Ijumaa tarehe 11 Novemba 2022
Leo ni Ijumaa tarehe 16 Mfunguo Saba Rabiuthani 1444 Hijria sawa na tarehe 11 Novemba 2022.
Siku kama ya leo miaka 133 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 68 Ayatullah Mullah Ahmad Khoeiini Qazvini, mtaalamu wa sheria za Kiislamu (fiqhi), mtafiti na mtaalamu wa Hadithi wa Kishia. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi alielekea Qazvin na baada ya hapo alielekea Isfahan kwa ajili ya masomo ya juu. Baada ya kustafidi na maulama wakubwa wa mji wa Isfahan alifanya ziara katika maeneo matakatifu nchini Iraq ambapo alikaa miaka kadhaa akijiendeleza kimasomo. Alirejea Qazvin na kuanza kazi ya ufundishaji na kutoa fatwa. Ayatullah Mullah Ahmad Khoeiini Qazvini ameacha athari kadhaa kama vile 'Mi’raajul-Wusuuli ila ilmil-Usuul’ chenye juzuu mbili, ‘Lawaamiu fil-Fiqhi’ chenye juzuu tatu na ‘Mir-atul-Muraadi fi Ilmir-Rijaal.’
Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, Vita vya Kwanza vya Dunia vilifikia kikomo baada ya kutiwa saini mkataba wa kuacha vita hivyo. Vita vya Kwanza vya Dunia vilipiganwa kuanzia mwaka 1914 hadi 1918 kati ya nchi waitifaki yaani serikali za Russia, Uingereza, Ufaransa na Italia kwa upande mmoja, na nchi za Ujerumani, Bulgaria, Utawala wa Othmania na ufalme wa Austria na Hungary kwa upande wa pili. Watu zaidi ya milioni 15 waliuawa katika vita hivyo na wengine milioni 20 kujeruhiwa. Vilevile vilisababisha hasara inayokadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 150 kwa nchi zilizopigana vita hivyo.
Katika siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, virusi vinavyosababisha maradhi hatari ya kupooza viungo vya miili ya watoto yaani Polio, viligunduliwa. Virusi hivyo vilipewa jina la virusi vinavyolemaza watoto kwa sababu ya kuwashambulia zaidi watoto wadogo na kuwapoozesha viungo vyao vya mwili. Baadaye kidogo mwanasayansi Dakta Jonas Salk aliyegundua virusi vya Polio alifanikiwa pia kugundua chanjo yake.
Miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo, Angola ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno. Wakoloni wa Kireno kwa mara ya kwanza waliingia katika ardhi ya Angola mwaka 1483 Miladia. Wakati huo, ardhi ya Angola ilikuwa sehemu ya ufalme wa Kongo, Zaire ya zamani.
Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, aliaga dunia Yasser Arafat Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) katika hospitali moja mjini Paris, Ufaransa. Alizaliwa mwaka 1929 na kuanza harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Israel akiwa katika rika la ujana. Mwaka 1946, Yasser Arafat alielekea nchini Misri kwa ajili ya masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Cairo na miaka mitano baadaye alihitimu masomo katika taaluma ya Usanifu Majengo. Mwaka 1965 alirejea Palestina na kuasisi Harakati ya Fat-h ili kupambana na utawala wa Tel Aviv. Miaka minne baadaye alichukua hatamu za kuongoza PLO hadi alipoaga dunia.