Dec 06, 2022 22:55 UTC
  • Jumatano, Disemba 7, 2022

Leo ni Jumatano tarehe 12 Mfunguo Nane Jumadil Awwal 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Disemba 2022 Milaadia.

Katika siku kama ya leo miaka 491 iliyopita alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu Ibn Tulun Dimashqi, aliyekuwa faqihi, mwanafasihi na mwanahistoria huko mjini Damascus, Syria. Ibn Tulun alizaliwa mwaka 880 Hijiria mjini Damascus na katika umri wake wote alifanya jitihada kubwa za utafiti, kufundisha na kuandika vitabu vya taaluma mbalimbali. Ibn Tulun Dimashqi ameandika vitabu vingi vya thamani kuhusiana na historia ya Kiislamu na pia katika uwanja wa tafsiri ya Qur'ani Tukufu, hadithi, lugha, tiba na irfani. Aidha kitabu cha 'as-Safiinatu al-Tuluuniyyah' ni miongoni mwa athari za mwanazuoni huyo.

Tarehe 7 Disemba miaka 133 iliyopita gari la kwanza la kisasa duniani lilitengenezwa. Gari hilo lililokuwa na uwezo wa kutembea kilomita 12 kwa saa lilitengenezwa na msomi wa Kijerumani aliyejulikana kwa jina la Karl Friedrich Benz. Gari hilo lilitumia nishati ya petroli au alkoholi. Karl Benz alifariki dunia mwaka 1929.

Friedrich Benz

Miaka 81 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, wakati Vita vya Pili vya Dunia vilipokuwa vimeshadidi barani Ulaya, ndege mia mbili za kivita za Japan zilishambulia kituo cha jeshi la Marekani katika bandari ya Pearl (Pearl Harbor). Shambulizi hilo lilifanyika wakati Japan ilipokuwa katika mazungumzo na Marekani kuhusu masuala ya mashariki mwa Asia. Sambamba na mashambulizi hayo ambayo yaliharibu meli 19 za kivita za Marekani, jeshi la Japan pia lilifanya mashambulizi makubwa katika nchi za kusini mwa Asia. Baada ya mashambulizi hayo Marekani ilitangaza vita dhidi ya Japan na Vita vya Pili vya Dunia vikapanuka zaidi hadi mashariki mwa Asia.

Shambulizi la Pearl Harbor

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, inayosadifiana na 16 Azar 1332 Hijria Shamsia, upinzani wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tehran dhidi ya safari ya Richard Nixon, Makamu wa Rais wa Marekani katika kipindi hicho hapa nchini, ulipelekea wanachuo watatu kuuawa na askari vibaraka wa utawala dhalimu wa Shah. Safari hiyo ilifanyika miezi mitatu na nusu tu baada ya mapinduzi ya Marekani dhidi ya serikali ya Dakta Muswaddeq. Siku ya pili baada ya mauaji hayo, Richard Nixon alitunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu wa sheria katika Chuo Kikuu cha Tehran. Kwa mnasaba huo, tarehe 16 Azar kila mwaka huadhimishwa nchini Iran kama "Siku ya Mwanachuo" hapa nchini. 

Na katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Abdul Wahhab Kayyali mmoja wa wanamapambano wa Palestina aliuawa na magaidi wa Kizayuni mjini Beirut. Aliingia katika masuala ya kisiasa akiwa mwanafunzi na risala yake ya shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha London pia ilihusu masuala ya Palestina na mapambano ya Waarabu dhidi ya ukoloni na Uzayuni.

Abdul Wahhab Kayyali