Jumapili, Mosi Januari, 2023
Leo ni Jumapili tarehe 8 Mfunguo Tisa Jamadu-Thani 1444 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe Mosi Januari 2023 Miladia.
Leo ni tarehe Mosi Januari inayosadifiana na kuanza mwaka mpya wa 2023 Miladia. Mpangilio wa miezi ya mwaka wa Kirumi unaoanza Januari hadi Disemba ulianza kutumiwa katika kipindi cha Mfalme Numa Pompilius yapata miaka 700 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih (as). Kwa msingi huo tarehe 31 Disemba huwa siku ya mwisho ya mwaka wa Miladia na usiku wa kuamkia tarehe Mosi Januari huanza sherehe za kupokea mwaka mpya katika jamii za Wakristo na nchi nyingi za Afrika, America, Ulaya, Australia na hata Asia. ***

Miaka 219 iliyopita sawa na tarehe Mosi Januari mwaka 1804 Miladia nchi ya Haiti ilijitangazia uhuru ikiwa nchi ya kwanza kufanya hivyo katika eneo la Amerika ya Latini. Uhuru wa Haiti ulipatikana kufuatia mapambano na harakati kubwa ya watumwa weusi wa nchi hiyo dhidi ya vitendo vya utumwa vya Ufaransa na kisha baadaye kuanzisha mapambano dhidi ya jeshi la Ufaransa. Ufaransa ilianza kuikoloni Haiti mwaka 1677. Baada ya kujipatia uhuru, Haiti ilikumbwa na machafuko ya ndani. ***
Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita Heinrich Rudolf Hertz mwanafizikia na mwanahisabati wa Ujerumani aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 37. Alizaliwa mjini Hamburg Ujerumani mwaka 1857. Alikuwa na mapenzi makubwa na fizikia na umakenika tangu akiwa kijana mdogo. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana akajiendeleza kimasomo katika uwanja huo. ***
Miaka 67 iliyopita katika siku kama ya leo nchi ya Sudan ilipata uhuru kutoka kwa Misri na Uingereza. Mwaka 1899 Uingereza na Misri zilitiliana saini mkataba wa kuitawala kwa pamoja Sudan. Katikati mwa karne ya 20 lilianza vuguvugu la kutaka kujipatia uhuru nchini Sudan na mwaka 1956 Misri na Uingereza zikalazimika kuutambua uhuru wa nchi hiyo. Sudan inapakana na nchi za Sudan Kusini, Misri, Libya, Chad, Kenya, Uganda, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. ***
Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin Aamili, alimu na msomi mkubwa wa Kiislamu. Ayatullah Sharafuddin alizaliwa mwaka 1290 Hijria huko Kadhimain moja kati ya miji ya Iraq. Alielekea Jabal Amil nchini Lebanon baada ya kuhitimu masomo yake na kuanza kujishughulisha na harakati za Kiislamu. Msomi huyo mkubwa ametoa huduma za thamani kubwa kwa ulimwengu wa Kiislamu na daima alikuwa akisisitiza suala la umoja baina ya Waislamu. Ayatullah Sayyid Abdul Hussein Sharafuddin ameandika vitabu na risala nyingi ili kufikiwa lengo hilo. ***
Tarehe Mosi Januari mwaka 1959 miaka 64 iliyopiita mapinduzi ya Cuba yalipata ushindi na dikteta Fulgencio Batista akaikimbia nchi hiyo. Ushindi wa mapinduzi hayo yaliyoongozwa na Fidel Castro uliiweka Marekani katika mazingira magumu baada ya kushindwa vibaraka wake nchini Cuba.***
Miaka 64 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Kiafrika ya Cameroon ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Kwa miaka mingi nchi hiyo ilikuwa chini ya ukoloni wa nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani ambayo iliikalia kwa mabavu Cameroon kuanzia mwaka 1884. Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia Ufaransa na Uingereza ziligawana baina yao ardhi ya Cameroon. Hata hivyo haukupita muda kabla ya kuanza mapambano ya kupigania uhuru nchini humo. Hatimaye mapambano ya kupigania uhuru nchini Cameroon yalizaa matunda katika siku kama ya leo baada ya nchi hiyo iliyoko magharibi mwa Afrika kujipatia uhuru.***
Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita nchi ya Brunei ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Nchi hiyo ndogo na yenye wakazi wachache kijiografia iko kusini mashariki mwa Asia. Tangu kale mfumo wa utawala nchini Brunei ulikuwa wa Kifalme ambao ulikuwa ukisimamiwa na Uingereza. Brunei inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi tajiri duniani kutokana na kuwa na akiba kubwa ya mafuta na gesi. ***
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Mosi Januari 1993, yalianza kutekelezwa makubaliano ya Maastricht, eneo lililoko kusini mwa Uholanzi yaliyokuwa na lengo la kuondoa mipaka ya kiuchumi kati ya nchi 12 za Ulaya. Mkataba wa muungano wa Ulaya ulitiwa saini tarehe 10 Disemba mwaka 1991 na viongozi wa nchi 12 wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya katika mji mashuhuri wa Maastricht. Baadaye Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya ilibadilishwa na kuwa Umoja wa Ulaya. Utekelezwaji wa makubaliano ya Maastricht ulikuwa hatua kubwa katika mchakato wa kuungana zaidi wanachama wa Umoja wa Ulaya japo kuwa umoja huo ulikabiliwa na matatizo mengi katika miaka iliyofuatia.***