Sep 27, 2022 02:15 UTC
  • Leo ni Jumanne tarehe 27 Septemba 2022

Leo ni Jumanne tarehe 30 Safar 1444 Hijria sawa na 27 Septemba 2022.

Katika siku ya mwisho ya mwezi wa Safar miaka 1240 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Ali bin Mussa ar Ridha AS, mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu SAW. Mtukufu huyo alizaliwa mwaka 148 Hijria katika mji wa Madina na alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Mussa al Kadhim AS. Mnamo mwaka 200 Hijria, Maamun, Khalifa wa Bani Abbasi, alimtaka Imam Ridha AS aelekee kwenye makao ya Khalifa huyo yaliyokuwa katika mji wa Marwi, kusini mashariki mwa Turkemenistan ambayo ilikuwa sehemu ya Khorasan Kuu. Ijapokuwa kidhahiri Maamun alimfanya Imam Ridha kuwa mrithi wake, lakini kwa njia hiyo alikusudia kuimarisha zaidi nguvu za utawala wake. Utukufu na daraja ya juu ya kielimu na kimaanawi aliyokuwa nayo Imam Ridha na ushawishi wake uliokuwa ukiongezeka siku hadi siku ndani ya fikra na nyoyo za watu, vilimtia woga na hofu Maamun, na hivyo akaamua kufanya njama za kumpa sumu na kumuua shahidi Imam Ridha katika siku kama leo. Imam AS amesema:"Mja bora zaidi ni yule ambaye kila anapofanya jema hufurahia, na kila anapokosea huomba msamaha, inapomfikia neema hushukuru, anapokumbana na masaibu husubiri na wakati anapoghadhibika husamehe".

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, mji wenye jamii kubwa ya watu wa Beijing ulichaguliwa rasmi kuwa mji mkuu wa Uchina. Mji wa kihistoria wa Beijing unapatikana mashariki mwa nchi hiyo na unahesabiwa kuwa moja ya vituo vikubwa vya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni nchini China. Beijing ilichaguliwa kuwa mji mkuu wa China baada ya Mao Tse-tung kuchukua madaraka ya nchi na kiongozi wa wakati huo wa China Chiang Kai-shek kulazimika kukimbilia Taiwan.

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita wapiganaji shujaa wa Iran walifanikiwa kuvunja mzingiro wa mji wa Abadan katika operesheni ya haraka na iliyokuwa imeratibiwa vyema dhidi ya ngome za jeshi la Saddam Hussein wa Iraq. Operesheni hiyo ilitekelezwa na wapiganaji wa Iran kufuatia agizo la kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu Amrehemu. Mji wa Abadan ulikuwa umezingirwa na wanajeshi wa Iraq kwa karibu mwaka mmoja tangu kuanza vita vya kulazimishwa vya utawala wa dikteta Saddam dhidi ya Iran.

Tarehe 27 Septemba inasadifiana na Siku ya Kimataifa ya 'Utalii. Utalii ni moja ya sekta muhimu za mabadilishano ya kiutamaduni baina ya watu wa mataifa mbalimbali. Aidha utalii unaweza kutimia kupitia safari na utalii wa ndani na nje ya nchi kwa madhumuni tofauti. Licha ya kwamba utalii umekuwa na historia ya muda mrefu katika maisha ya mwanadamu, lakini utalii wa mfumo wa kisasa ulianza mwanzoni mwa karne ya 16, wakati yaliposhika kasi mapinduzi ya kiviwanda barani Ulaya na kuvumbuliwa aina mpya ya maisha barani humo. Ni kuanzia karne ya 17 ndipo istilahi ya utalii ilipoenea zaidi hasa katika jamii ya watu wa Ufaransa.