Nov 29, 2022 23:10 UTC
  • Jumatano, Novemba 30, 2022

Leo ni Jumatano tarehe 5 Mfunguo Nane Jumadil-ula 1444 Hijria sawa na tarehe 30 Novemba 2022 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1439 iliyopita alizaliwa Bibi Zainab (s.a) binti mtukufu wa Imam Ali bin Abi Twalib na Bibi Fatimatu Zahra (as). Bibi Zainab alikuwa mashuhuri miongoni mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo. Katika tukio la Karbala, Bibi Zainab (s.a) alisimama kidete na kukabiliana na dhulma za watawala dhalimu na ujahili watu wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (a.s). Bibi Zainab alipelekwa Sham pamoja na mateka wengine wa Nyumba Tukufu ya Mtume (saw) baada ya mapambano ya Imam Hussein (a.s) huko Karbala. Hotuba za Bibi Zainab mbele ya majlisi ya Ibn Ziyad mtawala wa Kufa na katika ikulu ya Yazid bin Muawiya huko Sham zilikuwa na taathira kubwa katika kufichua dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayya na kuonesha jinsi Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume walivyodhulumiwa.

Siku kama ya leo, miaka 1436 iliyopita kulijiri vita vya Mu'utah, baina ya jeshi la Waislamu na jeshi la Roma na waitifaki wake. Vita hivyo vilitokea baada ya mjumbe aliyekuwa ametumwa na Mtume (saw) huko Sham kwa ajili ya kulingania dini ya Kiislamu, kuuawa shahidi na askari wa kulinda mpaka wa eneo hilo. Baadhi ya wanahistoria wanasema kuwa, miongoni mwa sababu zilizomfanya Mtume (saw) kutuma jeshi la wapiganaji 3,000 kukabiliana na utawala wa Roma katika eneo hilo ni kuuawa shahidi walimu 14 wa Qur'ani Tukufu waliokuwa wametumwa na Mtukufu Mtume katika maeneo ya mpakani ya Sham. Katika vita hivyo Mtume alimteua Jaafar bin Abi Twalib, mtoto wa ami yake, kwa ajili ya kuongoza jeshi la Kiislamu, na akawateua Zaid bin Haritha na Abdullah bin Rawaaha kwa ajili ya kukaimu nafasi hiyo. Jeshi la Kiislamu ambalo lilikuwa limechoka kutokana na kwamba ilikuwa mara ya kwanza kwenda safari ndefu kama hiyo, lilipambana na jeshi la Roma na wapiganaji wa kikabila katika eneo la Mu'utah, magharibi mwa Jordan ya leo ambapo liliwapoteza viongozi wote watatu wa jeshi hilo la Kiislamu. Hatimaye Waislamu walimpa jukumu la kuongoza jeshi hilo Khalid Bin Walid ambaye ndiye kwanza alikuwa amesilimu, ambapo naye alitoa amri ya kuwataka Waislamu kurudi nyuma. Hata kama jeshi la Kiislamu halikushinda vita hivyo, lakini liliweza kusoma mbinu za jeshi la adui hatua ambayo ilikuwa utangulizi wa ushindi dhidi ya jeshi hilo la adui katika vita vya baadaye.

Siku kama ya leo miaka 462 iliyopita, alifariki dunia, Muhammad Mustafa Imadi, maarufu kwa jina la 'Abus-Suud', faqihi na mfasiri wa Qur'an Tukufu. Abus-Suud alizaliwa karibu na mji wa Istanbul, magharibi mwa Uturuki na kuanza kujifunza masomo ya dini ya Kiislamu ambapo alipanda daraja na kuanza kufundisha. Mbali na msomi huyo wa Kiislamu kufahamu lugha ya Kituruki, alikuwa hodari pia katika lugha ya Kifarsi na Kiarabu ambapo aliweza hata kusoma mashairi kwa lugha hizo. Miongoni mwa athari za Abus-Suud ni pamoja na 'Tafsir Abis-Suud' 'Dua Nameh' 'Qanun Nameh' na 'Mafruudhaat.'

Miaka 355 iliyopita katika siku kama ya leo, Jonathan Swift mwandishi mashuhuri wa Ireland alizaliwa huko Dublin mji mkuu wa nchi hiyo. Swift alishiriki pakubwa katika harakati za ukombozi wa Ireland. Baadaye, Jonathan Swift alianza kujishughulisha na kazi ya uandishi. Swift alifariki dunia akiwa na miaka 78. 

Jonathan Swift

Siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, alizaliwa Theodor Mommsen mwanahistoria na mtafiti wa Ujerumani. Baada ya kumaliza masomo, Mommsen alijishughulisha na utafiti kuhusiana na vitabu tofauti na athari za tamaduni za zamani. Miongoni mwa vitabu vyake maarufu zaidi ni kitababu kinachoitwa 'Historia ya Roma ya Kale' ambacho ndiyo kitabu kamili cha historia ya mji wa Roma. Mwanahistoria huyo wa Ujerumani alitunukiwa tuzo ya Nobel katika fasihi hapo mwaka 1902 na alifariki dunia mwaka mmoja baadaye, akiwa na umri wa miaka 86.

Theodor Mommsen

Miaka 187 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Mark Twain mwandishi mashuhuri wa Kimarekani. Twain alikipitisha kipindi cha utoto na ubarobaro wake na matukio yasiyo ya kawaida ambayo baadaye yalikuja kuwa maudhui kuu ya vitabu vyake. Mark Twain alikuwa mwandishi mwenye utani na mzaha. Aliandika visa na simulizi nyingi kwa ajili ya watoto na vijana wadogo ambapo tunaweza kuashiria hapa vitabu vyake viwili vya The Andventures of Tom Sawyer na (Matukio Yasiyo ya Kawaida ya Tom Sawyer) The Prince and The Pauper (Mrithi wa Kiti cha Ufalme na Ombaomba). Mwishoni mwa umri wake Mark Twain alikumbwa na ukata na umasikini mkubwa na hatimaye akaaga dunia mwaka 1910 baada ya kuugua.

Mark Twain

Miaka 122 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Oscar Wilde, mwandishi na malenga mahiri wa Ireland. Wilde alizaliwa mwaka 1854 katika familia iliyokuwa na mapenzi maalumu na masuala ya kiutamaduni na Sanaa. Baada ya kukamilisha masomo yake ya sekondari alijiunga na Chuo Kikuu. Oscar Wilde alianza kujihusisha na taaluma ya uandishi akiwa katika rika la ujana na katika kipindi kifupi cha umri wake alifanikiwa kuandika vitabu mbalimbali vilivyokuwa na madhumuni ya riwaya, mashairi na maigizo. Baadhi ya vitabu vya Oscar Wilde ni The Model Millionaire, The Soul of Man Under Socialism na The Canterville Ghost. 

Mark Twain

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, aliaga dunia Ustadh Abdul-Basit Abdul-Samad katika mji wa Cairo nchini Misri. Abdul Basit alikuwa mmoja wa waalimu na maqarii wakubwa wa Qur'ani Tukufu. Alianza kujifunza Qurani Tukufu akiwa mdogo na alipofikia umri wa miaka 12 akafanikiwa kupata tuzo ya kuhifadhi na kusoma Qur'ani. Katika maisha yake Ustadh Abdul-Basit alijishughulisha na usomaji wa Qurani Tukufu na kutunukiwa zawadi na tunzo muhimu katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani tukufu kwenye nchi mbalimbali za Kiislamu, sambamba na kuwavutia Waislamu wengi kwenye kusoma maneno hayo ya Mwenyezi Mungu. Abdul Basit ameacha kanda nyingi za sauti yake nzuri ya qiraa ya Qur'ani Tukufu.

Siku ya leo inayosadifiana na tarehe 9 Azar kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsiya huadhimiwa hapa nchini Iran kama siku ya kumbukumbu ya Sheikh Mufid, alimu, msomi na mwanafikra mkubwa wa Kishia. Alimu huyu ambaye ni mashuhuri zaidi kwa jina la Sheikh Mufid, jina lake kamili ni Muhammad bin Nu'man na alizaliwa huko Baghdad mwaka 336 Hijria. Alionyesha kipaji kikubwa cha masomo na ufahamu tangu akiwa katika rika la utoto na ni katika kipindi hicho pia alipoanza kusoma masomo ya Kiislamu. Sheikh Mufid ameandika vitabu vingi ambavyo vinakadiriwa kufikia 200. Al'Alam, Amali na Irshad ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya Sheikh Mufid. Alimu huyu amezikwa huko Kadhimain nchini Iraq.