Apr 13, 2023 02:38 UTC
  • Alkhamisi tarehe 13 Aprili 2023

Leo ni tarehe 22 mwezi Mtukufu wa Ramadhani 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 13 Aprili 2023.

Siku kama ya leo miaka 1171 iliyopita, alifariki dunia Ibn Majah, mpokezi wa hadithi na mfasiri mashuhuri wa Qur’ani wa Kiislamu. Ibn Majah alizaliwa mwaka 209 Hijria katika mji wa Qazvin nchini Iran. Alielekea katika nchi mbalimbali za Kiislamu ili kujifunza elimu ya hadithi. Aliandika kitabu chake mashuhuri kwa jina la "Sunan Ibn Majah" baada ya kuhitimu masomo katika elimu ya hadithi, kitabu ambacho ni moja kati ya vitabu sita vya hadithi vyenye itibari vya Waislamu wa madhehebu ya Suni.

Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita alifariki dunia, Haj Abdul-Hussein Tehrani, maarufu kwa jina la Sheikhul-Iraaqiyyin, mmoja wa maulama wakubwa wa Iran. Haj Abdul-Hussein Tehrani alitabahari katika elimu ya fiqhi, huku akiwa mcha-Mungu sana. Kadhalika alitambulika kwa kuwa na kumbukumbu ya hali ya juu katika msomo ya dini. Mbali na fiqhi, pia alikuwa alimu katika elimu ya hadithi na tafsiri ya Qur'an Tukufu. Alifanya juhudi kubwa katika kuasisi maktaba na kukusanya turathi za Kiislamu ambapo baada ya kufariki kwake dunia kuliasisiwa maktaba kubwa kwa ajili ya wanafunzi wa Kiislamu.

Haj Abdul-Hussein Tehrani

Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, kulijiri tukio la umwagaji damu mkubwa katika Bustani ya Jallianwala nchini India. Mwaka 1919 na kwa lengo la kuzuia uasi na mapambano ya wananchi, serikali ya kikoloni ya Uingereza ilipasisha sheria iliyowapa polisi haki ya kuwatia mbaroni wanaharakati wa India bila sababu yoyote na kuwashikilia kwa muda usiojulikana. Sheria hiyo iliwakasirisha mno wananchi wa India na katika siku kama ya leo zaidi ya Wahindi elfu tano waliokuwa wamekusanyika kwa amani katika Bustani ya Jallianwala katika mji wa Amritsar walimiminiwa risasi kwa amri ya kamanda mmoja wa Uingereza. Watu 1200 waliuawa na wengine 4000 kujeruhiwa katika tukio hilo. Baada ya mauaji hayo, harakati ya ukombozi wa India ikiongozwa na shujaa Mahatma Ghandhi ilipamba moto.

Mahatma Ghandhi

Tarehe 13 Aprili mwaka 1945 yaani miaka 78 iliyopita, Austria ilidhibitiwa na kukaliwa kwa mabavu na vikosi vya nchi Waitifaki. Tukio hilo lilijiri katika miezi ya mwisho ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Kabla ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, Austria ilikuwa nchi huru na inayojitawala. Lakini muda mchache baada ya kuanza vita hivyo, Adolph Hitler aliiunganisha ardhi ya nchi hiyo na Ujerumani na wanajeshi wa Austria wakaingia vitani kupigana upande wa Ujerumani. Baada ya Ujerumani kuondoka Austria na nchi hiyo kukaliwa kwa mabavu na madola Waitifaki, iligawanywa katika maeneo matano ambapo kila eneo likadhibitiwa na kuendeshwa na moja ya madola hayo, huku mji mkuu Vienna ukiendeshwa kwa pamoja na madola manne. Hatimaye mwaka 1946, madola Waitifaki yalitambua rasmi uhuru wa Austria ambapo baada ya kutiwa saini mkataba wa amani kati ya pande mbili, mwaka 1955, majeshi ya nchi waitifaki yakaondoka katika ardhi ya Austria.

Austria

Katika siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, shambulio la wanamgambo wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa kundi la Mafalanja lililolenga basi moja lililokuwa na Wapalestina na kuua watu 30 kati yao, lilipelekea kuibuka vita vya ndani nchini Lebanon. Kufuatia mauaji hayo, Waislamu na wazalendo wa Lebanon walianzisha mapambano ya kukabiliana na Mafalanja hao. Muda mfupi baadaye harakati za wapiganaji wa Kipalestina pia ziliingia katika vita hivyo vya ndani vya Lebanon. Vita hivyo ambayo vilikuwa vikichochewa na utawala haramu wa Israel, viliisababishia hasara kubwa ya mali na roho serikali ya Beirut.

Wanamgambo wa Kikristo wa Lebanon

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu, Ayatullah Mujtaba Hatami Lankarani. Ayatullah Lankarani alizaliwa katika mji wa Isfahan hapa nchini Iran na katika kipindi cha ujanani alielekea katika mji wa Najaf huko Iraq kwa ajili ya kupata masomo. Akiwa huko Najaf, Ayatullah Mujtaba Hatami Lankarani aliweza kusoma chini ya maulama wakubwa wa zama zake kama vile Dhiyaudin Iraqi, Ayatullah Mirzai Naayini na Sayyid Abul-Hassan Isfahani. Baada ya kumaliza masomo yake na kufikia daraja ya juu ya elimu alirudi katika mji alikozaliwa wa Isfahan na kutumia umri wake wote katika kutoa mafunzo ya dini tukufu ya Kiislamu. Ayatullah Lankarani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 75.

Ayatullah Mujtaba Hatami Lankarani

Katika siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, yaani tarehe 13 Aprili 2003, maandamano ya kwanza ya wananchi wa Iraq dhidi ya wavamizi baada ya miongo mitatu ya mbinyo na ukandamizaji ya utawala wa dikteta Saddam Hussein yalifanyika. Baada ya kuangushwa utawala wa Saddam na chama cha Baath Aprili 9 mwaka 2003 na kisha nchi hiyo kukaliwa kwa mabavu na vikosi vamizi hususan majeshi ya Marekani, maandamano ya kwanza ya wananchi ya kupinga kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu nchi yao yalifanyika.

Wanajeshi vamizi wa Marekani nchini Iraq

Na katika siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, wananchi kadhaa wa Iran waliuawa shahidi kufuatia shambulio la kigaidi na utegaji bomu. Bomu hilo lilitegwa katika Husseiniya ya Shuhadaa katika mji wa Shiraz. Jinai hiyo ilifanyika kwa uongozi na usimamizi wa mashirika ya kijasusi ya kigeni. Baadhi ya watekelezaji wa shambulio hilo la bomu walitiwa mbaroni katika moja ya hoteli za Tehran ambapo baada ya kufunguliwa mashtaka walilipwa ujira wa amali yao hiyo.