Ijumaa, Disemba 23, 2022
Leo ni Ijumaa tarehe 28 Mfunguo Nane Jumadil Awwal 1444 Hijria inayosadifiana na 23 Disemba 2022 Milaadia.
Miaka 125 iliyopita na katika siku kama hii ya leo, Mirza Muhammad Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni wakubwa na mashuhuri wa Kiislamu, aliaga dunia.
Alizaliwa Shiraz huko kusini mwa Iran na baada ya kuhitimu masomo ya msingi alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kuendeleza masomo yake ya kidini na kupata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa mji huo kama Sheikh Murtadha Ansari. Bidii yake kwenye masomo ilimuwezesha kukwea haraka daraja za elimu na kuwa mhadhiri na mwanazuoni wa ngazi za juu mjini hapo na katika ulimwengu mzima wa Kiislamu.
Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa yake ya kuharamisha tumbaku katika kipindi cha utawala wa Nassiruddin Shah kutoka ukoo wa Qajaar. Fatuwa yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa ikihodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran.

Fatuwa hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Kwa hakika hatua hiyo iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni nchini.
Katika siku kama ya leo miaka 97 iliyopita mji wa Jeddah ulitekwa na Ibn Saud na kwa msingi huo utawala wa ukoo wa Hashemi ukahitimishwa katika mji huo. Baada ya kusambaratishwa uasi wa Mawahabi katika nusu ya kwanza ya karne ya 19 kundi hilo liliendelea kuwachochea watu dhidi ya serikali ya utawala wa Othmaniya. Mwanzoni mwa karne ya 20, Abdul Aziz ibn Abdulrahman ibn Saud, kinara wa moja kati ya makabila ya Hijaz aliamua kuteka moja ya maeneo ambayo yalikuwa yakitawaliwa na utawala wa Uthmaniyah ambayo alidai eti yalikuwa yameghusubiwa. Kwa msingi huo mwaka 1906, baada ya kuteka eneo la Riyadh, alijitangaza kuwa mtawala wa eneo hilo. Baada ya hapo watawala wa Uthmaniya walimpa eneo la Al Ahsa la mashariki mwa Hijaz na akapata tamaa ya kuendelea kuteka maeneo mengine. Mwaka 1924, Shariff Hussein, Amiri wa Makka ambaye alikuwa kutoka ukoo wa Hashimi, alijitangaza Khalifa na hapo Abdul Aziz ibn Saud kwa kisingizo kuwa Amiri aliyekuwa amejipachika cheo asichostahiki, alianza vita dhidi yake na katika uasi wake huo alifanikiwa kupata uungaji mkono wa makabila na mashekhe wa Kiwahabi. Hatimaye Disemba 23 mwaka 1925, ukoo wa Hashimi ulisalimu amri na 8 Januari 1926, Abdul Aziz ibn Saud alijitangaza kuwa mfalme wa eneo lote la Hijaz. Hatua hiyo ilikuwa utangulizi na kuundwa rasmi Ufalme wa Saudi Arabia mnamo September 18 mwaka 1932.

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita watu saba miongoni mwa viongozi mashuhuri wa Japan wakati wa Vita vya Pili vya Dunia walinyongwa, kufuatia hukumu iliyotolewa na mahakama moja ya kimataifa huko Tokyo mji mkuu wa nchi hiyo. Mahakama hiyo ambayo iliundwa ikiwa ni katika muendelezo wa mahakama ya Nuremberg ya Ujerumani kwa ajili ya kuwahukumu watenda jinai za kivita huko Japan, iliwahukumu viongozi 25 wa Japan ambapo 15 kati yao walihukumiwa kwenda jela.

Tarehe 23 Disemba miaka 69 iliyopita mkuu wa zamani wa shirika la kuogofya la usalama na la siri la Russia ya zamani ambaye pia alikuwa kiongozi nambari mbili wa nchi hiyo katika zama za Joseph Stalin, Lavrentiy Pavlovich Beria, alihukumiwa kifo na kunyongwa kwa tuhuma za kwenda kinyume na misingi ya sheria za Chama cha Kikomonisti sambamba na kufanya njama dhidi ya serikali. Katika kipindi cha utawala wa Stalin, Pavlovicha Beria alitoa amri ya kuuliwa watu wengi na akafanya umwagaji damu ndani ya Chama cha Kikomonisti na katika Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani.

Siku kama ya leo, tarehe 23 Disemba mwaka 2013, aliaga dunia Mrussia, Mikhail Kalashnikov ambaye ndiye aliyevumbua bunduki mashuhuri ya Kalashnikov ambayo inajulikana kama AK-47. Alizaliwa mwaka 1919 katika familia masikini kaskazini mwa Russia, na hakufanikiwa kupata masomo ya juu na hivyo alijiunga na Jeshi la Shirikisho la Sovieti akiwa na umri mdogo. Mwaka 1941, kufuatia shambulizi la Jeshi la Shirikisho la Sovieti dhidi ya wanajeshi wa Ujerumani ya Kinazi, Klashnikov alijeruhiwa na kulazwa hospitalini. Akiwa hospitalini alitumia muda wa kuuguza majeraha kufanya uchunguzi kuhusu sifa za kipekee za bunduki ya Kimarekani ya M1 Garand na bunduki ya StG 44 ya Ujerumani na kwa kutegemea sifa za silaha hizo mbili akaanza kuunda silaha mpya. Uundwaji silaha hiyo ulikamilika mwaka 1947 na kukabidhiwa rasmi Jeshi la Shirikisho la Sovieti mwaka 1951. Bunduki hiyo ilipewa jina la AK-47.

Mwishoni mwa Umri wake, Klashnikov alikuwa amelazwa hospitalini mjini Moscow kutokana na matatizo ya moyo na Septemba 2013 alihamishwa na kupelekwa katika hospitali moja huko Izhevsk, mji mkuu wa Jamhuri ya Udmurtia katika Shirikisho la Russia na hatimaye 23 Disemba 2013, akiwa na umri wa miaka 94 aliaga dunia akiwa anapata matibabu hospitalini.