Mabomu ya Marekani yanavyoua watoto Ukanda wa Gaza
Baada ya kupita miezi mitatu ya mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ukanda wa Gaza, eneo hilo sasa limegeuka na kuwa kaburi kubwa zaidi la watoto kuwahi kushuhudiwa duniani.
Mamia ya watoto wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza wanauliwa shahidi kila siku kwa ndege za kivita na mabomu ya Marekani. Hadi sasa watu zaidi ya elfu 20 wameuliwa shahidi kwa ndege za kivita na mabomu ya Marekani na nusu ya idadi hiyo ni watoto. Ripoti ya maafisa wa sekta ya afya wa Ukanda wa Gaza inaeleza kuwa, maelfu ya watu wengine wangali chini ya vifusi ya nyumba na majengo yaliyobomolewa katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni. Vilevile watoto 100 wa Kipalestina waliuliwa shahidi katika jinai kubwa iliyofanywa na Wazayuni katika mkesha wa Sikukuu ya Krismasi. Miongo kadhaa imepita tangu kubuniwa Azimio la Kimataifa la Haki za Watoto, na nchi zote zilizotia saini, isipokuwa Marekani ambayo bado inakataa kutia kusaini azimio hilo, zimekubali kuwajibika na kuahidi kufanya kila linalowezekana ili kulinda haki na maisha ya watoto hususan wakati wa vita. Kwa mujibu wa azimio hilo, sehemu yoyote duniani ambako watoto watakuwa bila kujali utaifa, jinsia, dini na lugha zao, wanapasa kulindwa na kubakia salama katika hali ya mizozo na vita na kupewa hifadhi katika kambi za zinazosimamiwa na Umoja wa Mataifa na taaasisi zake tanzu. Hata hivyo kwa mtazamo wa nchi za Magharibi zinazodai kutetea haki za watoto, watoto wa Kipalestina ni wanyama wanaofanana na binadamu, kama wanavyosema viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wanajeshi wa Israel wameshindwa kukabiliana ana kwa ana vitani na wanamuqawama wa Palestina; hivyo wanafanya kila wawezalo kusambaratisha mapambano ya Wapalestina kwa kuua watoto na wanawake wa Kipalestina. Licha ya kupita miezi mitatu tangu kuanza mashambulizi ya kikatili ya Wazayuni dhidi ya Gaza, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala huo ameshindwa kufanikisha malengo yake ya awali. Hali hii imelifanya jeshi la Israel lizidishe mauaji ya wanawake na watoto wa Kipaestina huko Gaza. Marekani na nchi za Ulaya zinaodai kutetea haki za binadamu zimekaa kimya mbele ya jinai kubwa za Wazayuni na zinaendelea kutoa misaada ya kifedha na kijeshi kwa Israel. Marekani na washirika wake pia wamekwamisha vikao vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuyapigia kura ya veto maazimio yanayotaka kusimamishwa vita Ukanda wa Gaza na kwa msingi huo moja kwa moja katika maangamizi ya kizazi dhidi ya raia wa Palestina.
Wanajeshi makatili wa Israel hawahurumii hata maiti za Wapalestina. Jinai za Israel dhidi ya Wapalestina tunaweza kuzigawa katika sehemu kadhaa na kila sehemu inahitaji mazingatio makubwa. Katika kipindi cha miaka 75 iliyopita, utawala bandia wa Israel mbali na kuwalenga Wapalestina walio hai hususan watoto wadogo kwa sera zake za kibaguzi na mauaji ya umati, vilevile umekkuwa ukizilenga maiti za Wapalestina kwa vitendo vya kinyama na kikatili.
Kuiba na kuteka maiti za Wapalestina ili kutumia viungo vyao limekuwa jambo la kawaida kwa Wazayuni wa Israel. Kwa maneno mengine ni kuwa, sambamba na mauaji ya kimbari na ya halaiki dhidi ya Wapalestina yanayoendelea kufanywa na Israel na kuwalazimisha kuondoka katika ardhi yao, kuchukua maiti za Wapalestina na kuiba viungo vyao vya mwili pia ni moja ya mbinu zinazotumiwa na Israel kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza. Msemaji wa harakati ya Fat'h ya Palestina, Jamal Nazzal, amesema kuhusu uchunguzi uliofanywa na Misri juu ya wizi wa viungo vya miili ya mashahidi wa Gaza unaofanywa na Israel kuwa: Wapalestina 10,000 wako chini ya vifusi vya nyumba na majengo yaliyobomolewa katika mashambulizi ya Israel na hatimaye yao haijulikani. Gazeti la Al-Yawm al-Sabi linalochapishwa Misri Ijumaa Disemba 29 mwaka jana wa 2023 lilichapisha uchunguzi huo na kuandika: Utawala wa Kizayuni unaiba viungo vya mwili na ngozi za maiti za Wapalestina inazozishukilia kwa muda mrefu. Dk. Marwan al-Hams, Mkurugenzi wa Hospitali ya Mashahidi huko Rafah, Mohammed Yusuf al-Najjar, amefichua kuwa: "Jeshi la Israel limeiba sehemu za miili ya mashahidi wa Kipalestina ambayo iliikabidhi mnamo Disemba 26. Amesisitiza kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limekabidhi lori lililokuwa limejaa miili ya mashahidi wa Kipalestina. Baadhi ya viungo vya miili ya mashahidi hao viliwekwa katika mifuko ya rangi bluu na miili yote haikuwa na viungo muhimu na ilijazwa mchanga." Miongoni mwa ripoti za awali kuhusu wizi wa viungo vya miili ya mashahidi wa Kipalestina ni ile iliyochapishwa na mwandishi wa habari wa kujitegemea Mswidi, Donald Bostrom, katika gazeti la Aftonbladet mnamo tarehe 26 Agosti mwaka 2009 chini ya anwani "Wanapora Viungo vya Miili ya Vijana Wetu". Katika ripoti yake, anataja uzinduzi wa kampeni kubwa iliyolenga kuandikisha umma kwa ajili ya kuchangia viungo baada ya kufariki dunia iliyoanzishwa katika majira ya joto ya 1992 na Ehud Olmert, Waziri wa Afya wa wakati huo wa Israel, kutokana na uhaba wa viungo uliosababisha pengo kati ya usambazaji na mahitaji, na kuandika: Wakati kampeni hiyo ilipokuwa ikitekelezwa, vijana wengi we kiume wa Kipalestina kutoka vijiji vya Ukingo wa Magharibi na Gaza walitoweka; na baada ya siku tano, wanajeshi wa Israel walirudisha maiti zao kwa familia zao wakiwa na majeraha makubwa yaliyoshonwa kwenye miili yao. Donald Bostrom aligundua katika mahojiano yake na familia za Kipalestina alipokuwa akichunguza madai ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kuhusu wizi wa viungo vya miili unaofanywa na Wazayuni, kwamba viungo vya miili ya vijana hao vilinyofolewa kabla ya kuuawa.

Munir Albursh Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Palestina Novemba 18 mwaka jana aliiambia televisheni ya al Jazeera kwamba: Wanajeshi wa Israel wamechukua maiti 130 katika hospitali ya al Shifa kaskazini mwa Gaza na nyingine 15 zilitolewa kwenye kaburi la umati. Miili hiyo ilichukuliwa kwa muda na kisha baadhi ilirejeshwa kwa Wapalestina. Wakati huo huo katika tukio la karibuni kabisa, Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza Disemba 27 mwaka jana ilitangaza kuwa wanajeshi wa Israel wamekabidhi miili iliyokatwakatwa ya Wapalestina 80 waliouliwa shahidi baada ya kunyofoa viungo muhimu bila ya kutaja majina yao au mahali miili hiyo ilipoibwa. Madaktari wa Gaza pia wametoa ushahidi unaothibitisha kuwa miili hiyo ya Wapalestina haikuwa na viungo kama cochlea ya sikio, cornea, maini, figo na moyo.
Kwa hakika utawala wa Kizayuni wa Israel hausiti kutenda jinai ya anina yoyote dhidi ya Wapalestina ili kusambaratisha mapambano ya kishujaa ya raia hao; ikiwa ni pamoja na kufanya mauaji ya kimbari ya watoto na wanawake, kuvunjia heshima miili ya mashahidi, kuiba viungo vyao vya mwili na kuharibu miundo mbinu yote ya Ukanda wa Gaza. Gazeti la Wal Street Journal limesisitiza katika ripoti yake kuwa, vita vya Israel Ukanda wa Gaza vimesababisha uharibifu na maafa ambayo yanaweza kulinganishwa na uharibifu mkubwa wa kivita kuwahi kushuhudiwa katika historia ya sasa na kuandika: Hadi kufikia katikati ya Disemba mwaka jana wa 2023, Israel ilirusha Ukanda Gaza mabomu na makombora zaidi ya 29,000. Aidha karibu asilimia 70 ya nyumba za Gaza zimeharibiwa au kubomolewa kikamilifu. Mashambulizi ya Israel pia yamesababisha maafa na kuharibu makanisa ya Byzantine, misikiti ya kale, viwanda, majengo ya ghorofa, maduka, hoteli za kifahari, sinema na shule. Francesca Albanese, ripota wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataiafa kuhusu Palestina anasema: Kile Israel inachowafanyia Wapalestina hasa raia wa Gaza ni ukatili mkubw zaidi wa karne ya sasa.

Makala yetu ya wiki hii inaishia hapa kwa leo. Tukutane wiki ijayo katika kipindi kingine.