Jumamosi tarehe 18 Februari 2023 Miladia
Leo ni Jumamosi tarehe 27 Rajab 1444 Hijria sawa na Februari 18 mwaka 2023 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1457 iliyopita, Mtume Muhammad (saw) alibaathiwa yaani kupewa Utume na Mwenyezi Mungu. Kipindi hicho Mtume Muhammad (saw) alikuwa na umri wa miaka 40. Mtume Muhammad (saw) alianza kutafakari na kudurusu maumbile ya dunia akiwa bado mdogo na daima alikuwa akifirikia njia za kunyanyua juu utukufu wa mwanadamu. Alikuwa maarufu kwa ukweli, uaminifu na kutenda mema. Jumla ya sifa hizo njema zilimfanya Muhammad (saw) kuwa shakhsia mwenye hadhi na heshima kubwa katika jamii. Alitumia muda wake mwingi katika ibada na kutafakari katika Pango la Hiraa. Malaika Jibrail alimteremkia Muhammad akiwa katika pango hilo na kumwambia kwamba ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mtume wake wa Mwisho kwa walimwengu wote. Tangu siku hiyo mtukufu huyo alipewa jukumu kubwa la kuongoza wanaadamu na kupambana na ujahili, ukafiri, dhulma na uonevu. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa siku hii adhimu. **
Siku kama ya leo miaka 977 iliyopita alizaliwa faqihi, mfasiri wa Qur'ani na msomi wa Kiislamu na Kiirani, Jarullah Zamakhshari. Mwanazuoni huyu pia alikuwa gwiji katika elimu za Hadithi na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Muqaddimatul Adab na Asasul Balagha. Kitabu muhimu zaidi cha Jarullah Zamakhshari ni tafsiri ya Qur'ani ya al "Kash'shaf". **
Miaka 459 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Michelangelo di Lodovico Buonarroti, mchongaji wa sanamu, msanifu majengo na malenga mkubwa wa Kiitalia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 89. Michelangelo alizaliwa mwaka 1475 na kuanza kujishughulisha na uchoraji na kuchonga sanamu licha ya upinzani wa baba yake. Malenga huyo wa Kiitalia alionyesha kipaji chake haraka katika uwanja wa uchoraji, uchongaji sanamu na usanifu majengo. Uchongaji wa sanamu za Manabii Isa na Musa huko Italia ni moja kati ya kazi kubwa za kisanaa zilizofanywa na Michelangelo katika zama zake hizo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 216 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa msomi na fakihi mtajika wa Kishia. Alizaliwa mjini Najaf huko Iraq na kuanza kujihusisha na masomo ya dini tangu katika kipindi cha utoto wake. Awali alisoma masomo ya utangulizi kwa baba yake na kisha baadaye akahudhuria masomo kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama sayyid Mahdi Bahr al-Uluum. Baadaye Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa alianza kufundisha na kuandika vitabu na kufanikiwa kuwalea wanafunzi wengi na vile vile kuandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali. ***
Siku kama ya leo miaka 189 iliyopita, vikosi vya utawala wa kikoloni wa Ufaransa ambavyo vilianza kuikalia kwa mabavu Algeria mwaka 1830, vilishindwa vibaya na wapiganaji wa Amir Abdelkader al-Djezairi, kiasi kwamba theluthi moja ya askari wa Ufaransa waliuawa na nusu nyingine ya waliobakia hai walikamatwa mateka. Wakati huo Wafaransa ambao ndio ilikuwa mara yao ya kwanza kupata hasara kubwa ya namna hiyo barani Afrika, waliamua kuomba suluhu ili kujipanga upya na kukusanya nguvu. Hata hivyo Amir Abdelkader al-Djezairi alikataa ombi hilo, hadi baada ya kupita karibu miaka miwili na kuikomboa ardhi yote ya Algeria kutoka mikononi mwa Wafaransa hao wavamizi. Miaka kadhaa baadaye Ufaransa iliweza kuidhibiti tena nchi hiyo baada ya kuongeza askari na zana za kijeshi sambamba na kuwatumia baadhi ya viongozi wasaliti wa makabila ndani ya Algeria. ***
Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, askari wa Ufaransa na Uhispania, walivunja mapambano ya wapiganaji wa Morocco chini ya uongozi wa Abdel-Karim Rifi, na shujaa huyo Muislamu akapelekwa uhamishoni kusini mwa Afrika. Abdel-Karim Rifi alianzisha mapambano yake sambamba na kuanza uvamizi wa Uhispania katika sehemu ya ardhi ya Morocco hapo mwaka 1912. Hata hivyo na licha ya mkoloni huyo kuwa na nguvu kubwa na kutekeleza mauaji ya umati dhidi ya raia wa Morocco wasio na hatia, mwaka 1921 wapiganaji wa Abdel-Karim Rifi walipata ushindi mkubwa kiasi cha kuyafanya baadhi ya maeneo ya nchi hiyo kutangaza Jamhuri. Wafaransa nao ambao walikuwa wakiyadhibiti baadhi ya maeneo ya nchi hiyo walipatwa na hofu kufuatia ushindi wa wananchi dhidi ya Wahispania na mwanzoni mwa mwaka 1924 walianzisha hujuma kubwa dhidi ya wanamapambano hao. Jeshi la Ufaransa chini ya Jemadari Philippe Pétain ambalo mwanzoni lilishindwa vibaya na wanamupambano wa Morocco, mwezi Februari 1926 katika siku kama ya leo liliwashinda wapiganaji wa Abdel-Karim Rifi baada ya kupata msaada wa kijeshi na kutekeleza jinai kubwa dhidi ya raia wa Morocco. Kwa utaratibu huo Ufaransa ikaweza kuendeleza ukoloni wake nchini Morocco. ***
Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita yaani mnamo tarehe 18 mwezi Februari mwaka 1965, Gambia ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Uingereza ilianza kuikoloni Gambia mwaka 1588 na kupora maliasi za nchi hiyo kwa karibu karne nne. Mwaka 1963, Uingereza iliipatia Gambia mamlaka ya ndani baada ya kudhoofika kisiasa na kiuchumi kutokana na Vita vya Pili vya Dunia na kushindwa kuendesha makoloni yake. Hatimaye ilipofika mwaka 1965 Gambia ilipatia uhuru wake. ***
Miaka 56 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mwanafizikia na mtengenezaji wa bomu la atomiki wa Marekani, Robert Oppenheimer. Kabla ya Vita vya Pili vya Dunia mtaalamu huyo alifanya utafiti kuhusiana na jinsi ya kupasua atomu na kupata nishati ya nyuklia. Wakati wa vita hivyo alipewa wadhifa wa kusimamia kitengo cha utafiti katika Wizara ya Vita ya Marekani na chini ya usimamizi wake yakatengenezwa mabomu matatu ya kwanza ya nyuklia. Hata hivyo, wakati Marekani ilipoishambulia Japan kwa mabomu ya nyuklia mwaka 1945, makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia waliuawa katika kipindi kifupi, hali iliyomfanya Oppenheimer kujutia kitendo chake hicho na akatoa wito wa kutumiwa nishati ya atomiki katika masuala ya amani. ***
Katika siku kama ya leo miaka 24 iliyopita Ayatullah Sayyid Muhammad Swadiq al-Sadr mmoja wa maulamaa mashuhuri wa Iraq aliuawa kigaidi katika mji mtakatifu wa Najaf nchini humo. Wananchi Waislamu wa Iraq walifanya maandamano kadhaa kufuatia kuuawa kwa msomi huyo mkubwa na kuutaja utawala wa zamani wa Baath huko Iraq kuwa ndio uliomuuwa shahidi Ayatullah Sadr. Utawala wa zamani wa Baahi nchini Iraq ulifanya mauaji mengi dhidi ya maulamaa na wanazuoni wa Kiislamu katika siasa zake za kuidhoofisha Hauza na chuo kikuu cha kidini katika mji mtakatifu wa Najaf tangu uliposhika hatamu za uongozi nchini humo mwaka 1968 hadi ulipoondolewa madarakani. **