Dec 07, 2022 22:50 UTC
  • Alkhamisi tarehe 8 Disemba 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe 13 Jumadil Awwal 1444 Hijria sawa na Disemba 8 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1433 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria na kwa mujibu wa baadhi ya riwaya, Bibi Fatimatu Zahra binti wa Mtume Muhammad (saw) alikufa shahidi baada ya kuishi maisha mafupi lakini yaliyojaa mafunzo makubwa ya kimaadili na kimaanawi. Baba yake ni Mtume Muhammad (saw) na mama yake ni Bibi Khadija Binti Khuwaylid (as). Bibi Fatima alishiriki katika medani mbalimbali za mapambano mwanzoni mwa kudhihiri Uislamu akiwa bega kwa bega na baba yake, Mtume Muhammad (saw), Imam Ali bin Abi Talib pamoja na watoto wake wema, yaani Imam Hassan na Hussein (as) ambao Mtume amewataja kuwa ni vinara wa mabarobaro wa peponi. Bibi Fatima alisifika kwa tabia njema, uchamungu, elimu na maarifa, na alikuwa mfano na kigezo chema cha mwanamke na Waislamu kwa ujumla. 

Katika siku kama ya leo miaka 1372 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Ibrahim bin Malik al Ashtar mmoja wa makamanda na mashujaa wa Uislamu aliuawa katika vita na jeshi la Bani Umayyah. Alikuwa mtoto wa Malik al Ashtar, Swahaba na kamanda wa jeshi la Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as). Ibrahim alikuwa pamoja na baba yake katika kipindi cha ujana katika vita vya Siffin na alionesha ushujaa mkubwa dhidi ya jeshi la Muawiyyah.  Ibrahim Malik Ashtari aling'ara zaidi katika harakati iliyoanzishwa na Mukhtar Thaqafi huko Kufah dhidi ya utawala dhalimu wa bani Umayyah. Harakati hiyo ilianzishwa kwa lengo la kulipiza kizazi cha damu ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) pamoja na masahaba zake waliouawa katika tukio la Karbala mwaka 61 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 154 iliyopita, ulianguka utawala wa Washugani au kwa jina jingine watawala wa kijeshi huko Japan. Kuanguka kwa utawala huo kulipelekea kuanza kwa marekebisho ya kijamii, kisiasa na kiutamaduni nchini humo. Washugani walikuwa moja kati ya makumi ya silsila zenye nguvu huko Japan, walioanzisha utawala wao wa kidikteta tangu karne ya 12 Miladia.

Motso Hito

Katika siku kama ya leo miaka 119 aliaga dunia Herbert Spencer mwanafikra na mwanafalsafa wa Kiingereza. Spencer alizaliwa mwaka 1820 na kujifunza elimu mbalimbali kutoka kwa baba yake. Alijiongezea ujuzi na elimu kutokana na juhudi zake za kupenda kutalii mambo mbalimbali. Herbert Spencer aliamini kuwa, mtu anaweza kujipatia elimu kwa kushuhudia na kupata uzoefu. 

Herbert Spencer

Miaka 108 iliyopita katika siku kama ya leo, vilijiri vita vya baharini vya Falklands pambizoni mwa visiwa vya Falklands katika Bahari ya Atlantic kati ya Uingereza na Ujerumani. Vikosi vya wanamaji vya Ujerumani vilipigwa vibaya na vile vya Uingereza na visiwa hivyo vikatwaliwa tena na Waingereza. Visiwa vya Falklands ambavyo Argentina inasema ni milki yake, bado vinakaliwa kwa mabavu na Waingereza.

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, Chian Kai-shek kiongozi wa wapigania uhuru wa China alikimbilia Taiwan akiwa na wafuasi wake wengi baada ya kushindwa na wapiganaji wa chama cha Kikomonisti chini ya uongozi wa Mao Tse Tung na akaunda serikali ya kitaifa ya Uchina. Uungaji mkono wa Marekani kwa kiongozi huyo wakati huo ulipelekea Taiwan kujitenga na Uchina na kiti cha nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama kikatolewa kwa Taiwan. Hata hivyo mwaka 1971, kufuatia mazungumzo kati ya China na Marekani, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitambua Jamhuri ya Watu wa China kwa kura nyingi, na nchi hiyo ilikubaliwa katika Baraza la Usalama, na hivyo Taiwan ikapokonywa uanachama katika Umoja wa Mataifa.

Chian Kai-shek

Na katika siku kama ya leo miaka 23 iliyopita sawa na tarehe 17 Azar 1378 Hijria Shamsia aliaga dunia Husseini Makki mwanasiasa, mwanahistoria na mwandishi wa zama hizi wa Iran. Hussein Makki alizaliwa mwaka 1290 Hijria Shamsia. Baada ya kukamilisha masomo ya utangulizi alielekea katika mji wa Tehran na kuanza kufanya kazi serikalini. Baada ya mwaka 1320 Hijria Shamsia kupatina anga ya wazi ya kisiasa alianza rasmi harakati zake katika magazeti. Maandishi ya Husseini Makki ya kihistoria, kiutafiti na kifasihi yalikuwa sehemu muhimu ya makala katika magezeti mashuhuri ya Tehran zama hizo. Kujiunga kwake na Chama cha Iran na Chama cha Demokrasi cha Iran ndio uliokuwa mwanzo wa safari yake ya kuelekea katika harakati za kisiasa ambapo aliwahi kushika wadhifa wa Bunge katika duru tatu mtawalia.

Husseini Makki