Apr 28, 2023 06:28 UTC
  • Leo ni Ijumaa, 28 Aprili mwaka 2023

Leo ni Iijumaa tarehe 7 Shawwal 1444 Hijria sawa na Aprili 28 mwaka 2023.

Siku kama hii ya leo miaka 1441 iliyopita kulipiganwa vita vya Uhud kando kando ya mlima wenye jina hilo kaskazini mwa mji wa Madina, kati ya Waislamu na Washirikina. Baada ya washirikina wa Kiquraishi kushindwa vibaya na Waislamu katika vita vya Badr walianzisha vita hivi vya Uhud kwa kuandaa jeshi la watu 3,000 waliokuwa na zana kamili kwa ajili ya vita hivyo, huku wapiganaji wa Kiislamu wakuwa 700 tu. Kabla ya kuanza kwa vita hivyo, Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w) aliwashauri masahaba zake juu ya namna atakavyopambana na Maquraishi na iliamuliwa kuwa vita hivyo vipiganwe nje ya mji wa Madina. mwanzoni mwa vita hivyo, Waislamu walionekana kushinda, hata hivyo kufuatia kughafilika na baadhi yao kuasi amri ya Mtume (saw) aliyewataka kuendelea kubakia mlimani, Waislamu hao walishuka mlimani kwa tamaa za kupata ngawira hali iliyowafanya washirikina kuwashambulia na kudhoofika nguvu na uwezo wao. Waislamu 70 waliuawa shahidi katika vita hivyo akiwemo Hamza, ami yake Mtume (s.a.w). Hata hivyo washirikina hawakuweza kupata ushindi kamili na hivyo wakalazimika kurejea Makka.

Siku kama ya leo miaka 468 iliyopita, Kongamano la Augsburg lilifanyika katika mji wenye jina hilo huko nchini Ujerumani. Katika kongamano hilo, viongozi wa Kikatoliki chini ya uongozi wa Papa Paul IV (wa Nne) kwa mara ya kwanza waliunga mkono uhuru wa madhehebu ya Waprotestanti. Katika kongamano hilo pia ulichukuliwa uamuzi wa kurejeshwa mali za Waprotestanti walizokuwa wamenyang'anywa. Hata hivyo uamuzi huo haukutekelezwa na hivyo kuzusha vita vya miaka kumi kati ya Waprotestanti na Wakatoliki katika nchi mbalimbali za Ulaya.

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, Benito Mussolini dikteta wa Kifashisti wa Italia aliuawa kwa kunyongwa na wazalendo wa nchi hiyo. Mussolini alizaliwa Julai 29 mwaka 1883 katika familia masikini huko kaskazini mwa Italia. Baada ya kumaliza masomo yake ya Chuo Kikuu alianza kufanya kazi ya uandishi katika magazeti. Machi 23 mwaka 1919 Mussolini alistafidi na uasi na hali ya vurugu iliyojitokeza  nchini italia na kuanzisha Chama cha Ufashisti na kuwa kiongozi wa chama hicho. Ushindi wa chama hicho katika uchaguzi wa 1922 ulimfanya Benito Mussolini kuwa Waziri Mkuu baada ya kumridhisha mfalme.

Benito Mussolini

Siku kama hii ya leo miaka 51 iliyopita inayosadifiana na tarehe 7 Shawwal 1393 Hijria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul Hussein Shaarani mfasiri wa Qurani Tukufu inayojulikana kwa jina la 'Manhaj Swadiqiin', akiwa na umri wa miaka 73. Msomi huyo licha ya kubobea katika elimu za kidini alikuwa mahiri katika kuzungumza lugha za kigeni kama vile Kifaransa, Kiingereza na Kiarabu. Licha ya kuonyesha uwezo wake katika tafsiri ya Qurani Tukufu ya Manhaj Swadiqiin chenye juzuu 10 aliacha athari ya kitabu cha Sharh Kifayatil Usul.

Ayatullah Mirza Abul Hussein Shaarani

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita Marekani ililazimika kuondoka kwa madhila huko Vietnam baada ya kupata kipigo cha kuaibisha. Majeshi ya Marekani yaliingia Vietnam kwa shabaha eti ya kukabiliana na kasi ya kuenea ukomonisti na kukabiliwa na mapambano makali ya wapiganaji waliokuwa maarufu kwa jina la Viet Cong huko Vietnam ya kaskazini. Katika vita hivyo Marekani ilitumia silaha zote zilizopigwa marufuku isipokuwa silaha za nyuklia. Wapiganaji hao wa mwituni walifanikiwa kutoa kipigo kikali kwa majeshi ya Marekani na tarehe 28 Aprili mwaka 1975 Rais Richard Nixon wa Marekani aliwaamuru wanajeshi wa nchi hiyo kuondoka Vietnam.

Vita vya Vietnam

Tarehe 8 Ordibehesht miaka 35 iliyopita watawala wa kizazi cha Aal Saud walikata uhusiano wa Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya utawala wa Saudia kufanya mauaji ya umati ya mahujaji wa Wairani wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu mjini Makka katika siku iliyopewa jina la Ijumaa ya Damu hapo tarehe 9 Mordad 1366 Hijria Shamsia, uhusiano wa Iran na nchi hiyo ulifika kiwango cha chini zaidi na wanadiplomasia wa Iran nchini Saudia wakapunguzwa kwa kiasi kikubwa. Wanadiplomasia wa Saudia mjini Tehran walikuwa tayari wamekwishaondoka. Hatimaye uhusiano wa nchi hizi mbili ulikatwa kikamilifu tarehe 28 Aprili 1986. Safari za Wairani waliokuwa na hamu ya kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Makka na Harama tukufu ya Mtume Muhammad (saw) mjini Madina pia zilisimamishwa kwa kipindi cha miaka mitatu.Uhusiano wa nchi hizo mbili ulikatwa katika kipindi ambacho Saudi Arabia ilikuwa msaidizi mkubwa wa kifedha wa utawala wa Saddam Hussein katika vita vyake dhidi ya Iran na hatua hiyo ilichukuliwa sambamba na siasa za Marekani za kubana na kuzidisha mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mauaji ya halaiki dhidi ya mahujaji wa Kiirani

Miaka 31 iliyopita katika siku kama ya leo, makundi ya Mujahidina wa Afghanistan hatimaye yalipata ushindi baada ya mapambano ya miaka 13 dhidi ya jeshi la Urusi ya zamani na serikali ya kibaraka ya nchi hiyo. Baada ya majeshi ya Urusi ya zamani kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa miaka 13, hatimaye mwezi Februari mwaka 1989 wanajeshi hao wa Urusi walilazimika kuondoka Afghanistan. Hata hivyo kutokana na makundi hayo ya Kiafghani kutokuwa na mikakati mizuri na pia kutopata misaada kutoka nje, vikosi vya serikali ya Afghanistan viliendelea kubakia madarakani chini ya uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Urusi ya zamani. Aprili 28 Mujahidina walifanikiwa kuuteka kikamilifu mji wa Kabul na kuiondoa madarakani serikali kibaraka ya Afghanistan.

اBendera ya Afghanistan

 

Tags