Jumapili Nne Disemba 2022
Leo ni Jumapili tarehe tisa Jamail Awwal 1444 Hijria Qamaria sawa Nne Disemba 2022 inayosadifiana na 13 Azar 1401 Hijria Shamsiya
Miaka 658 iliyopita, tarehe 9 Jamadil Awwal mwaka 786 Hijria, aliuawa shahidi faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi Muhammad bin Jamaluddin Makki Amili, mashuhuri kwa jina la "Shahidi wa Kwanza." Alizaliwa mwaka 734 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Jabal Amil nchini Lebanon. Alijifunza elimu mbalimbali kutoka kwa walimu wakubwa wa zama zake kama vile Allama Hilli. Mbali na elimu ya dini, Muhammad bin Jamaluddin pia alikuwa hodari katika taaluma za mashairi na fasihi. Katika miaka 52 ya umri wake uliojaa baraka, Shahidi wa Kwanza aliandika vitabu vingi, ikiwa ni pamoja na "Albaqiyatus-Swalihat" na "al Lumuatu Dimashqiyya." Aliuawa na wapinzani wenye taasubi katika siku kama ya leo.

Katika siku kama ya leo miaka 464 iliyopita alizaliwa katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran Ṣadruddin Muḥammad bin Ibrahim al-Shirazi maarufu kwa jina la Ṣadrul Muta'allihīn au Mulla Sadra, mwanafalsafa na arif mkubwa wa Kiislamu. Awali alielekea katika mji wa Qazwin uliokuwa katika zama hizo mji mkuu wa utawala wa Safavi na kuhudhuria darsa na masomo ya walimu wakubwa kama Sheikh Bahai. Alisoma Fikihi, Usul, hadithi na hisabati kwa Sheikh Bahai na kusoma mantiki, falsafa na Irfan kwa Mirdamad. Baada ya Isfahan kufanywa mji mkuu, Mulla Sadra naye alihamia katika mji huo na kuanza kufundisha. Hata hivyo kutokana na mitazamo yake kupingana na maulama kadhaa, Mulla Sadra alilazimika kuuhama mji huo na kuanza kuishi katika kijiji cha karibu na mji wa Qum. Baada ya muda alianza tena kujishughulisha na kazi ya kufundisha na kualifu vitabu. al Mabdau Wal-Maad, Zadul Musafir na Mutashaabihaat al-Qur'an ni baadhi tu ya vitabu vya Ṣadrul-Muta'allihīn.
Miaka 122 iliyopita, kwa mara ya kwanza chanjo ya homa ya matumbo au Typhoid ilitumiwa kwa mwanadamu ili kukabiliana na maradhi hayo ambayo husababisha kuhara damu. Awali chanjo hiyo ilivumbuliwa na mtafiti mmoja wa Kifaransa na baadaye ilikamilishwa na tabibu wa Kiingereza kwa jina la Almroth Edward Wright.

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, mkutano wa pande tatu yaani Marekani, Uingereza na Ufaransa ulifanyika katika kisiwa cha Bermuda kaskazini mwa Amerika Kusini. Mbali na nchi hizo tatu kujadili uhusiano baina yao, zilichukua maamuzi muhimu na kuratibu namna ya kukabiliana na siasa za Shirikisho la Umoja wa Sovieti huko Berlin. Katika zama hizo sehemu ya magharibi ya mji wa Berlin, Ujerumani ilikuwa chini ya udhibiti wa Marekani, Uingereza na Ufaransa na sehemu ya mashariki ilikuwa chini ya udhibiti wa Umoja wa Sovieti. Kupamba moto hitilafu za namna ya kuuendesha mji huo, ndiko kulikopelekea kujengwa ukuta maarufu wa Berlin mnamo mwaka 1961.

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, mkutano wa kwanza wa Kiislamu kuhusiana na Palestina ulifanyika hapa mjini Tehran. Mkutano huo ulifanyika katika fremu ya mfungamano wa walimwengu na mapambano ya Intifadha ya Palestina na kukabiliana na wimbi la kuhajiri Mayahudi kuelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Ajenda kuu ya mkutano huo ilikuwa kuchunguza chanzo cha mapambano ya Intifadha ya wananchi Waislamu wa Palestina, Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi hao pamoja na taathira ya matukio ya Mashariki ya Kati kwa taifa la Palestina.
Miaka 11 iliyopita katika siku hii, tarehe 13 Azar 1390 Hijiria Shamsiya: Mamlaka ya kijeshi ya Iran ilitangaza kuidhibiti ndege ya kijasusi ya Marekani isiyo na rubani au drone aina ya RQ-170 mashariki mwa Iran. Ndege hii iliyokuwa imepaa kutoka kambi yake nchini Afghanistan, iliangukia kwenye mtego wa vitengo vya vita vya kielektroniki vya Iran katika kina cha kilomita 200 ndani ya Iran na iliangushwa ikiwa na uharibifu mdogo. Ndege hiyo ya RQ-170 ni mojawapo ya ndege za kisasa zaidi zisizo na rubani za Jeshi la Marekani.
Kwa hivyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuchukua udhibiti wa ndege ambayo ina uwezo wa kukwepa rada ilionyesha uwezo wake katika uwanja wa vita vya kielektroniki na kusababisha mshangao mkubwa miongoni mwa wataalam wa kijeshi na mkanganyiko katika safu za watawala wa Marekani. Baada ya miaka mitatu, wataalamu wa Iran waliweza kunakili teknolojia ya ujenzi wake na miaka mitatu baadaye walijenga mfano wake kamili.