Jul 28, 2022 21:53 UTC
  • Ijumaa, Julai 29, 2022

Leo ni Ijumaa tarehe 29 Mfunguo Tatu Dhulhija 1443 Hijria sawa na 29 Julai mwaka 2022.

Katika siku kama ya leo miaka 139 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 29 Julai 1883, alizaliwa Benito Mussolini mwanasiasa,  dikteta na mwasisi wa chama cha Kifashisti nchini Italia. Ufashisti ni utawala wa kidikteta uliojikita katika kuleta aidolojia ya kibaguzi na kiutaifa, kuwakandamiza wapinzani na kupotosha itikadi na fikra za wananchi. Mwaka 1922 Mussolini alinyakua wadhifa wa uwaziri mkuu wa Italia, na hivyo udikteta kuendelea kutawala nchini humo. Muda mfupi baadaye Mussolini alishirikiana na Adolph Hitler na kuandaa mazingira ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia.

Benito Mussolini

Miaka 105 iliyopita katika siku kama hii ya leo inayosadifiana na tarehe 29 Dhulhija mwaka 1338 Hijria aliuawa shahidi Sheikh Muhammad Khiyabani, mwanamapambano na mpigania uhuru na kujitawala wa Iran. Alizaliwa mwaka 1297 Hijria Shamsia katika eneo la Khamene katika mkoa wa Azarbaijan Mashariki. Sheikh Khiyabani alianzisha harakati za kupinga dhulma na ukandamizaji zilizokuwa zikifanywa na tawala za silsila ya Qajar hapa nchini. Baada ya kuusambaratisha udikteta wa Muhammad Ali Shah Qajar na kumlazimisha mtawala huyo kukimbia mwaka 1287 Hijria Shamsia, wananchi wa Tabriz walimchagua Sheikh Muhammad Khiyabani kuwa mwakilishi wao katika Bunge la Taifa. Hata hivyo katika siku kama ya leo Sheikh Khiyabani alikamatwa na kuuawa shahidi, wakati alipokuwa akipambana na askari wa serikali ya kifalme.

Sheikh Muhammad Khiyabani

Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 29 Julai 1957, Umoja wa Mataifa ulianzisha Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA. Lengo la kuanzishwa taasisi hiyo ya kimataifa, ni kusimamia shughuli zote za mitambo ya nyuklia na kuhakikisha kwamba miradi ya nyuklia duniani inatekelezwa kwa njia za amani na kutotumika kwa malengo ya kijeshi na  utengenezaji wa silaha za mauaji ya halaiki.

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita Abul Hassan Bani Sadr, rais aliyeuzuliwa wa Iran alikimbia nchi akiwa pamoja na kiongozi wa kundi la Munafiqin la MKO, Mas'ud Rajavi. Siku 37 kabla yake Bani Sadr alikuwa ameuzuliwa cheo cha rais kutokana na kukosa ustahiki, kuzusha machafuko nchini na kushindwa kulinda nchi mbele ya hujuma za utawala wa Saddam Hussein. Bani Sadr alikuwa na matumaini kwamba, mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa na kundi la MKO yangeweza kumrejesha tena madarakani. Hata hivyo kuchaguliwa Muhammad Rajai kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu kulimvunja moyo Bani Sadr ambaye aliamua kukimbilia Ufaransa akiwa amevaa nguo za kike.

Bani Sadr na Rajavi