Jumatano tarehe 5 Julai 2023
Leo ni Jumatano tarehe 16 Dhulhija 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 5 Julai mwaka 2023.
Tarehe 14 Tir katika kalenda ya Iran imepewa jina la Siku ya Kalamu. Kwa hakika kalamu huhifadhi elimu, maarifa na ni mlinzi wa fikra za wanazuoni na wanafikra na hivyo ni kiunganishi cha kifikra na daraja la mawasiliano baina ya watu wa zamani na wa leo. Aidha hata mawasiliano baina ya mbingu na ardhi yamepatikana kupitia kalamu. Hivyo basi kalamu ni mtunza siri wa mwanadamu na hazina ya elimu na mkusanyaji wa tajiriba za karne nyingi. Na kama tunaona katika Qur’ani Mwenyezi Mungu ameapa kwa kalamu kwa kusema: "Nuun. Naapa kwa kalamu na yale wayaandikayo", basi hilo linatokana na umuhimu wa jambo hili, kwani kiapo mara nyingi hufanywa kwa jambo au kitu ambacho kina thamani na chenye kuheshimiwa mno.
Siku kama ya leo miaka 212 iliyopita, nchi ya Venezuela ilijitangazia uhuru wake na kwa sababu hiyo, tarehe 5 Julai, hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo. Tangu mwanzoni mwa karne ya 16 Miladia, na kwa kipindi cha karne tatu Venezuela ilikuwa chini ya ukoloni wa Uhispania. Katika kipindi cha ukoloni huo, raia wa nchi hiyo walipatwa na matatizo mengi, kiasi kwamba makumi ya maelfu ya Wahindi Wekundu ambao ni raia asili wa taifa hilo waliuawa na mahala pao kuchukuliwa na Wahispania. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, mapambano ya wananchi yalianza chini ya uongozi wa Francisco Miranda na kuzaa matunda katika siku kama ya leo mwaka 1811.
Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita, alifariki dunia Nicéphore Niépce, mvumbuzi wa kamera. Niépce alifanikiwa kusajili kwa mara ya kwanza uvumbuzi huo, mnamo mwaka 1826, baada ya kufanya majaribio kadhaa ya kielimu katika uwanja huo.
Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, wananchi wa Algeria walipata uhuru dhidi ya wavamizi wa Ufaransa baada ya mapambano makali na ya muda mrefu na wavamizi hao. Ufaransa iliikalia kwa mabavu Algeria kwa kutegemea jeshi lake kubwa mnamo mwaka 1830. Kwa kipindi cha miaka 130 ya kukoloniwa taifa hilo, raia wa Algeria waliasisi harakati kadhaa za kupigania uhuru zilizokuwa zikiongozwa na Amir Abdulqadir al Jazairi, ambazo hata hivyo zilikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa jeshi la Ufaransa. Hata hivyo harakati hizo zilishika kasi zaidi na kuzaa matunda baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia na kujipatia uhuru wake miaka 53 iliyopita katika siku kama ya leo.
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, Jenerali Muhammad Zia-ul-Haq alifanya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali ya Zulfiqar Ali Bhutto nchini Pakistan. Muhammad Zia-ul-Haq alitwaa madaraka yote ya waziri mkuu na rais wa Jamhuri ya Pakistan na mbali na kuwanyonga Zulfiqar Bhutto na wapinzani wake wengine, alivunja mabunge ya nchi hiyo na kusimamisha shughuli zote za vyama vya siasa nchini Pakistan. Zia-ul-Haq aliuawa katika ajali ya ndege akiwa na maafisa kadhaa wa jeshi la Pakistan, na utawala wake ukakomea hapo.