Nov 20, 2022 22:55 UTC
  • Jumatatu, Novemba 21, 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 26 Mfunguo Saba Rabiuthani 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 21 Nevemba 2022 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 979 iliyopita, alizaliwa huko Marv, moja ya miji ya Khurasan ya zamani ulioko Turkmenistan ya sasa, Ainuz-Zaman Qatwan Marvazi, mtaalamu wa hesabati, tabibu na mwanafalsafa wa Kiislamu. Qatwan Marvazi alikuwa na umahiri mkubwa katika elimu za hesabati, falsafa, fasihi na elimu ya dini ya Kiislamu. Hata hivyo binafsi alipendelea sana elimu ya tiba. Marvazi ambaye alikuwa akijishughulisha na kutoa huduma ya tiba katika mji wa Marv aliandika vitabu kadhaa na moja ya vitabu hivyo ni 'Kaihaan Shenakht' ambacho kinahusu elimu ya hesabati. Ainuz-Zaman Qatwan Marvazi alifariki dunia mwaka 548 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 926 iliyopita alifariki dunia Hassan al-Sabbah mwasisi wa utawala wa Ismailiyah nchini Iran. Sabbah alizaliwa mwaka 445 Hijiria mjini Qum na akiwa mtoto pamoja na familia yake alielekea mjini Ray, kusini mwa mji wa Tehran. Akiwa mjini hapo alijifunza masomo ya dini ya Kiislamu na Ushia. Hata hivyo akiwa kijana alijiunga na madhehebu ya Ismailiyah. Wafuasi wa kundi hilo kinyume na Mashia wengine baada ya Imam Swadiq (as) walikataa kumtambua mtoto wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) yaani al-Imam al-Kadhim (as) kuwa Imam na badala yake wakamtambua mtoto mwingine wa Imam Swadiq, yaani Ismail kuwa ndiye Imam. Baada ya Hassan al-Sabbah kujiunga na kundi hilo alielekea nchini Misri kwa lengo la kujifunza mafundisho zaidi ya Ismailiyah. Wakati huo viongozi wa Ismailiyah walikuwa ni makhalifa wa utawala wa Fatwimiyah nchini Misri. Mwaka 473 Hassan al-Sabbah alirejea Iran na kuanza kueneza mafundisho ya kundi hilo katika maeneo tofauti ya Iran. Mwaka 483 alidhibiti ngome imara ya Alamūt karibu na mji wa Qazvin na ukawa mwanzo wa harakati ya mapambano dhidi ya utawala wa Seljuk uliokuwa unatawala Iran. Utawala wa Ismailiya chini ya uongozi wa Hassan al-Sabbah ulidhibiti pia ngome tofauti za kaskazini mashariki, kusini na hata katikati ya Iran sambamba na kuua viongozi wengi wa utawala wa Seljuk. Sabbah alifahamika kwa ubora huku akitabahari katika elimu za theolojia, falsafa na elimu ya nyota. Aliwaaachia wafuasi wake vitabu kadhaa.

Hassan al-Sabbah

Miaka 239 iliyopita inayosadifiana na tarehe 21 Novemba mwaka 1783, kwa mara ya kwanza katika historia ya jitihada za mwanadamu za kupaa angani, puto lilitumwa angani. Puto hilo lilikuwa limepandwa na watu wawili mmoja akiwa mwanafizikia wa Ufaransa aliyejulikana kwa jina la Pilatre De Rozier. Tangu alipokuwa masomoni De Rozier alikuwa akifikiria kutengeneza wenzo wa kupaa angani na kwa kutengeneza puto hilo mwanafizikia huyo akawa amefanikiwa kuruka angani.

De Rozier

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, Butros Butros Ghali alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa sita wa Umoja wa Mataifa. Butros Ghali alizaliwa mwaka 1922 katika familia ya Kikristo katika mji mkuu wa Misri Cairo. Baada ya kumaliza masomo yake Butros Butros Ghali alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Siasa cha Cairo. Mwanadiplomasia huyo ndiye aliyemshawishi na kumshajiisha Anwar Sadat, Rais wa zamani wa Misri, kutia saini mkataba wa Camp David mwaka 1978 na katika kuutambua rasmi utawala ghasibu wa Israel.

Butros Butros Ghali

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita inayosadifiana na 21 Novemba 1995, makubaliano ya amani ya Bosnia yaliyojulikana kwa jina la "Makubaliano ya Amani ya Dayton", yalitiwa saini. Makubaliano hayo ambayo yalifanyika kwa mashinikizo ya viongozi wa Marekani tarehe 21 Novemba 1995, yalitiwa saini na Marais wa wakati huo wa Bosnia Herzegovina, Serbia na Croatia. Mafanikio pekee ya makubaliano hayo kwa upande wa Waislamu, yalikuwa kuhitimishwa mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa na Waserbia. Zaidi ya Waislamu laki moja waliuawa kwa umati katika vita vya Bosnia.

Mauaji ya kimbari Bosnia

Na siku hii ya leo tarehe 21 Novemba imetangazwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Televisheni. Lengo la Umoja wa Mataifa la kuianisha siku hii lilikuwa kuweko mabadilishano ya vipindi vya runinga hususan vipindi vinavyotayarishwa kwa lengo la kueneza amani, ustawi wa kijamii na kiuchumi na kuimarisha masuala ya kiutamaduni katika jamii.