Ijumaa, tarehe 7 Julai, 2023
Leo ni Ijumaa tarehe 18 Dhulhija 1444 Hijria sawa na Julai 7 mwaka 2023.
Siku kama hii ya leo miaka 1434 iliyopita Mtume Muhammad (SAW) akiwa katika safari yake ya mwisho ya Hija, kwa amri ya Mwenyezi Mungu alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib AS kuwa kiongozi wa Waislamu wote baada yake. Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu ilifanyika katika eneo linalojulikana kwa jina la Ghadir Khum katika makutano ya njia ya Makka na Madina. Siku hiyo Mtume SAW alitoa hotuba mbele ya hadhara kubwa ya Waislamu kisha akashika mkono wa Ali bin Abi Twalib na kusema: "Kila mtu ambaye mimi ni kiongozi wake basi huyu Ali pia ni kiongozi wake. Mwenyezi Mungu ampende atakayempenda, na amfanyie uadui atakayemfanyia uadui." Mtume SAW pia aliwausia Waislamu kushikamana na Qur'ani na Ahlubaiti wake na akasema viwili hivyo havitatengana hadi vitakapomkuta yeye katika Hodhi ya Kauthar, Siku ya Kiyama.

Siku kama ya leo miaka 772 iliyopita, alifariki dunia Nasiruddin Tusi, mwanafalsafa, mtaalamu wa hesabati na nujumu na msomi mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Tus, kaskazini mashariki mwa Iran. Nasiruddin Tusi aliishi katika kipindi cha Hulagu Khan Mongol na aliasisi kituo kikubwa na cha kwanza cha sayansi ya nujumu huko Maraghe kaskazini magharibi mwa Iran. Nasiruddin Tusi ameandika vitabu zaidi ya 80 kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi. Vitabu muhimu zaidi vya msomi huyo ni pamoja na ‘Asasul-Iqtibaas’, ‘Akhlaaq Naaswiri’, ‘Awsaful-Ashraaf’ na ‘Sharhul Ishaarat.

Tarehe 18 Dhulhija miaka 230 iliyopita alizaliwa faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Murtadha Ansari katika mji Dezful nchini Iran na baada ya kupata elimu ya msingi kwa baba yake alielekea katika miji mitakatifu ya Karbala na Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Miaka kadhaa baadaye Sheikh Ansari alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni na walimu mashuhuri wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Rasaail na Makaasib ambavyo vingali vinatumiwa hadi sasa kufundishia katika vyuo vikuu vya kidini.
Miaka 216 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, ulitiwa saini mkataba wa kihistoria wa Tilsit katika mji wenye jina hilo huko Russia kati ya Alexander wa Kwanza, mfalme wa Russia na Napoleon Bonaparte wa Ufaransa. Kwa mujibu wa mkataba huo Urusi na Ufaransa zilikubaliana kuwa, ikiwa nchi yoyote ingeishambulia nchi moja wapo kati ya hizo, zingesaidiana kumpiga adui. Mkataba huo wa urafiki, uliendelea hadi mwaka 1810.
Katika siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, tarehe 16 Tir 1301 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Zainul Abidin Marandi. Msomi huyo mkubwa alisoma elimu za awali katika mji aliozaliwa wa Marand, huko katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki nchini Iran. Baada ya hapo alielekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa kama vile Ayatullah Sayyid Mohammed Hassan Husayni Nouri Shirazi na Habib Allah Rashti. Baada ya muda fulani Ayatullah Marandi alikuwa marjaa taqlidi katika maeneo ya Azerbaijan na hatimaye akafariki dunia siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 72 na kuzikwa katika makaburi ya Wadi-al Salaam mjini Najaf.

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, visiwa vya Solomon vilivyoko kaskazini mashariki mwa Australia katika bahari ya Pacific vilipata uhuru. Visiwa hivyo viligunduliwa na watu kutoka Ulaya mwaka 1567. Mwaka 1885 Ujerumani ilidai umiliki wa visiwa vya kaskazini mwa Solomon na ndiyo maana ikachukua hatua ya kuvishambulia na kisha kuvikalia kwa mabavu. Muongo mmoja baadaye, Uingereza ilivishambulia visiwa hivyo na kuvidhibiti. Harakati ya kupigania uhuru ilianzishwa katika visiwa hivyo baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kuzaa matunda katika tarehe kama ya leo ambapo visiwa hivyo vilipata uhuru.

Na tarehe 7 Julai mwaka 2005 kulitokea mlipuko katika basi na milipuko mingine katika vituo vitatu vya treni ya chini ya ardhi katikati mwa mji mkuu wa Uingereza, London na kusababisha vifo vya watu 50 na wengine wapatao 700 kujeruhiwa. Mashambulio hayo yalifanywa sambamba na kikao cha Viongozi wa Nchi Tajiri Kiviwanda Duniani G8 huko nchini Scotland kaskazini kwa Uingereza. Mashambulio hayo ya mabomu yalitekelezwa ili kupinga ushirikiano wa London na Washington katika kuikalia kwa mabavu Afghanistran na Iraq na kuuawa kiholela wananchi wa nchi hizo. Serikali ya Uingereza ilidai kwamba, Waislamu walihusika na tukio hilo, na kwa muktadha huo mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Uingereza yaliyoanza baada ya mashambulio ya Septemba 11, 2001 yakashadidi zaidi.