Jul 30, 2022 22:57 UTC
  • Jumapili, Julai 31, 2022

Leo ni Jumapili tarehe Pili Mfunguo Nne Muharram 1444 Hijria sawa na Julai 31 mwaka 2022 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita yaani tarehe Pili Muharram mwaka 61 Hijria, Imam Hussein AS, mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na familia na masahaba zake waliwasili katika ardhi ya Karbala katika Iraq ya leo. Miezi kadhaa kabla ya hapo, Imam Hussein AS aliondoka katika mji mtakatifu wa Madina na kuelekea Makka akilalamikia utawala wa kimabavu wa Yazid bin Muawiya na baadaye akaelekea katika mji wa Kufa huko Iraq. Japokuwa watu wa Kufa mwanzoni waliunga mkono mapambano ya Imam Hussein na kumwalika katika mji huo, lakini waliacha kumuunga mkono mjukuu huyo wa Mtume kutokana na hofu na vitisho vya utawala wa Yazid bin Muawiya. Jeshi la Yazidi mlaaniwa liliuzuia msafara wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) kuingia katika mji wa Kufa na kuzingirwa katika jangwa na Karbala.

Tarehe 31 Julai miaka 216 iliyopita ardhi ya Cape huko kusini mwa bara la Afrika ilivamiwa na wanajeshi wa Uingereza. Ardhi ya Cape au mji wa Cape Town ni sehemu ya kusini ya nchi ya Afrika Kusini iliyoko pembeni ya Rasi ya Tumaini Jema au (Cape of Good Hope) ambayo ipo kati ya Bahari za Atlantic na Hindi. Eneo hilo lina utajiri mkubwa wa dhahabu na almasi na ni kwa sababu hiyo ndiyo maana daima wakoloni wakawa wanalikodolea jicho la tamaa.

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita aliaga dunia Antoine de Saint-Exupery mwandishi na mwanaanga wa Kifaransa katika Vita vya Pili vya Dunia baada ya ndege yake kuanguka. Exupery alizaliwa mwaka 1900 katika mji wa Lyon nchini Ufaransa. Mwandishi Antoine de Saint Exupery alijishughulisha na masuala ya kusafiri angani kutokana na kupenda sana fani hiyo. Alijiunga na jeshi la Ufaransa katika Vita vya Pili vya Dunia na kuwa afisa wa masuala ya usafirishaji wa posta. Siku hiyo Antoine de Saint Exupery alirusha ndege hewani akiwa katika kazi zake za kawaida, lakini ndege yake ilitoweka na mabaki ya mwili wake na ndege hiyo hvijaonekana hadi leo hii. Mwandishi huyo ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwao ni "The Little Prince", "Southern Mail" na "Night Flight."

Antoine de Saint Exupery

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita kiongozi wa Waislamu weusi wa Marekani, Elijah Muhammad alitoa wito wa kuundwa dola la watu weusi nchini Marekani chini ya usimamizi wa serikali ya Federali ya nchi hiyo. Lengo la kutolewa fikra hiyo lilikuwa kukomboa Wamarekani weusi kutoka kwenye siasa za ubaguzi wa kimbari na kizazi nchini Marekani. Elijah Muhammad mwenyewe ambaye aliathiriwa na kiongozi mwingine wa Waislamu weusi wa Marekani kwa jina la la Wallace Fard Muhammad na kuwa Muislamu, alikuwa mmoja kati ya watu waliokuwa na taathira kubwa katika harakati hiyo ya kudai dola la Wamarekani weusi. Elija Muhammad aliasisi chama cha Umma wa Uislamu (Nation of Islam) na kujenga misikiti na vituo kadhaa kwa ajili ya Waislamu wa Marekani. Hata hivyo baadhi ya wanachama wa harakati hiyo ya Waislamu weusi wa Marekani kama Malcolm X walikataa na kupinga baadhi ya itikadi za kidini na siasa za Elijah Muhammad.

Elijah Muhammad