Jun 09, 2023 01:23 UTC
  • Ijumaa, tarehe 9 Juni, mwaka 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 20 Dhulqaada 1444 Hijria sawa na Juni 9 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 1955 iliyopita inayosadifiana na tarehe 9 Juni mwaka wa 68 Milaadia, Mfalme Nero Claudius Caesar mtawala katili na aliyemwaga damu nyingi wa Rome alijiua, baada ya kuishi kwa miaka 31 na kutawala kwa maiaka 14. Si vibaya kuashiria hapa kwamba Nero aliasiliwa na mjomba wake Mfalme Claudius aliyekuwa mtawala wa kwanza wa Rome. Lakini Nero alimpa sumu mfalme huyo na kuchukua nafasi yake baada ya kufa. Mfalme huyo katili na wa mwisho wa Rome, wakati wa utawala wake aliwaua watu wengi wa familia yake akiwemo mama yake, mkewe, kaka yake na ndugu zake wengine. Pia aliwaua wananchi wake wengi. Aliwaua kwa umati Wakiristo pamoja na kuuchoma moto mji wa Rome.

Nero Claudius Caesar

Miaka 988 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 20 Dhulqaada mwaka 456 alifariki dunia Abu Ali Qirawani, mshairi, mwanafasihi na mkosoaji wa fasihi wa Morocco. Abu Ali alijifunza mashairi, fasihi na elimu nyingi za kipindi hicho akiwa bado mdogo na baada ya hapo alielekea katika mji wa Qirawan nchini Tunisia kwa shabaha ya kushiriki katika vikao na majlisi za wasomi wakubwa. Kipindi hicho mji wa Qirawan ulikuwa kituo kikuu cha ustaarabu wa Kiislamu huko kaskazini mwa Afrika na Andalusia na wasomi wa Kiislamu na wanazuoni wengi mashuhuri walikuwa wakiishi katika mji huo. Mashairi mengi ya malenga huyo yanaakisi vipindi mbalimbali vya maisha yake ya kijamii. Mshairi huyo aligundua mbinu mpya ya kukosoa kazi za fasihi na kuacha athari nyingi katika uwanja huo.

Miaka 138 iliyopita muwafaka na leo, jeshi la Ujerumani lilivamia ardhi ya Togo huko magharibi mwa Afrika. Wakati huo maeneo ya pwani ya Togo yalipendelewa zaidi na watu wa Ulaya kwa ajili ya biashara ya utumwa. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Togo imekuwa maarufu kwa jina la "Pwani ya Utumwa." Wakoloni wa Ujerumani waliendelea kuikalia kwa mabavu ardhi ya Togo hadi wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Baada ya hapo Togo ilikoloniwa na Wafaransa na Waingereza. Nchi hiyo ilipata uhuru mwaka 1960.

Bendera ya Togo

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita moto mkubwa ulitokea katika Chuo Kikuu cha Algiers mji mkuu wa Algeria. Moto huo ulichoma zaidi ya nakala laki tano za vitabu vyenye thamani kubwa zilizokuwa kwenye maktaba ya chuo hicho. Asilimia kubwa ya vitabu vilivyoungua vilikuwa miongoni mwa marejeo muhimu na nadra. Chuo Kikuu cha Algiers na maktaba yake vilichomwa moto na jeshi la siri la Ufaransa nchini Algeria. Jeshi hilo la siri liliundwa na askari wa Ufaransa waliokuwa wakipinga suala la kupewa uhuru Algeria. Moto huo ulikuwa miongoni mwa makumi ya mioto kadhaa iliyotokea katika siku hiyo nchini Algeria na mingi ilisababishwa na jeshi la siri la Ufaransa.

Maktaba ya Chuo Kikuu cha Algiers

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Hassan Ilahi Tabatabai, mmoja wa maulamaa na wataalamu wa elimu ya irfani. Sayyid Muhammad Tabatabai alizaliwa Tabrizi huko kaskazini mwa Iran mwaka 1325 Hijiria. Akiwa na miaka 19 alielekea  Najaf, Iraq akiwa na kaka yake mkubwa, Allamah Muhammad Hassein Tabatabai na kupata elimu ya dini katika mji huo. Baada ya kutabahari katika taaluma za Kiislamu alirejea eneo alikozaliwa la Tabriz na kujishughulisha na malezi na kueneza elimu na maarifa yya Kiislamu. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha Uhusiano wa Kimaanawi Baina ya Roho na Sauti. 

Ayatullah Sayyid Muhammad Hassan Ilahi Tabatabai