Jumapili, 25 Disemba, 2022
Leo ni Jumapili tarehe Mosi Mfunguo Tisa Jamadu-Thani 1444 Hijriia sawa na tarehe 25 Disemba 2022 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 2022 iliyopita, Nabii Issa Masih (AS) alizaliwa katika mji wa Bait Laham (Bethlehem) huko Palestina. Nabii Issa Masih alipewa uwezo na Mwenyezi Mungu wa kufanya miujiza mingi. Issa Masih AS alianza kuzungumza akiwa mdogo na kujibashiria Unabii. Mwenyezi Mungu anaashiria tukio la kuzaliwa kwa Nabii Issa katika Qur'ani Tukufu katika Suratu Aal Imran aya ya 45 kwa kusema: Kumbukeni waliposema Malaika: "Ewe Mariam! Mwenyezi Mungu anakubashiria mwana kwa neno litokalo kwake; jina lake ni Masih, Issa mwana wa Maryam, mwenye hishima katika dunia na Akhera na miongoni mwa waliokurubishwa." Inafaa kuashiria hapa kwamba, tarehe 25 Disemba kila mwaka inajulikana kote duniani hasa kwa Wakristo kuwa ni Sikukuu ya Krismasi. ***
Katika siku kama ya leo miaka 379 iliyopita, alizaliwa Isaac Newton, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika na alitambuliwa kama mwanasayansi mkubwa aliyepata umashuhuri. Newton alibainisha pia sheria tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy. Ugunduzi wa Isaac Newton ulikuwa msingi mkuu wa ugunduzi wa wasomi wengine kuhusu kanuni kuu za hisabati na uhandisi. ***
Siku kama ya leo miaka 357 iliyopita mwafaka na tarehe 25 Disemba 1665, Ufaransa ilianzisha French East India Company katika kipindi cha utawala wa Mfalme Louis II ili kushindana kisiasa, kiuchumi na kiukoloni na serikali ya Uingereza huko India. Uingereza ilikuwa imeasisi British East India Company miaka 66 kabla ya hapo. Vilitokea vita kadhaa baina ya tawala hizo mbili za kikoloni kwa shabaha ya kuikoloni ardhi ya India. ***

Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Charles Spencer Chaplin mcheza filamu na msanii mashuhuri wa tasnia ya filamu. Alipokuwa mdogo, alianza na michezo ya kuigiza na kupata umashuhuri hatua kwa hatua. Mwanzoni mwa ujana wake, Chaplin alielekea nchini Marekani kwa lengo la kutengeneza filamu. Lakini kutokana na kutengeneza filamu ya ukosoaji na yenye kuonyesha mshikamano wake na matabaka ya kimasikini katika jamii ya Marekani, serikali ya nchi hiyo ilitoa amri ya kubaidishwa kwake mnamo mwaka 1952. Chaplin alikumbana na mazingira magumu ya kufanya shughuli zake nchini Marekani na hivyo akahamia nchini Uswisi pamoja na mkewe. ***
Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita inayosadifiana na tarehe 25 Disemba 1979, viongozi watatu wa ngazi za juu wa Palestina waliuawa kigaidi na Shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD. Viongozi hao walikuwa Ali Hassan Salameh, afisa wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) aliyeuawa Beirut baada ya kutegwa bomu ndani ya gari lake, Samir Touqan mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya PLO huko Cyprus na Ali Nasser Yassin, shakhsia mwingine wa Palestina aliyekuwa mwakilishi wa PLO nchini Kuwait. Jinai hiyo ilidhihirisha tena jinsi utawala katili wa Israel unavyotumia ugaidi katika maeneo mbalimbali dunia kwa ajili ya kufikia malengo yake haramu. ***