Gaza: Mtihani kwa Dhamiri ya Ulimwengu katika mwaka 2026
https://parstoday.ir/sw/news/event-i135316-gaza_mtihani_kwa_dhamiri_ya_ulimwengu_katika_mwaka_2026
Makala yetu ya wiki inazungumzia hali ya Ukanda wa Gaza ambapo watu wanataabika kutokana na mafuriko, mvua kubwa, nyumba zilizobomoka, na uhaba mkubwa wa chakula na maji ya kunywa katika majira ya msimu wa baridi kali baada ya miaka mingi ya vita na uharibifu unaofanywa na utawala wa Israel.
(last modified 2026-02-15T09:07:51+00:00 )
Jan 10, 2026 06:18 UTC
  • Wapalestina na mateso ya mafuriko, nyumba zilizobomoka, baridi kali n.k.
    Wapalestina na mateso ya mafuriko, nyumba zilizobomoka, baridi kali n.k.

Makala yetu ya wiki inazungumzia hali ya Ukanda wa Gaza ambapo watu wanataabika kutokana na mafuriko, mvua kubwa, nyumba zilizobomoka, na uhaba mkubwa wa chakula na maji ya kunywa katika majira ya msimu wa baridi kali baada ya miaka mingi ya vita na uharibifu unaofanywa na utawala wa Israel.

Mwaka wa 2026 umeanza watu wengi duniani wakiwa na matumaini ya kuwa na mwaka wenye baraka, amani na mafanikio. Hata hivyo katika kona nyingine ya dunia hii, watu wa Gaza, mwaka mpya haujaanza kwa sherehe na furaha, bali kwa baridi kali, mvua, njaa na vifo vya watu wasio na hatia.

Gaza ya leo, ni dhamiri ya dunia na mizani inaoonyesha uzito wa ubinadamu katika mwaka huu mpya.

Gaza, ni eneo linaloonyesha thamani ya ubinadamu katika kukabiliana na mateso ya watu wasio na makazi. Watu wa Ukanda wa Gaza wamekuwa wakiishi kwa miaka mingi kando ya ufukwe wa Mediterania katika mazingira ya hali nzuri ya hewa, majira ya baridi ya wastani na mvua ambazo hapo awali zilitambuliwa kuwa ni baraka kwao. Lakini mwaka huu hali ni tofauti. Msimu wa baridi, hata ukiwa wa kiwango cha chini huwa mgumu sana kwa raia waliolazimika kuhama makazi yao, hasa katika kipindi cha dhoruba kali za Byron iliyopita kwenye anga ya Gaza na kuathiri mji huo. 

Wapalestina na mateso ya msimu wa baridi kali 

Taswira za siku za Jahanamu za vita vya utawala ghasibu wa Israel bado zinaendelea kupita katika fikra za Hamza, mkazi wa Gaza; siku ambazo ziligubikwa na njaa, kiu na mashambulizi mtawalia ya Israel dhidi ya nyumba za raia, shule na hospitali za Gaza. Harufu ya moshi wa risasi na silaha nzito zinahisika katika mji huo ulioharibiwa, na uhai umekuwa kama mwali mdogo wa moto kwenye upepo ukiyoyoma polepole.

Katika moja ya siku hizo zilizojaa moto na moshi, nyumba ya familia ya Hamza katika kitongoji cha Shojaiyeh ilibomolewa katika mashambulizi ya Israel, na miguu ya Hamza ikapondwapondwa chini ya kifusi. Madaktari wa Gaza walitumia suhula chache za kitiba walizokuwa nazo na kumuwekea vyuma miguuni ili aweze kuishi na kuisaidia familia yake. 

Hamza ni miongoni mwa majeruhi 171,000 wa Kipalestina walionusurika katika vita na mauaji ya kimbari ya miaka miwili ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza. Hamza bado hajasahau maumivu aliyopata siku ambayo miguu yake ilipondwapondwa chini ya kifusi baada ya nyumba yao kupigwa na ndege za kivita za Israel. Sasa, maumivu yamemrudia tena yakiandamana na upepo, mvua na baridi kali iliyotanda wingu jeusi katika anga ya Gaza kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Upepo na mvua hiyo kali vinapiga kwa nguvu kwenye hema, na Hamza anaonekana akiwa ameketi juu ya kitanda kikongwe cha mbao kwenye kona ya hema, akiwa amewakumbatia watoto wake ili wasizame kwenye maji ya mafuriko. Hali ya hewa ni ya baridi, na giza na baridi inaingia taratibu ndani ya ngozi na mifupa ya Hamza na wanafamilia wake. Vyuma viliyovyowekwa kwenye miguu iliyovunjika huwa kama barafu ndani ya mwili wakati wa baridi kali, na maumivu yanayompata Hamza kutokana na vyuma hivyo yanazuia usingizi wakati wa usiku. 

Hamza hayuko pekee yake katika hali hii ya mateso; maelfu ya majeruhi katika Ukanda wa Gaza waliowekewa platinamu mikononi na miguuni mwao, wanateseka kwa maumivu hayo hayo. Baridi inachoma mifupa na nyama za miili yao; sawa kabisa na namna vita vya utawala wa Israel vilivyoangamiza maisha yao. ******************                      Hebu sasa jiulize, watoto wa Gaza wanakuwa na hali gani katika mazingira hayo ya baridi kali?

Ilikuwa saa nane usiku wakati upepo na mvua zilipokuwa zikivuma kwa nguvu, na hali ya hewa katika mji wa Khan Yunis ikizidi kuwa baridi. Hema lililochakaa la Hajar na mumewe lilikuwa likipeperushwa na upepo, na hawakuwa na chochote cha kuwakinga mbele ya baridi kali ya kuumiza mifupa. 

Hajar alikuwa amechoka huku akiwa amemkumbatia kifuani Rahaf, mtoto wake mwenye umri wa miezi kadhaa; akimwimbia wimbo wa kubembeleza ili apate kusinzia. Binti huyo mdogo alikuwa dhaifu sana, na kichanga hicho kilikuwa kikisumbuliwa na utapiamlo. Usiku wa manane, Hajar alishtuka kutoka usingizini kutokana na baridi kali na sauti ya matone ya mvua. Hema lilipasuka sehemu kadhaa, na mvua ilikuwa ikiwanyeshea vichwani.

Hajar alinyoosha mkono na kugusa uso wa Rahaf kwenye giza totoro... Uso wake ulikuwa baridi. Rahaf alikuwa ameganda kwa baridi kali na kuwa kama jiwe. Hajar alipiga mayowe kwa hofu na kumkumbatia bintiye, Rahaf. Jitihada za madaktari za kunusuru maisha ya kichanga hicho hazikufua dafu..... 

Saeed Asad Abedin, mtoto wa mwezi mmoja wa Gaza, pia alifariki dunia kutokana na baridi kali, sawa kabisa na Rahaf. Vivyo hivyo, Hadeel Hamdan aliyekuwa na umri wa miaka tisa; alifariki dunia kutokana na baridi kali katika shule ambayo ilikuwa imegeuzwa kuwa kambi ya wakimbizi.

Watoto hawa wameaga dunia kutokana na vita vya mauaji ya kimbari, utapiamlo na baridi kali. Majira ya baridi ya mwaka huu huko Gaza yanatofautiana na majira mengine ya baridi, na ulimwengu unaendelea kutazama tu mateso yanayowapata malaika hawa wasio na hatia. 

Picha nyingine ya Gaza ni ya mandhari ya nyumba zikiporomoka na kuanguka. Mvua inaendelea kunyesha bila kukoma, na sauti ya kupasuka paa zinasikika zikitoa tahadhari. Nyumba zilizonusurika mabomu mwaka jana sasa zimepoteza nguvu na uwezo wa kustahamili. Kuta zimepasuka, dari zimeingiwa na unyevu, na kuna uwezekano kwamba wakati wowote zinaweza kuporomoka na kuanguka chini kutokana na mvua kali na maji yanayoendelea kupenya kwenye kuta zilizopasuka. 

Nyumba zilizobomolewa kufuatia mashambulizi ya Israel Ukanda wa Gaza 

Mitaa yote ya Gaza imejaa matope, maji na vipande vya vifusi vya nyumba zilizobolewa kwa mabomu na makombora ya Kimarekani ya Israel. Watu wanatazama balconi za nyumba kwa hofu, na kila sauti, kila mtetemo, hutia wahka na mtikisiko kwenye roho zao.

Familia ya Yasin ilinusurika kimiujiza wakati sehemu moja ya paa la nyumba yao ilipoporomoka na kuanguka chini kwenye vita, lakini hofu ya kufa chini ya kifusi na mvua inaendelea kuandama fikra na mawazo yao. Familia hii inahofia kwamba paa lililoharibika la nyumba linaweza kuanguka vichwani mwao wakati wowote. Sakafu ya ghorofa ya kwanza katika jengo la makazi ya watu ambapo Ebtisam anaishi ilianguka, na vyumba vyote, jiko na hata vifaa vya nyumbani viliparaganyika barabarani. Sauti ya kuta na vifaa vilivyoanguka huunda mchanganyiko wa hofu na ukosefu wa usalama, na hata wapitanjia wanaotembea kwa miguu mitaani wamejawa hofu na wasiwasi.

Kuanguka kwa nyumba za watu wa Gaza si matokeo ya mvua tu; bali pia kuvuja kwa maji ya mvua na uharibifu wa miundombinu, mitandao ya maji taka na vituo vya kusukuma maji, vyote vimedhoofisha ardhi na majengo. Kuta nyingi, ambazo hapo awali zilikuwa na nyufa ndogo, sasa zinaanguka kwa shinikizo dogo kabisa na uzito wa maji. Amnesty International hapo awali iliripoti kwamba asilimia 81 ya majengo ya Gaza yameharibiwa katika mashambulizi ya Israel. Sasa, hata mvua ya wastani inaweza kusababisha kuanguka kabisa yajengo yaliyoharibiwa.

Picha jumla ya vitongoji vya mji wa Gaza inafanana na ndoto mbaya isiyo na mwisho; vifusi vimerundikana mitaani, nyumba zimeharibiwa nusu, na mahema ya watu waliokimbia makazi yao karibu na majengo yaliyobomolewa, yanaonekana kuchakaa. Watu wa Gaza wanalazimika kutembea kati ya mabaki ya nyumba na mahema yasiyo salama, wakiogopa kwamba paa litawaangukia au kuta zitaporomoka. Kila tone la maji ya mvua, na kila upepo mkali, ni tishio tarajiwa.

Nyumba hizi si tu kwamba si makazi ya watu tu, lakini sasa zimekuwa tishio kwa maisha ya watu wa Gaza. Hata wale waliodhani kwamba wako salama katika majengo yao, wapambana na hofu na wasiwasi mara zote mvua au upepo mkali unapovuma. Mvua iliyochanganyika na udongo na kutengeneza matope, imefanya mahema na mitaa kuteleza, na hivyo kufanya iwe vigumu kupita maeneo hayo. Wakati wowote, kuna uwezekano kwamba nyumba zinaweza kuanguka kabisa na kuua watu, na hakuna mtu aliye na dhamana yoyote ya kubakia hai.

Kwa wale waliokimbia nyumba zao, kambi za wakimbizi zimejaa maji na matope. Mahema mengi yameraruka na hayako salama. Alia Abdullah, mkazi wa kambi hizo anasema: "Nimeloa usiku kucha, na asubuhi rangi ya ngozi yangu ilikuwa imebadilika kabisa. Nimelia sana na kumuomba Mungu asitishe mvua...".       

Vita vimesitishwa lakini hakuna amani hadi sasa. Vivuko vya kutoka na kuingia Gaza vimefungwa na misaada ya kimataifa haijaruhusiwa kuingia ipasavyo kwa ajili ya watu walioathiriwa na vita. Watu wa Gaza wameachwa peke yao, huku mvua na mafuriko yakiendelea kuathiri maisha yao.

Dhoruba kali ya Byron haikuwa mvua na upepo tu; vilevile ni pigo kwa muundo wa mji wa Gaza ambao miundombinu yake imeharibiwa kwa makusudi. Mitandao ya kukusanya maji, mitambo ya kusukuma maji, na mifumo ya maji taka, yote imeharibiwa na jeshi la Israel. Maji ya mvua hayana njia na mifereji ya kuelekea baharini, na ardhi haina uwezo wa kuyameza. Matokeo yake ni mafuriko yanayochanganyika na maji taka ambayo yanaingia kwenye nyumba, mahema, na kuathirii maisha ya watu.

Katika siku chache tu, makumi ya maelfu ya mahema yameharibiwa, majengo yamebomoka na maisha yamepotea. Sasa, wakimbizi wa Gaza wanakabiliana na machaguo mawili hatari: Ama kubakia ndani ya mahema yaliyoraruka au kurudi kwenye nyumba iliyoharibika nusu ambayo paa lake linaning'inia na linaweza kuanguka wakati wowote.

Kipupwe cha Gaza si baridi tu, bali pia kinaambatana na njaa. Zaidi ya watu milioni moja na nusu wanasumbuliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Utapiamlo umefikia viwango vya kutisha, huku watoto na wanawake wajawazito wakiteseka zaidi. Maji salama ya kunywa ni machache, na asilimia 97 ya vyanzo vya maji ya ardhini vimechafuliwa.

Njaa wakati wa baridi hupata maana mpya. Miili dhaifu huzidiwa nguvu haraka na kusalimu amri. Watoto wachanga wa Gaza wanakufa na kuaga dunia kabla ya kupata fursa ya kuishi. Naam, Gaza imekuwa mtihani wa ubinadamu. 

Watu wa Gaza wamevumilia miaka mingi ya vita na mabomu ya utawala wa Israel. Sasa wanakabiliwa na majira ya baridi kali ambayo, kama walimwengu wangetaka, yangekuwa baridi lakini salama, si hatari. Dunia imeziba masikio na haitaki kusikia kilio cha Wapalestina wanaoendelea kuteseka na kufa kwa baridi na njaa.

Mwaka wa 2026 ndio umeanza. Dunia bado ina wakati wa kuamua na kuchukua hatua. Gaza leo si jiografia tu; ni mtihani wa dhamiri ya binadamu. Je, ubinadamu utabakia hai katika mwaka huu mpya au la? Jibu la swali hili linapaswa kutafutwa katika hatima ya watu wa Gaza.