Ijumaa tarehe 17 Februari 2023
Leo ni Ijumaa tarehe 26 Rajab 1444 Hijria sawa na Februari 17 mwaka 2023.
Siku kama ya leo miaka 1447 iliyopita, Abu Twalib ami ya Mtume Muhammad (SAW) na baba wa Imam Ali (A.S) alifariki dunia wakati Waislamu walipokuwa chini ya mzingiro wa washirikina wa Makka. Abu Twalib alikuwa pamoja na Waislamu wengine huko katika Shiibi Abi Twalib. Mtume Muhammad (SAW) alikuwa chini ya uangalizi wa Abu Twalib tangu alipokuwa na umri wa miaka minane, baada ya kuaga dunia babu yake, Abdul Muttalib. Abu Twalib alisilimu baada ya kubaathiwa Mtume na alikuwa muungaji mkono na mtetezi mkubwa wa Mtume Mtukufu dhidi ya washirikina wa Kiquraishi. Kabla ya kuaga dunia, Abu Twalib aliwausia jamaa na marafiki zake kufuata Uislamu na kumtetea Mtume Muhammad (saw).
Katika mwaka uhuo huo wa kifo cha Abu Twalib, aliaga dunia pia Bibi Khadija bint Khuwailid, mke mwaminifu na mwema wa Mtume wetu Muhammad (saw), na kutokana na ukubwa wa huzuni na masikitiko yaliyosababishwa na matukio haya mawili, Mtume aliutaja mwaka huo kuwa ni “Aamul Huzn", kwa maana ya mwaka wa huzuni. ***
Siku kama ya leo miaka 213 iliyopita, vilimalizika vita vya umwagaji damu vya Zaragoza vilivyopiganwa kati ya wanajeshi wa Ufaransa na wale wa Uhispania, huku Ufaransa ikipata ushindi na kuukalia kwa mabavu mji wa Zaragoza ulioko mashariki mwa Uhispania. Vita hivyo vilianza Novemba 15 mwaka 1808, kufuatia uvamizi wa jeshi la Napoleon.
Katika siku kama ya leo miaka 195 iliyopita, aliaga dunia Johann Heinrich Pestalozzi, msomi wa Uswisi na mmoja wa walimu mashuhuri. Pestalozzi alikuwa mjuzi wa elimu nyingi hasa hisabati na tiba na alizungumza lugha kadhaa za kimataifa. Msomi huyo wa Uswisi alikuwa na mtindo wake makhsusi wa kufundishia ambapo aliweza kutoa mafunzo ya masuala mbalimbali kwa watoto kwa wakati mmoja.
Miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo, mazungumzo ya amani ya pande tatu kati ya Iran na utawala wa Baath wa Iraq yalianza huko New York Marekani. Katika hali ambayo mazungumzo hayo hayakuwa na natija ya maana na hata kulikuwa na uwezekano wa kuvunjuika kwake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa imethibitisha nia yake njema kwa jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa hususan Katibu Mkuu wake.
Katika siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, mkataba wa kuasisiwa Jumuiya ya Magharibi ya Kiarabu za ulitiwa sana huko Morocco kwa kuhudhuriwa na Marais wa nchi za kaskazini mwa Afrika. Nchi washiriki wa mkataba huo zilikuwa Libya, Mauritania, Algeria, Tunisia na mwenyeji Morocco. Lengo la kuasisiwa jumuiya hiyo lilikuwa kuanzisha taasisi ya kieneo kwa lengo la kupanua ushirikiano baina ya nchi wanachama na kupunguza utegemezi kwa nchi za Magharibi. Hata hivyo, hitilafu za kimitazamo za baadhi ya wanachama wa Jumuiya ya Magharibi ya Kiarabu kama Algeria na Morocco kuhusiana na suala la Sahara Magharibi na vilevile mizozo ya mipaka na kisiasa zilizuia kufikiwa malengo ya kuasisiwa jumuiya hiyo.
Miaka 11 iliyopita katika siku kama ya leo utawala kandamizi wa Aal Khalifa nchini Bahrain uliyageuza maandamano ya amani ya wananchi katika medani ya Lulu kuwa dimbwi la damu. Bahrain ambayo nayo ilikuwa imetumbukia katika mkondo wa harakati ya mwamko wa Kiislamu katika nchi za Kiarabu, wananchi wa nchi hiyo wakiwa na lengo la kupigania haki zao za kimsingi na za kiraia walikuwa wameanza kufanya maandamano ya amani dhidi ya utawala wa Manama. Katika miaka 6 iliyopita licha ya kutiwa mbaroni wanaharakti wengi wapigania uhuru nchini Bahrain, wananchi hao hawajasalimu amri na kuachana na harakati yao na wamekuwa wakiandelea kudai matakwa yao yatekelezwe na utawala wa Aal Khalifa wa Bahrain.
Tarehe 17 Februari miaka 11 iliyopita ilianza harakati ya wananchi wa Libya dhidi ya utawala wa kidikteta wa Kanali Mummar Gadafi. Libya ilikuwa nchi ya tatu kukumbwa na wimbi la mwamko wa Kiislamu na kuziangusha tawala kadhaa za kidikteta. Baada ya kuondolewa madarakani serikali ya Zainul Abidin bin Ali nchini Tunisia na ile wa dikteta wa zamani wa Misri, Husni Mubarak, wananchi wa Libya pia walianzisha harakati kubwa dhidi ya dikteta wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi. Awali Gaddafi alidhani kwamba angeweza kuzima harakati hiyo ya wananchi kwa kutumia jeshi na vyombo vya usalama na kwa msingi huo alianza kutumia mkono wa chuma na kuua wananchi waliokuwa wakiandamana. Wanachama wa shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO pia walipanda mawimbi ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Libya na kushambulia vituo vya kijeshi na viwanda vya Libya. Hatimaye dikteta Muammar Gaddafi aliyeitawala Libya kwa kipindi cha miongoni minne kwa mkono wa chuma aliondolewa madarakani kwa madhila na kuuawa kwa kudhalilishwa na kisha akazikwa sehemu isiyojulikana.
Na katika siku kama ya leo miaka 6 iliyopita Mohamed Hassanein Heikal mwandishi na mwanafikra mtajika wa Misri alifariki dunia. Mohamed Heikal alizaliwa Septemba 23 1923 katika jimbo la Qalyubia huko Misri. Alikuwa mhariri mkuu katika gazeti la al-Ahram la Misri kwa muda wa miaka 17. Heikal alikuwa muasisi wa kituo mashuhuri cha utafiti wa kisiasa na kiistratejia cha al-Ahram.