Dec 28, 2023 09:31 UTC
  • Kuongezeka idadi ya watu wanaotumia intaneti duniani mwaka 2023

Karibuni wasikilizaji wapendwa wa Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran katika kipindi chetu cha makala ya wiki ambapo tutatupia jicho ongezeko la watumiaji wa intaneti duniani mwaka 2023.  

Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa mwaka wa 2023, watumiaji wa Intaneti wamekuwa mtandaoni yaani (online) kwa zaidi ya saa trilioni 1.3. Maisha ya mwanadamu kila siku yanaunganishwa zaidi na ulimwengu wa kidijitali. Chunguzi mbalimbali zinaonyesha kuwa, kwa wastani, kila mtu hutumia karibu masaa saba kutazama skrini za simu, tarakilishi na kadhalika kila siku kwa ajili ya kazi, burudani au mawasiliano.

Kama ambavyo ustawi na hali bora ya kimwili inatofautiana kutoka eneo moja hadi jingine, vivyo hivyo ustawi wa kidijitali.

Kulingana na Kielezo cha Ubora wa Maisha ya Kidiijitali kwa mwaka 2023 cha SurfShark, baadhi ya nchi zimefanya vyema zaidi kuliko nyingine katika kutoa huduma za mtandao na za kidijitali kwa bei nafuu na hivyo kusababisha ustawi bora wa kidijitali miongoni mwa jamii.

Ustawi wa kidijitali umeainishwa kwa mujibu wa vigezo vikuu vitano ambavyo ni upatikanaji wa huduma ya intaneti kwa bei nafuu, ubora wa mawasilianao ya haraka na ya kudumu ya intaneti, kupanuliwa miundomsingi ya kielektroniki, kuweza kukabiliana na hujuma za kimtandao, kudumisha ulinzi wa faragha mtandaoni na kuzifanya huduma za serikali kuwa za kidijitali. 

Kila leo kasi ya Intaneti inaongezeka duniani

 

Katika hali ambayo nchi tajiri duniani ambazo aghalabu zina huduma bora za kidijitali kutokana na kuwa na uwezo wa kifedha kwa ajili ya uwekezaji na kuboresha vigezo vinavyojitajika; nchi 22 miongoni mwazo ambazo zimepindukia matarajio yao katika Pato la Taifa kwa mwaka zimepata alama za juu katika upande wa usalama wa kielektroniki, miundombinu na katika kutoa huduma za serikali kwa njia ya kielektroniki. Akthari ya nchi hizo ni kutoka Asia na Ulaya Mashariki.

Watu duniani kote wanatumia zaidi ya robo ya muda wao katika intaneti, na zaidi ya asilimia 60 ya jamii ya watu duniani wanatumia mitandao ya kijamii.  Takwimu hizi zimechapishwa katika ripoti ya karibuni zaidi ya DataReportal, maktaba ya marejeleo ya mtandaoni yenye mamia ya ripoti na data zisizolipishwa, katikati ya 2023. Ripoti hiyo imeonyesha kuongezeka maradufu kiwango cha kukubalika mitandao ya kijamii kimataifa katika miaka 8 iliyopita.

Takwimu na viwango vyote hivi vimebeba ujumbe wa wazi kwamba: Intaneti na mitandao ya kijamii ni sehemu ya dharura ya maisha ya mwanadamu wa leo, na kwamba kama unataka kuvutia maoni ya watu basi jambo hilo linapaswa kutimia kupitia intaneti na mitandao ya kijamii. Swali muhimu la kujiuliza hapa ni kuwa, je, watu huwa wanatafuta muhtawa na maudhui yepi mtandaoni? Na Je, ni tovuti na programu gani zinazovuwatia zaidi? na je, watumiaji hulipia aina gani ya maudhui ya kidijitali?

Tangu 2013, kikundi cha uchanganuzi wa data cha Domo kimekuwa kikichapisha ripoti ya kila mwaka iliyopewa jina la "Data Never Sleeps" ambayo ina maelezo ya takwimu za mwaka za Intaneti. Kulingana na ripoti hiyo, idadi ya watumiaji wa mtandao mwaka huu wa 2023 ilikuwa watu bilioni 5.2, ambayo inaonyesha ongezeko kubwa la idadi ya watu bilioni 4.5 ikilinganishwa na mwaka 2020.

Miongoni mwa takwimu zilizotolewa mwaka 2023, tunaweza kuashiria utumaji wa barua pepe yaani E-mail milioni 241 katika muda wa dakika moja; ambapo kiwango hiki mwaka uliopita wa 2022 kilikuwa barua pepe milioni 231.4 kwa dakika moja. Aidha utafutaji milioni 6.3 ulifanyika kwenye Google, kiwango kinachotajwa kuongezeka kwa 6.7 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, katika kila sekunde 60, watumiaij wa intaneti duniani kote walikuwa online kwa jumla ya masaa milioni 25.1; na kwa utaratibu huu tunaweza kusema kuwa, walimwengu wametumia zaidi ya masaa trilioni 1.3 mtandaoni.

Katika sekta ya habari, mada iliyotafutwa na kufuatiliwa zaidi katika intaneti mwaka huu 2023 ilihusiana na vita huko Gaza. Neno nyambizi ya Titan lilishika nafasi ya pili, na nafasi ya tatu ilichukuliwa na tetemeko la ardhi la Uturuki.

World Wide Web

 

Miongoni mwa vipengele muhimu katika kuchunguza idadi ya watu wanaoingia mtandaoni ni mitandao ya kijamii. Mitandao hii ya kijamii ni vyombo vya mawasiliano ambavyo ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na maisha ya mabilioni ya watu.  

Uchambuzi wa kina wa ripoti za taasisi za utafiti na kampuni ambazo zinafanya kazi katika uwanja wa kuchanganua mienendo ya watumiaji wa mitandao unaonyesha kuwa kiwango cha kukubalika mitandao ya kijamii kimeongezeka maradufu katika miaka 8 iliyopita. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwezi Julai mwaka 2015 chini ya asilimia 30 ya jamii ya watu duniani walikuwa wakitumia mitandao ya kijamii. Idadi hii iliendelea kuongezeka haraka katika miaka iliyofuatia na kufikia karibu asilimia 51 ya watu duniani mnamo Julai 2020, wakati wa kilele cha karantini na utekelezaji wa hatua nyingine za kuzuia maambukizi wakati wa janga la Corona.

Kiwango cha kukubalika mitandao ya kijamii mwezi Julai mwaka huu kiliongezeka kwa asilimia 2.8 ikilinganishwa na wakati kama huo mwaka wa kabla yake jambo linaloonyesha kwamba sambamba na ongezeko la idadi ya watu duniani, kukubalika mitandao ya kijamii kinaogezeka na kupanda juu kimataifa.

Ripoti ya kampuni ya utafiti wa masoko ya GWI inaonyesha kuwa muda uliotumiwa na watu katika mitandao ya kijamii mwaka 2023 umepungua kwa dakika 3 ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha mwaka uliopita, lakini wastani wa matumizi ya mitandao ya kijamii bado unatofautiana kwa kiasi kikubwa baina ya nchi na nchi.

Swali jingine linalojitokeza ni kwamba: Ni mitandao gani ya kijamii ambayo watumiaji kote ulimwenguni hutumia zaidi? Kulingana na habari zilizochapishwa, mitandao kumi maarufu ya kijamii inayopendwa zaidi baina ya watumiaji wenye umri wa kati ya miaka 16 hadi 64 ni: WhatsApp, Instagram, Facebook, Wechat, Tik Tok, Douyin, X (Twitter), Facebook Messenger, Telegraph na Line.

Licha ya kushika nafasi ya pili, Instagram bado ni fursa muhimu kwa alama za biashara (brands), huku zaidi ya asilimia 62 ya watumiaji wa Instagram wakitumia jukwaa hilo kufanya utafiti kabla ya kununua au kutazama maudhui za chapa. Takwimu hizo pia zimethibitishwa na ripoti ya Kituo cha Kukuza Biashara ya Mtandaoni cha Iran ambapo miongoni mwa mitandao tofauti ya kijamii, Instagram yenye hisa ya asilimia 55 inaongoza kati ya majukwaa ya kijamii ya Iran kwa kuwa na watu wengi wanaotumia mtandao kununulia bidhaa mbalimbali.

Licha ya takwimu hizi zote zinazoongezeka, matokeo ya uchunguzi yanaonyesha kuwa upatikanaji wa huduma ya intaneti unasalia kuwa changamoto kubwa kwa vikundi vya kijamii vilivyo hatarini zaidi, na suala la uwezo wa kupata huduma za gharama nafuu siku zote limekuwa kizuizi kikuu.

Takwimu zinaonyesha kuwa, maka jana, huduma za intaneti ziliongezeka kwa asilimia 93 kwa watu wa Umoja wa Ulaya. Walakini, data zinaonyesha kuwa, mamilioni ya raia wa EU bado hawakuweza kulipia gharama za kuunganisha huduma za intaneti mwaka jana.

Idadi ya watumiaji wa intaneti na mitandao ya kijamii nchini Iran pia imeongezeka kwa asilimia saba mwaka wa 2023. Kiwango cha kusambaa mtandao wa intaneti nchini Iran kimefikia takriban 80% na kuna karibu watumiaji milioni 70 wa Intaneti hapa nchini.  

                                                                     ***********

Makala yetu ya wiki hii inaishia hapa kwa leo. Tukutane wiki ijayo panapo majaliwa yake Mola Muumba.

Tags