Jumamosi, 10 Desemba, 2022
Leo ni Jumamosi tarehe 15 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1444 Hijria, mwafaka na tarehe 10 Disemba 2022 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1406 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, wema, ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali Swala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah Hisham bin Abdul Malik. Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya. ***

Tarehe 15 Mfunguo Nane Jamadil Awwal mwaka 38 Hijria, yaani miaka 1406 iliyopita aliuawa shahidi Muhammad bin Abu Bakr ambaye alikuwa miongoni mwa maswahaba waaminifu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kamanda maarufu wa jeshi la Uislamu katika vita dhidi ya jeshi la Muawiya lililokuwa likiongozwa na Amr bin al As. Mtawala wa kizazi cha Banii Umayyah, Muawiya alituma jeshi la wapiganaji elfu sita nchini Misri kwa ajili ya kupigana na jeshi la Muhammad bin Abu Bakr lililokuwa na wapiganaji elfu mbili. Jeshi la Muhammad bin Abu Bakr lilishindwa katika vita hivyo na kiongozi huyo akauawa shahidi kwa kuchomwa moto baada ya kukamatwa mateka. ***
Siku kama ya leo miaka 192 iliyopita, alizaliwa Bi Emily Dickinson malenga wa Kimarekani. Bi Emily alijiendeleza na masomo yake katika ngazi ya Chuo Kikuu nchini Marekani. Aidha alivutiwa na fasihi ya lugha na kutunga mashairi baada ya kufahamiana na baadhi ya waandishi mashuhuri wa Kimarekani. Malenga huyo wa Kimarekani aliweza kutunga beti karibu elfu mbili za mashairi, ambapo sehemu tatu tu za mashairi hayo zilichapishwa wakati wa uhai wake na zilizosalia zikachapishwa baada ya kuaga kwake dunia. ***
Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita toleo la kwanza la gazeti la al Uruwatul Wuthqaa lilichapishwa chini ya uongozi wa Sayyid Jamaluddin Asadabadi maarufu kwa jina la Jamaluddin Afghani na Sheikh Muhammad Abduh mjini Paris, Ufaransa. Sayyid Jamaluddin aliasisi Jumuiya ya al Uruwatul Wuthqaa kwa shabaha ya kutimiza lengo lake la kujenga umoja na mshikamano kati ya mataifa ya Kiislamu na akaanza kuchapisha gazeti kwa kutumia jina hilo hilo. Gazeti hilo lilisimamishwa mwezi Dhilhija mwaka huo huo baada ya kuchapishwa kwa kipindi cha miezi kadhaa tu katika nchi za Ulaya, India, Misri, Iran na katika nchi kadhaa za Kiarabu kutokana na mashinikizo ya kisiasa ya baadhi ya nchi. ***
Miaka 126 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mwanakemia maarufu wa Sweden, Alfred Bernhard Nobel. Nobel alizaliwa mwaka 1833 na kuhamia nchini Russia wakati wa ujana wake. Alfred Nobel alifanikiwa kuvumbua dynamite au baruti baada ya kufanya utafiti mkubwa kwa miaka kadhaa katika uwanja wa sayansi ya kemia. Hata hivyo mada hiyo badala ya kutumiwa kwa matumizi ya amani, ilianza kutumiwa kama kifaa cha kivita. Ni kwa sababu hiyo, ndipo Nobel akatoa pendekezo la kutolewa tuzo kila mwaka kwa shakhsia aliyefanya juhudi kubwa katika uwanja wa kuimarisha amani na usalama duniani. Tuzo hiyo ambayo imepewa jina la mwasisi wake yaani Nobel mwenyewe, hutolewa katika nyanja tano za fizikia, kemia, tiba, fasihi na amani ya kimataifa kwa wasomi waliofanya jitihada kubwa za kuleta amani na mafanikio ya kielimu, uvumbuzi, na mambo mengine makubwa duniani. Hata hivyo uteuzi wa washindi wa tuzo ya Nobel hususan ile ya amani duniani umeathiriwa na ushawishi wa baadhi ya madola makubwa na kuiondoa tuzo hiyo katika mkondo wa asili wa mwanzilishi wake. ***
Katika siku kama hii ya leo miaka 74 iliyopita, yaani tarehe 10 mwezi Disemba mwaka 1948, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu na kuidhinisha haki za kimsingi na kijamii za binadamu. Azimio hilo la haki za binadamu lilitayarishwa kwa maelekezo ya Umoja wa Mataifa kupitia jopo la wawakilishi wa nchi kadhaa duniani. Kipengee nambari moja cha azimio hilo kinasisitiza kuwa binadamu wote ni sawa. Licha ya kupasishwa azimio hilo, leo hii vitendo na siasa za madola ya Magharibi hasa Marekani vinakinzana wazi na azimio hilo. Leo hii pia baadhi ya madola hayo ya Magharibi yamekuwa yakilitumia suala la haki za binaadamu kama wenzo wa kuyashinikiza mataifa mengine. ***
Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni liliundwa nchini Iran kwa amri ya Imam Ruhullah Khomeini mwasisi na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu, makundi mbalimbali yalikuwa yakikwamishwa mwenendo wa masomo katika vyuo vikuu na shule mbalimbali hapa nchini. Kuna waalimu na wahadhiri wengi wapotofu ambao walikuwa wakifanya kazi katika vyuo vikuu na skuli tofauti hapa nchini na hakukuwa kumefanyika mabadiliko yoyote ya ratiba, mbinu za ufundishaji, malezi na masomo. Natija ya hilo ikawa ni kufungwa kwa muda vyuo vikuu. Baada ya vyuo vikuu kufungwa, Imam Khomeini alitoa amri ya kuundwa Baraza la Mapinduzi ya Kiutamaduni kwa shabaha ya kuboresha masuala ya utamaduni wa shule na vyuo vikuu. ***