Al-Azhar: Wanawake Waislamu ndio waathiriwa wakuu wa ubaguzi barani Ulaya
-
Al-Azhar: Wanawake Waislamu, waathiriwa wakuu wa ubaguzi barani Ulaya
Taasisi ya Kiislamu ya Al-Azhar nchini Misri imeonya kuhusu mashaka yanayowapata wanawake Waislamu barani Ulaya kutokana na ubaguzi.
Ni baada ya ripoti rasmi na hitimisho la Umoja wa Ulaya kuonyesha kwamba ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya Waislamu katika nchi nyingi wanachama ni endelevu na unaongezeka, na kwamba wanawake Waislamu ndio walio katika hatari zaidi ya kutukanwa, kufukuzwa kazini na mashinikizo ya kijamii kuliko watu wengine kutokana na mavazi yao na kutambulika utambulisho wao wa kidini.
Al-Azhar imetangaza kwamba wanawake Waislamu ndio wanaoteseka zaidi kutokana na ubaguzi barani Ulaya. Imesisitiza kwamba ubaguzi wa kimbari dhidi ya Waislamu si tukio la kupita, bali umejikita sana katika taasisi za kisiasa na vyombo vya habari, jambo linaloashiria mmomonyoko wa kimaadili wa Ulaya. Al-Azhar pia imesisitiza haja ya kutambuliwa rasmi kuwepo "ubaguzi wa kimfumo" barani Ulaya na kupitishwa sheria zinazotambua chuki dhidi ya Uislamu kuwa ni kosa la jinai.
Taarifa hiyo imesema, asilimia 47 ya Waislamu katika nchi za Umoja wa Ulaya walikumbana na ubaguzi wa moja kwa moja mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 39 mwaka 2024.
Finland imerikodi kiwango cha juu zaidi cha ubaguzi dhidi ya Waislamu katika soko la ajira kwa asilimia 63, na uhalifu wa chuki dhidi ya Waiislamu nchini Austria umefikia visa 1,500, kiwango ambacho ni cha juu zaidi tangu 2015.
Ripoti hiyo inasisitiza kwamba wanawake Waislamu, hasa wale wanaovaa hijabu, wameathiriwa zaidi na ubaguzi na kutengwa katika soko la ajira barani Ulaya.
Takwimu za ripoti hiyo zinaonyesha kuwa asilimia 31 ya wahamiaji Waislamu waliripoti ubaguzi wa jumla, na asilimia 74.82 kati yao waliripoti ubaguzi walipojaribu kupata makazi.
Takwimu rasmi nchini Uhispania zinakanusha madai kwamba wahamiaji Waislamu wanasababisha matatizo ya kiuchumi kwa nchi hiyo. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Waislamu wanachangua asilimia 10 ya mapato ya hifadhi ya jamii huku wakinufaika na asilimia 1 pekee ya hifadhi hiyo.
Nchini Uingereza, matukio ya chuki dhidi ya Waislamu yameongezeka sana huku kukiwa na mkwamo wa kisiasa kuhusu ufafanuzi wa chuki dhidi ya Uislamu.
Nchini Ufaransa, mashambulizi dhidi ya misikiti yaliongezeka mwaka uliomalizika wa 2025 kwa kisingizio cha kulinda mfumo wa kisekulari.
Huko Ujerumani, uhamiaji unahusishwa na usalama, na maandamano yanayounga mkono Wapalestina yanadhibitiwa vikali. Nchini Denmark na Austria pia, ubaguzi wa rangi umefanywa kuwa jambo la kawaida katika maisha ya kila siku.