Jumamosi tarehe 16 Julai 2022
Leo ni Jumamosi tarehe 16 Dhulhija 1443 Hijria sawa na 16 Julai 2022.
Miaka 972 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Abu Abdullah Muhammad bin Jiyani, mnajimu na mwanahisabati wa Kiislamu huko Andalusia. Alizaliwa mwaka 379 Hijiria huko Cordoba moja ya miji ya kale ya Uhispania na alisoma hadi kuhitimu katika mji huo huo. Baada ya hapo alikwenda katika mji mkuu wa Misri, Cairo na kuishi huko kwa miaka minne. Jiyani alikuwa mahiri mkubwa katika elimu ya nujumu na miongoni mwa athari za mwanahisabati huyo ni kitabu chake cha nujumu ambacho kimetajwa katika makala ya 5 ya kitabu cha elementi cha baba wa jiometri, Euclid wa Ugiriki ya kale.

Siku kama ya leo miaka 132 iliyopita James Parkinson aligundua ugonjwa wa Parkinson na namna unavyotokea. Kwa sababu hiyo ugonjwa huo ulipewa jina la tabibu huyo. Dalili za ugonjwa huo ni kama vile kutetemeka sana na kwa muda mrefu kwa ulimi, kichwa na mikono na kushindwa kuvuta miguu wakati wa kutembea hususan katika kipindi cha uzeeni na pia kukakamaa misuli katika sehemu yoyote ya mwili. Ugonjwa wa Parkinson unasababishwa na baadhi ya matatizo katika ubongo na hadi kufikia sasa hakuna dawa mujarabu iliyopatikana kwa ajili ya kutibu maradhi hayo.
Miaka 77 iliyopita katika siku kama hii ya leo bomu la kwanza la nyuklia la Marekani liliripuliwa wakati wa majaribio. Marekani ilifanya jaribio hilo la bomu la nyuklia ili kujiandaa kuishambulia Japan kwa kutumia mabomu hayo. Wakati huo Japan ilikuwa ikipigana na madola makubwa na majeshi ya nchi waitifaki, ikiwemo Marekani.
Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon kwa mara nyingine tena ilifanikiwa kupokea mateka watano na miili ya karibu mashahidi 200 wa Kilebanoni kutoka kwa utawala wa Kizayuni. Ubadilishanaji huo wa miili na mateka hao ulifanyika kufuatia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya pande mbili hizo kwa usimamizi wa serikali ya Ujerumani. Nukta ya kushangaza katika oparesheni hiyo ni hii kwamba vyombo vya usalama na ujasusi vya utawala wa Kizayuni hadi dakika ya mwisho havikuwa na habari kwamba wanajeshi wake wawili waliuawa mwanzoni mwa mapigano kati ya jeshi la utawala wa Kizayuni na wapiganaji wa Huzbullah. Shakhsia wengine kutoka makundi ya mapambano ya Lebanon pia walikuwa miongoni mwa mateka walioachiwa huru na utawala wa Kizayuni. Shakhsia muhimu zaidi kuliko wote alikuwa Samir Qantar ambaye alipoteza karibu miaka 30 ya umri wake akiwa katika jela za utawala wa Kizayuni.
Na katika siku kama hii ya leo miaka 7 iliyopita alifariki dunia qarii mashuhudi wa Misri, Sheikh Sayyid Mutawalli Abdul Aal. Alizaliwa Aprili 1947 katika familia ya wachamungu nchini Misri na aliweza kuhifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu akiwa na umri wa miaka 12.
Alianza kujifunza qiraa ya Qur'ani Tukufu kwa kuiga mitindo ya maustadhi bingwa kama vile Sheikh Abdulbasit Abdusamad na Sheilh Mustafa Ismail.
Katika umri wake uliojaa baraka za Qur'ani, Sayyid Mutawalli Abdul Aal alitembelea nchi nyingi duniani kama qarii na pia jaji wa mashindano ya Qur'ani. Alifariki Julai 16, 2015 akiwa na umri wa miaka 68.