Jun 19, 2023 09:24 UTC
  • Jumatatu, tarehe 19 Juni, 2023

Leo ni Jumatatu tarehe 30 Dhulqaada 1444 Hijria sawa na tarehe 19 Juni 2023.

Siku kama ya leo miaka 1223 iliyopita, yaani siku ya mwisho ya mwezi Dhulqaada mwaka 220 Hijria Imam Muhammad Taqi (as) mmoja kati ya wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Mtukufu huyo alipewa jina la 'Jawad' likiwa na maana ya mtu mkarimu sana kutokana na ukarimu wake mkubwa. Imam Jawad alizaliwa katika mwezi wa Ramadhani mwaka 195 Hijria na kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ridha (as). Kipindi cha maisha ya Imam Jawad kilikuwa kipindi cha kuchanua utamaduni wa Kiislamu na kuenea kwa fikra, itikadi na falsafa na kujitokeza mifumo ya fikra za Kimagharibi za Wagiriki na Warumi katika ulimwengu wa Kiislamu. Imam alifanya juhudi kubwa kulea kizazi chenye maarifa na kueneza elimu na mafundisho sahihi ya Uislamu kama njia ya kukabiliana na fikra za kigeni sambamba na kufichua siri na maovu ya watawala wa Bani Abbas. Suala hilo liliwakasirisha mno watawala hao ambao hatimaye waliamua kumuua shahidi mjukuu huyo wa Mtume (SAW) katika siku kama hii ya leo.

Siku kama ya leo miaka 156 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1867, Maximilian mwana wa mfalme wa Austria ambaye aliikalia kwa mabavu Mexico, alinyongwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo. Baada ya Benito Juarez kujinyakulia urais wa Mexico mwaka 1855, aliwakata mikono wazungu na kupunguza nguvu za Kanisa nchini Mexico. Hatua hiyo iliwakasirisha mno wazungu na wakoloni wa Ulaya waliokuwa wakiongozwa na Ufaransa, na kulazimika kutuma jeshi nchini Mexico kwa shabaha ya kulihami Kanisa pamoja na wawekezaji nchini humo. 

Siku kama ya leo miaka 146 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1877, Enrico Forlanini mhandisi wa Kiitalia alifanikiwa kufanya majaribio ya kwanza ya kurusha angani helikopta katika mji wa bandari wa Alexandria nchini Misri. Helikopta hiyo iliboreshwa zaidi na mtaalamu wa Kipolandi, na ubunifu huo ukaandikwa kwa jina lake.   

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita nchi ya Kuwait iliyoko katika eneo la Ghuba ya Uajemi ilijipatia uhuru baada ya kufutwa makubaliano ya ukoloni ya mwaka 1899 kati ya Uingereza na Kuwait. Katikati ya karne 18, iliasisiwa silsila ya al Swabah nchini humo na ilipofikia mwishoni mwa karne ya 19, Kuwait iliomba uungaji mkono wa Uingereza kwa shabaha ya kukabiliana na dola la Othmaniya. Mwaka 1899, Uingereza na Kuwait zilifanya makubaliano ambayo yaliiweka Kuwait chini ya ukoloni wa Uingereza.   

Bendera ya Kuwait

Na Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, sawa na tarehe 29 Khordad 1356 Hijria Shamsia, alifariki dunia Dakta Ali Shariati mwandishi na msomi wa zama hizi wa Kiirani mjini London, Uingereza. Dakta Shariati alipata elimu yake ya juu katika taaluma ya fasihi sambamba na kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya utawala wa mfalme hapa nchini. Dakta Shariati alikuwa bega kwa bega na Shahidi Mutahhari na Shahidi Bahonar, katika kuanzisha Husseiniya ya Ershad mjini Tehran kwa shabaha ya kuzikomaza fikra za tabaka la vijana. Ameandika zaidi ya vitabu 200 na miongoni mwao ni 'Uislamu na Mwanadamu', 'Historia ya Ustaarabu' na 'Fatima ni Fatima'.   

Dakta Ali Shariati

 

Tags