Jumatatu tarehe Mosi Agosti 2022
Leo ni Jumatatu tarehe 3 Mfunguo Nne Muharram 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe Mosi Agosti 2022.
Siku kama ya leo miaka 1437 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, inayosadifiana na tarehe 3 Muharram mwaka wa 7 Hijria, Mtume Muhammad SAW aliwatumia barua wafalme wa tawala mbalimbali duniani na kwa hatua hiyo akawa ameanza rasmi kuwalingania watu Uislamu kimataifa. Baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani kati ya Mtume SAW na washirikina wa Makka huko Hudaibiya, Mtume Muhammad SAW alipata fursa ya kuwalingania dini ya Uislamu viongozi wa tawala kubwa duniani bila wasi wasi. Wanahistoria wanasema kuwa, Mtume aliandika barua 12 hadi 26 kwa watawala mbalimbali katika kipindi hicho wakiwamo watawala wa Roma, Iran, Uhabeshi, Bahrain, Yemen na maeneo mengine makubwa katika zama hizo ambapo kila mmoja kati ya watawala hao alionesha radimalia yake. Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu ilionesha wazi kuwa dini ya Kiislamu inalingania haki kwa kutumia mantiki na hoja madhubuti.
Miaka 1383 iliyopita yaani tarehe 3 Muharram mwaka 61 Hijria, jeshi la Umar bin Saad liliwasili katika ardhi ya Karbala. Baada ya Hurr bin Yazid kumzingira Imam Hussein AS na maswahaba zake katika ardhi ya Karbala na kuwazuia wasisonge mbele, Ubaidullah bin Ziyad aliyekuwa kibaraka wa Yazid huko Kufa alikabidhi jukumu la ukamanda wa jeshi la Yazid kwa Umar bin Saad alikuwa na jeshi na wapiganaji elfu nne. Umar bin Saad alikubali kuongoza jeshi la kumuua mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), watu wa familia yake na masahaba zake kwa sharti la kupewa utawala wa eneo kubwa la Rei, ndoto ambayo alikwenda nayo kaburini.

Siku kama ya leo miaka 615 iliyopita, alizaliwa Ibn Khallouf mtaalamu wa fasihi, mwandishi na malenga mkubwa wa Kiislamu. Akiwa kijana mdogo alifanya safari mjini Makkah na baadaye Quds, Palestina huku akisafiri pia mjini Cairo, Misri baada ya kuwa ni kijana. Lengo la safari hizo ilikuwa ni kwa ajili ya kutafuta elimu kiasi kwamba, akiwa na umri wa miaka 26 alihesabika kuwa mmoja wa wasomi wakubwa katika vyuo vikubwa vya nchini Misri. Mbali na hayo ni kwamba Khallouf alikuwa akisoma pia mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad (saw) na watu wa familia yake. Hadi leo turathi za msomi huyo zipo katika maktaba za Bairut, Lebanon na Damascus, Syria.

Katika siku kama ya leo mika 47 iliyopita, mkutano wa wakuu wa Urusi ya zamani, Marekani na Canada na nchi za Ulaya isipokuwa Albania ulianza huko Helsinki mji mkuu wa Finland. Mkutano huo ambao ulipewa jina la Mkutano wa Usalama na Ushirikiano wa Ulaya ulifanyika kwa lengo la kuondoa mivutano kati ya nchi za kambi ya Mashariki chini ya uongozi wa Urusi ya zamani na kambi ya Magharibi chini ya uongozi wa Marekani. Hata hivyo mkutano huo wa usalama na ushirikiano haukuwa na mafanikio muhimu katika kuzikurubisha pamoja kambi mbili hizo hasa kufuatia uvamizi uliofanywa na Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani nchini Afghanistan mwaka 1979.

Miaka 17 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe Mosi Agosti mwaka 2005, Fahd bin Abdulaziz mfalme wa zamani wa Saudi Arabia alifariki dunia baada ya kuugua kwa miaka mingi. Mfalme Fahd alizaliwa mwaka 1921 huko Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia. Mwaka 1967, Fahd bin Abdulaziz alikuwa Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo na miaka minane baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia. Alichukua hatamu za uongozi mwaka 1982 akiwa mfalme wa tano wa silsila ya Aal-Saud baada ya kufariki dunia kaka yake, Khalid bin Abdulaziz. Wakati wa vita vya kichokozi vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran, Mfalme Fahd alikuwa akimuunga mkono dikteta Saddam.
Tarehe Mosi Agosti ni Siku ya Kimataifa ya Maziwa ya Mama. Utumiaji mkubwa wa maziwa ya kopo na vyakula vya watoto vilivyotengenezwa viwandani ulikithiri sana baada ya Vita vya Pili vya Dunia hususan katika nchi zilizostawi na suala hilo limezidisha wasiwasi wa jamii ya kimataifa. Hivyo suala la kunyonyesha watoto kwa maziwa ya mama na kuzidisha uelewa wa umma kuhusu faida kubwa na za aina yake za maziwa ya mama kwa mtoto na katika usalama na afya yake lilihitajia kuchukuliwa hatua kubwa na za kimsingi. Kwa msingi huo Shirika la Afya Duniani (WHO) likishirikiana na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) tarehe Mosi Agosti mwaka 1990 ziliitisha mkutano katika mji wa Florence nchini Italia na kutia saini taarifa iliyosisitiza udharura wa kudumishwa, kutangaza na kusisitiza suala la kuwalisha watoto wadogo kwa maziwa ya mama. Taarifa hiyo ilitilia mkazo umuhimu wa mtoto kunyonyeshwa maziwa ya mama katika kipindi cha miezi sita ya awali ya maisha yake na taathira yake kubwa kwa afya ya mtoto na mama.
