Jumamosi, Julai 30, 2022
Leo ni tarehe Mosi Mfunguo Nne Muharram mwaka 1444 Hijria sawa na tarehe 30 Julai 2022.
Tarehe Mosi Muharram inasadifiana na kuanza mwaka mpya wa Hijria Qamaria. Mwaka wa Hijria Qamaria unahesabiwa kwa mujibu wa mzunguko wa mwezi na katika nchi nyingi za Kiislamu unatumiwa kwa ajili ya masuala ya kidini au hata kijamii. Mwaka wa Hijria Qamaria pia unatumika katika masuala mengi ya kiibada kama vile kuainisha mwanzo wa funga ya mwezi wa Ramadhani, Hija, kuainisha miezi mitakatifu na kwa ajili ya historia ya matukio mbalimbali. Mwaka wa Hijria ulianzishwa katika zama za utawala wa Khalifa Umar bin Khattab kutokana na ushauri uliotolewa na Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) ambaye aliagiza mwanzo wa hijra ya Mtume kutoka Makka na kwenda Madina uwe mwanzo wa mwaka wa Kiislamu. Kabla ya kalenda ya Miladia kutumika kote duniani, nchi nyingi za Kiislamu zilikuwa zikitumia kalenda ya Hijria Qamaria.

Tarehe 8 mwezi Mordad kwa mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi mwanafalsafa, arifu na msomi mkubwa wa Kiislamu, Shahabuddin Sohravardi aliyepewa lakabu ya Sheikhul Ishraq. Sheikhul Ishraq alizaliwa mwaka 549 Hijria karibu na mji wa Zanjan kaskazini magharibi mwa Iran. Alibobea haraka katika taaluma nyingi za Kiislamu za wakati huo hususan falsafa. Sheikh Sohravardi alifanya safari katika miji mbalimbali ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya kutafuta elimu. Aliasisi mfumo mpya wa falsafa uliopewa jina la Ishraq. Sheikhul Ishraq ameandika vitabu vingi kama vile "Hikmatul Ishraq", al Mabda wal Maad", na "Talwihat".
Siku kama ya leo miaka 124 iliyopita, alifariki dunia Otto von Bismarck, Kansela wa kwanza na mwanasiasa mkongwe wa Ujerumani. Bismarck aliongoza vita vitatu ambavyo viliainisha mustakbali wa Ujerumani kama nchi huku akikabiliana pia na madola ya Ulaya wakati huo. Bismarck alikuwa rais wa Prussia akiwa na umri wa miaka 28 na kwa mara ya kwanza akawa pia Kansela wa Ujerumani. Mwaka 1862 aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa Prussia na kuanzisha mpango wa Ujerumani moja. Ili kufikia lengo hilo hakuwa na njia nyingine ghairi ya kuiondoa Austria katika shirikisho la majimbo ya Ujerumani ya Kikatoliki sambamba na kulikomboa jimbo la Schleswig-Holstein kutoka udhibiti wa Denmark na kuhitimisha upenyaji wa Ufaransa katika majimbo ya kusini mwa Ujerumani. Baada ya kujiimarisha kijeshi alipigana vita vitatu na kufikia malengo yake katika vita vyote hivyo. Kwa mujibu wa historia, Otto von Bismarck alizishinda nchi za Denmark, Austria na Ufaransa, kulikoenda sambamba na kuteuliwa kuwa kansela wa Ujerumani mwaka 1890.
Tarehe 30 Julai miaka 75 iliyopita alifariki dunia mvumbuzi wa Kimarekani anayejulikana kama baba wa sekta ya utengenezaji magari wa nchi hiyo Henry Ford. Alizaliwa tarehe 30 Julai 1863 katika familia ya kimaskini na tangu utotoni alikuwa na hamu kubwa ya masuala ya mekaniki. Siku moja Ford aliona gari likitembea barabarani bila ya kuvutwa na farisi na akaamua kutengeneza gari lake mwenyewe. Henry Ford alifanyia majaribio mkokoteni wa kwanza usiotumia farasi akiwa na umri wa miaka 12 tu. Mvumbuzi huyo aliboresha zaidi mkokoteni huo na mwaka 1896 alifanikiwa kutengeneza gari lake la kwanza. Mwaka 1895 alipewa haki ya kutengeneza magari licha ya kwamba watu wengine pia walikuwa wanatengeneza chombo hicho na mwaka 1903 aliasisi kampuni ya magari ya Ford Motor. Ford aliwapiku watengeneza magari wengine kwa kutengeneza magari mengi ya bei rahisi.
Na Katika siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Ali Akbar Faydh mashuhuri kwa jina la Ayatullah Mishkini. Ayatullah Mishkini alisoma kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo kama Ayatullah Burujerdi na Imam Khomeini. Alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kujiunga na harakati ya mapambano ya Imam Khomeini dhidi ya utawala wa Shah. Alitiwa nguvuni na kufungwa jela mara kadhaa sambamba na kubaidishwa. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Mishkini alishika nyadhifa mbalimbali, na muhimu zaidi ni ule wa Mwenyekiti wa Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu na Kusimamia Kazi Zake. Alimu huyo ameandika vitabu vingi.