Mar 06, 2024 10:12 UTC
  • Mauaji katika safu ya chakula

Karibuni kuwa nasi katika kipindi chetu cha leo cha Makala ya Wiki. Kipindi hiki kinatupia jicho mauaji yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wa Gaza waliokuwa katika safu za kupokea misaada ya kibinadamu huko Rafah.

Kila siku inayopita kwenye mashambulizi ya Wazayuni katika Ukanda wa Gaza, inafichua zaidi sura mpya ya maafa ya mauaji ya raia Wapalestina. Jioni ya Alhamisi, Februari 29, jeshi la Israel liliumiminia risasi umati mkubwa wa watu wa Gaza waliokusanyika karibu na msafara wa malori ya misaada ya kibinadamu yaliyokuwa yamebeba unga wakisubiri kupokea msaada. Katika hujuma hiyo ya mauaji ya kimbari, Wapalestina 112 waliuawa shahidi na wengine karibu 800 walijeruhiwa. 

Yahya El Masry, mmoja wa madaktari wa Kipalestina, anasema kwamba, aliona makumi ya watu wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi; Baadhi yao walipigwa risasi kichwani, shingoni na mapajani. Anaendelea kusimulia kwamba: "Mifuko ya unga wa ngano ilikuwa na damu ya raia waliojeruhiwa na waliouawa." Daktari huyo wa Kipalestina, ambaye alishuhudia mauaji hayo ya siku ya Alhamisi, alisema pia kwamba aliona miili kadhaa ya watu walioaga dunia kutokana na mkanyagano au kugongwa na malori ya misaada yaliyokuwa yakijaribu kuhepa mashambulizi ya Israel. Dakta El Masry anasema: Baadhi ya watu walijaribu kuwapakia majeruhi kwenye magari au mikokoteni, na wakati huo huo kubeba unga wa ngano kutoka kwenye malori kabla ya kwenda hospitali. 

Wapalestina wasalia bila ya chakula kufuatia mauaji ya kimbari ya Israel Gaza 

Utawala wa Kizayuni wa Israel umefunga njia zote za nchi kavu na baharini za kutuma misaada kwa watu wasio na makazi na waliokimbia nyumba zao wa Gaza. Israel inamimina risasi na mabomu juu ya vichwa vya watu wa Gaza kutokea pande zote, na inazuia au kubana operesheni za kudondosha misaada kutokea angani kwa Wapalestina wa Gaza. Kwa mfano tu, Jordan imejaribu mara kadhaa kutuma shehena za msaada wa chakula kwa watu wa Gaza kutokea angani, lakini Wazayuni hawaruhusu hata shehena hizo kuwafikia watu wenye njaa wa Gaza. Wakati huo huo Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza kuwa watu 700,000 wa kaskazini mwa eneo hilo wanasumbuliwa na njaa.

Sambamba na mashambulizi makubwa na kuzingirwa kwa eneo hili, Gaza inateseka kwa aina mbaya zaidi ya mgogoro, yaani, tatizo la njaa na maafa makubwa yanayotengenezwa kikamilifu na mwanadamu. Msaada kiduchu unaowasili Gaza haujaweza kuzuia ongezeko la njaa, na vyanzo vya habari na taasisi za kimataifa zinaelezea kuwa, janga hilo linaongezeka siku baada ya nyingine.

Michael Fakhri, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki ya Chakula, amesema kwamba: Utawala wa Kizayuni wa Israel unatumia njaa kama silaha katika vita vya Gaza. Fakhri anasema: "Tulichoona baada ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ni hatua za Israel za kuzidisha hali mbaya kwa watu wa Gaza na kuongeza: "Vita vya Gaza ni kati ya serikali dhalimu na watu wanaopigania uhuru."

Michael Fakhri

Sambamba na uharibifu mkubwa wa vituo na miundombinu, kunyima watu chakula na mahitaji mengine ya kimsingi ya maisha kama vile dawa, maji safi na malazi, utawala wa Kizayuni wa Israel umezidisha mbinyo dhidi ya watu wa Gaza na kuwasababishia ukosefu wa usalama katika nyanja mbalimbali za maisha yao, ikiwa ni pamoja na uhaba wa chakula kwao.

Ripota wa New York Times, Megan Stack, anaeleza maafa yanayoendelea sasa katika eneo la Gaza huko Palestina katika ripoti yake yenye kichwa cha maneno: "Hadithi ya kusikitisha zaidi kutoka Gaza: Watu wanaoaga dunia kwa kifo kigumu". Ripoti hiyo inazungumzia mauaji ya kimbari ya Wapalestina yanayofanywa na utawala ghasibu wa Israel na kuonesha kuwa, viongozi ayari na waongo wa Marekani wanajua kikamilifu yanayojiri katika Ukanda wa Gaza na wanashiriki katika jinai za Wazayuni za kuwaua Wapalestina.

Megan Stock anaandika katika ripoti yake ya gazeti la New York Times kwamba: "Inauma sana kuona baba kijana anasimama karibu na kifurushi kidogo kilichofunikwa kwa shuka kwenye kitanda cha hospitali. Anaonekana akifuta paji lake la soni kutokana na kukata tamaa kabisa." Megan Stock anaendelea kusimulia akisema: "Moussa Salem, mpiga picha kutoka Gaza ambaye alichukua video ya tukio hili la kutisha na kunitumia, anasema: shuka hiyo nyeupe ilikuwa sanda ya Mohammad Al-Zaigh, mtoto wa miezi 2 ambaye alifariki dunia katika Hospitali ya Kamal Adwan huko Gaza."

Katika video hiyo, mmoja wa wafanyakazi wa hospitali hiyo anasema: Mama yake Mohammad Al-Zaigh alimzaa wakati wa mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza. Anaendelea kusema: Kila mtu anajua kuwa afya ya mama huathiri afya ya mtoto. Hili limethibitishwa katika sayansi ya tiba na afya, na matatizo yote ya lishe ya mama yalihamishiwa kwenye mwili uliokondeana wa mtoto; aliugua na akafa kwa sababu ya kinga dhaifu ya mwili wake."

Image Caption

Ripota wa New York Times, Megan K. Stack ameandika pia kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: Hebu fikiria kuhusu Marekani kulazimika kudondosha chakula kutokea angani kwa sababu haina hata udhibiti wa kutosha juu ya vita vya Israel ambavyo tunavifadhili sisi wenyewe….  Anasema kuhusu mauaji ya majuzi huko Rafah kwamba: "Mauaji haya yalikuwa makubwa zaidi, mabaya zaidi, lakini si mapya. Kumekuwa na ripoti kwa wiki kadhaa za wanajeshi wa Israel kushambulia watu wanaojaribu kupata msaada wa chakula huko Gaza."

Televisheni ya Al Jazeera ya Qatar pia imeripoti kuwa, mtoto mwingine wa miezi 2 aitwaye "Mahmoud Fattuh" ameaga dunia kwa utapiamlo katika Hospitali ya al-Shafa katika Jiji la Gaza. Mmoja wa waokoaji waliompeleka mtoto huyo hospitalini anasema kwenye video kwamba: Mtoto huyo alikuwa hajanyonyeshwa maziwa kwa siku kadhaa. Dk. Hossam Abu Safieh, mkuu wa Wadi ya Watoto katika Hospitali ya Kamal Adwan, anasema kuhusiana na suala hili kwamba: Tumeshuhudia idadi kubwa ya vifo miongoni mwa watoto, hasa watoto wachanga, katika mwezi huu.  

Hapa inatupasa kuweka wazi kwamba, watoto wa Kipalestina wanaoishi Gaza hawafi kwa ukame au majanga mengine ya asili. La hasha. Njaa inayoua watoto hao ni janga linalotengenezwa na mwanadamu. Serikali ya Israel sio tu haipeleki chakula cha msaada kwenye eneo lililozingirwa la Gaza, lakini pia inazuia kutumwa misaada mingine ya kimataifa ya matibabu na chakula katika eneo hilo. Imeonekana mara nyingi kwamba, malori yanayobeba chakula yanapoingia Gaza, Israel inazuia zoezi la kugawa misaada ya kibinadamu kwa kushambulia watu wanaokabiliwa na njaa wanaotafuta walau kipande cha mkate.

Watu wa Gaza wanaendelea kusumbuliwa na njaa kwa sababu serikali ya Marekani, ikiwa ni mshirika mkubwa na muungaji mkono mkuu wa utawala bandia wa Israel, haitaki kutumia uwezo wake kuilazimisha Tel Aviv kupeleka chakula kwa watu wa Gaza. Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP) zimesema katika ripoti ya takwimu ya hali ya kutisha katika Ukanda wa Gaza kwamba: "Utapiamlo huu mkubwa na wa pande zote haujawahi kutokea duniani."

Michael Ryan, Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Dharura ya Afya wa Shirika la Afya Duniani (WHO), amasema kwa uwazi kwamba: "Watu wa Gaza wanakufa kwa njaa. Hatupaswi kujifanya kuwa vifo hivi haviepukiki. Tunajua kwamba wakazi wa Gaza wanakunywa maji machafu, wanakula nyasi na chakula cha wanyama".

Marekani na baadhi ya nchi za Maghribi kama Ufaransa, zimechukua hatua ya kimaonyesho na kinafiki na kudondosha misaada kiduchu ya chakula huko Gaza kwa njia ya anga. Serikali ya Marekani inajaribu kujidhihirisha kama inajali ubinadamu ilhahi tayari imetumia kura ya veto mara kadhaa katika Baraza la Usalama la UN kuzuia maamuzi yote ya kimataifa yanayolaani mauaji ya Israel huko Gaza au yanayotaka kusimamishwa vita katika eneo hilo la Palestina. Hapo awali pia, utawala wa Joe Biden uliamua kukata msaada wa kifedha kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudimia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, kama sehemu ya uungaji mkono wake kwa utawala katili wa Israel. ****

 

Tags