Jumatano tarehe 6 Julai 2022
Leo ni Jumatano tarehe 06 Dhulhija 1443 Hijria sawa na Julai 6 mwaka 2022.
Siku kama ya leo miaka 1185 iliyopita, yaani tarehe 6 Dhul-Hijja mwaka 258 Hijria, alizaliwa Abu Ali Muhammad ibn Hammam, mmoja wa maulama mashuhuri wa Iran. Ibn Hammam alikuwa akiishi mjini Baghdad, Iraq ambapo alifanikiwa kusoma elimu ya hadithi kutoka kwa maulama wakubwa wa enzi zake. Aidha msomi huyo alikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao walijifunza toka kwake elimu ya hadithi na elimu nyingine za Kiislamu. Msomi huyo ameacha vitabu kadhaa katika uga wa hadithi.

Katika siku kama ya leo miaka 168 iliyopita, alifariki dunia George Simon Ohm mwanahisabati na mwanafizikia wa Ujerumani akiwa na umri wa miaka 67. Simon Ohm alizaliwa mwaka 1789 na kuanza kupenda sana somo la fizikia na kufanikiwa kuvumbua kanuni katika uwanja wa umeme kutokana na utafiti mkubwa aliokuwa akiufanya katika uwanja huo. Alizipa kanuni hizo jina lake yaani "Ohm Laws". Kanuni ambazo zinatumiwa hadi leo hii.
Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia mwandishi wa Kimarekani kwa jina la William Faulkner. William alizaliwa mwaka 1897. Baada ya kushiriki katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Faulkner alirejea tena nchini kwake. Alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake, Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili Wamarekani wenye asili ya Afrika. Hadithi za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa leo nchini Marekani.
Tarehe 6 Julai miaka 58 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Malawi ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kabla ya Malawi kupata uhuru, ilikuwa ikijulikana kwa jina la Nyasaland. Mwaka 1859, makundi ya Wamishonari kutoka Scotland wakiwa pamoja na mvumbuzi David Livingstone waliwasili Nyasaland na kufuatiwa na Uingereza. Uingereza iliunga mkono uvamizi wa Ujerumani na Ureno huko Nyasaland na hatimaye mwaka 1891 nchi hiyo ikawekwa chini ya mamlaka yake. Kwa utaratibu huo Nyasaland ambayo ni Malawi ya leo ikawa miongoni mwa makoloni ya Uingereza katika eneo la Mashariki mwa Afrika. Kijiografia Malawi iko kusini mashariki mwa Afrika ikipakana na nchi za Tanzania, Zambia na Msumbiji.
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, visiwa vya Comoro vilipata uhuru. Raia wengi wa visiwa vya Comoro walianza kuingia katika dini ya Kiislamu na kueneza utamaduni wa dini hiyo visiwani humo, baada ya wafanya biashara wa Kiislamu kuwasili visiwani humo katika karne ya 12 Miladia. Tangu karne ya 16 visiwa vya Comoro vilikuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno na baadaye Sultan wa Oman alifanikiwa kuhitimisha ukaliwaji mabavu wa visiwa hivyo. Hata hivyo mwaka 1842 sehemu kadhaa za visiwa hivyo ziliingia chini ya udhibiti wa Wafaransa na taratibu wakoloni hao wakaidhibiti ardhi yote ya nchi yote hiyo. Mapambano ya wananchi yalipelekea kutangazwa uhuru rasmi wa nchi ya Kiislamu ya Comoro mwaka 1975. Comoro ina ukubwa wa kilomita mraba 1862 na kijiografia inapatikana kusini mashariki mwa bara la Afrika katika bahari ya Hindi.
Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, mamia ya mahujaji wa Iran na wengine kutoka nchi tofauti waliokuwa wameenda kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu mjini Makka na wakiwa katika hali ya kutekeleza ibada ya faradhi ya kujitenga na washirikina, waliuawa shahidi na askari wa utawala wa Saudi Arabia. Ni vyema kukumbusha kuwa, mahujaji wa Iran kwa miaka yote huwa wanatekeleza ibada hiyo kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo mbali na kuwasisitizia Waislamu kuungana, hutangaza kujitenga na maadui wa Uislamu hususan Marekani na utawala haramu wa Israel. Ibada hiyo ambayo hufanyika kwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, huwa na taathira kubwa katika msimu wa Hija. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akasisitiza sana umuhimu wa ibada ya kujitenga na mushrikina na maadui wa dini ya Kiislamu.
Na miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sayyid Javad Khamenei, baba wa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Alizaliwa katika mji wa Khamenei karibu na Tabriz huko Azerbaijan Mashariki na akaondokea kuwa alimu na fakihi kupitia malezi ya baba yake. Akiwa katika rika la ujana, Sayyid Javad Khamenei alifanya safari katika maeneo matakatifu na akauchagua mji mtakatifu wa Mash’had kuwa makazi yake ya kudumu. Akiwa mjini Mash’had alisoma masomo ya Hawza kwa Ayatullah Aghazadeh Khorasani na al Haj Hussein Qumi na kukwea daraja za kielimu. Aidha akiwa na nia ya kujiendeza zaidi kielimu alifanya safari huko Najaf Iraq na kufanikiwa kusoma kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo kama Ayatullah Mirza Naini na Abul-Hassan Isfahani. Hatimaye Sayyid Javad Khamenei aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 91 na kuzikwa jirani na haram ya Imam Ridha AS.