alikuwa mmoja kati ya wasaidizi wakuu wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Mlipuko huo wa bomu uliwaua shahidi Dakta Beheshti na wasaidizi 72 wa Imam Khomeini wakiwemo mawaziri na wabunge kadhaa.

Shamsiya, Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti

Miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo mji wa Sardasht huko magharibi mwa Iran ulishambuliwa kwa mabomu ya kemikali na ndege za kivita za utawala wa zamani wa Iraq. Raia wasio na ulinzi 110 wa Iran wakazi wa mji huo waliuawa shahidi na wengine 530 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya utawala wa zamani wa Saddam Hussein. Utawala wa Saddam ambao ulikuwa umekata tamaa ya kupata ushindi katika medani za vita dhidi ya Iran ulikuwa ukidhani kwamba kwa kufanya mashambulizi yake hayo ya kemikali dhidi ya raia wa mji wa Sardasht ungeweza kulitwisha taifa la Iran matakwa yake. Taasisi muhimu za kimataifa na madola makubwa duniani hata hivyo hazikuchukua hatua yoyote ya jadi ya kuuzuia utawala wa Saddam kutumia silaha za kemikali wala hata kulaani jinai hizo ulizozifanya dhidi ya raia wasio na hatia wa Iran. 

Na siku kama ya leo miaka 15 iliyopita sawa na tarehe 28 mwezi Juni mwaka 2006 jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulio makubwa dhidi ya watu wa Ukanda wa Ghaza. Utawala wa Kizayuni uliendesha mashambulio hayo ya kinyama kwa kisingizio cha kuuawa wanajeshi wake wawili siku tatu kabla ya mashambulio hayo. Israel ilidai kuwa wanamapambano wa Palestina walifanya oparesheni katika kituo kimoja cha upekuzi na kuua wanajeshi wake wawili na kumkamata mateka mwingine mmoja. Idadi kadhaa ya mawaziri, wabunge na wawakilishi wa baraza la mji la serikali halali ya Palestina inayoongozwa na Hamas walitekwa nyara na wanajeshi wa Israel katika siku za kwanza za mashambulizi hayo makubwa ya jeshi yaliyopewa jina la "Mvua za Kiangazi". Mbali na hayo, mamia ya raia madhlumu wa Palestina waliuawa shahidi na kujeruhiwa katika mashambulizi ya kinyama ya anga na nchi kavu ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza.

Gaza