Jumamosi, 03 Disemba, 2022
Leo ni Jumamosi tarehe 8 Mfunguo Nane Jamadul Awwal 1444 Hijria sawa na tarehe 3 Disemba 2022 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 138 iliyopita, alizaliwa Dakta Rajendra Prasad, mwanasiasa na mwanafilosofia wa India huko katika mojawapo ya vijiji vya jimbo la Bihar. Rajendra Prasad aliweza kuendelea na masomo na kufikia daraja ya udaktari, licha ya hali duni ya kifedha ya familia yake. Aidha alishiriki na wananchi wa India katika mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yao. Prasad vilevile alishirikiana bega kwa bega na Mahatma Gandhi katika mapambano ya kisiasa dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na kwa mara kadhaa aliteuliwa kuongoza chama cha Congress ya Kitaifa ya India. Rajendra Prasad aliteuliwa kuwa Rais wa kwanza wa India baada ya uhuru na kuasisiwa mfumo wa jamhuri nchini humo mwaka 1950. ***
Miaka 121 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sheikh Muhammad Abduh ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika mji wa Alexandria nchini Misri. Alipata elimu katika Chuo Kikuu cha al Azhar na kisha akahudhuria darsa za Jamaluddin Asadabadi, mwanazuoni aliyepigania uhuru wa nchi za Kiislamu. Baada ya kupelekwa uhamishoni Sayyid Jamaluddin, Sheikh Muhammad Abduh alichukua nafasi yake ya kufundisha na kutoa elimu kwa wanazuoni na wanafikra za Kiislamu. Hata hivyo Sheikh Abduh alibaidishiwa nchini Syria baada ya satuwa ya wakoloni wa Kiingereza kuenea nchini Misri. Baada ya kufunza kwa kipindi cha miaka sita nchini Syria alihamia Paris na kusaidiana na Sayyid Jamaluddin Asadabadi katika kuchapisha gazeti la al Uruwatul Wuthqaa. ***
Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipasishwa kwa wingi wa kura za wananchi. Katiba hiyo inasisitiza juu ya kuzingatiwa thamani za Kiislamu, uadilifu wa kijamii na kuheshimiwa haki za binadamu. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, katika mwaka 1368 Hijria Shamsia, kipengee cha ziada kiliongezwa kwenye katiba hiyo, baada ya kupasishwa na Baraza la Wataalamu linalomteuwa Kiongozi Mkuu wa Iran na kuidhinishwa pia na wananchi. Kwa mujibu wa kipengee hicho cha nyongeza, katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa ina vipengee 14 na vifungu 177. ***
Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 3 mwezi Disemba mwaka 1984, kulitokea janga kubwa la kuvuja gesi ya kemikali katika kiwanda kimoja cha Marekani katika mji wa Bhopal huko katikati mwa India. Kiwanda hicho kilikuwa kikimilikiwa na kampuni ya Kimarekani iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Union Carbide. Uzembe wa maafisa wa kiwanda hicho na kutozingatiwa viwango vya usalama kulipelekea kuvuja kwa gesi ya sumu ya sianidi (cyanide) kutoka katika kiwanda hicho na kuenea katika hewa. Wakazi wasio na hatia wa mji wa Bhopal wasiopungua 2500 walipoteza maisha yao na mamia ya wengine pia kujeruhiwa katika janga hilo. ***
Miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo, kombora la kwanza la balestiki lililotengenezwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilifanyiwa majaribio kwa mafanikio wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi hicho ambapo Iran ilikuwa chini ya vikwazo vikali vya nchi za Magharibi huku ikipigana na adui kulinda ardhi yake, awamu ya kwanza ya majaribio ya kombora hilo ilifanyika kwa mafanikio na uzalishaji wake ukaanza wakati wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.***