Sep 15, 2018 12:03 UTC
  • Imam Hussein AS; mhimili wa umoja

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya siku hizi za Muharram na tukio la kuuawa shahidi Imam Hussein AS pamoja na masahaba zake katika jangwa la Karbala mwaka 61 Hijria.

Kipindi chetu cha leo kimebeba anuani isemayo "Imam Hussein, mhimili wa umoja". Ni matumaini yanguu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Kwa hakika Imam Hussein AS alitundika juu mwenge wa uongofu katika zama zake ambapo giza na upotovu vilikuwa vimewafanya watu na watawala kuwa mateka wake.

Miguu ilikuwa imesimama na kuacha kutembea kuelekea katika njia nyoofu ya haki huku hali ya mghafala ikiwa imetanda kila mahala kwa maana halisi ya neno. Machweo ya haki yalikuwa yakionekana nyuma ya milima mirefu ya dhulma na watu walikuwa wakifanya harakati kwa kuegemea kitu ambacho hakikuwa na uhakika katika anga iliyojaa vumbi la nifaki na ufisadi. Hali iliyokuwa ikitawala katika zama hizo ilikuwa ya kusikitisha, kwani dini, maisha, uongozi na masuala yote yalikuwa na maana ambayo ni kinyume na uhakika wake. Mikono michafu ya utawala, ilikuwa ikifanya njama za kuonyesha mambo yote ambayo kidhahiri yalikuwa machafu na ya hadaa kwamba, ni mazuri na yanayofaa. Kana kwamba, wahusika wote walikuwa wamekubaliana kuwa, wavae vazi la uongo na hila. Katika zama ambazo kiongozi jahili kabisa yaani Yazid bin Muayiwa alishika hatamu za uongozi na kugeuza uongo kuwa ukweli, Imam Hussein AS aliona ni wajibu kwake kusimama na kwenda kumtimizia hoja kiongozi huyo dhalimu. Imam Hussein AS aliamua kusimama ili kupambana na dhulma na uovu uliokuwa ukifanywa na watawala wa zama hizo, ili avunje kuta za mghafala na udhalili na aziamshe na kuzizindua nyoyo zilizokuwa zimekufa na kupata kutu ya mghafala ili zirejee kwa Mola wake.

Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS ambaye ni mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, alisimama kidete kukabiliana na uongo na hila na kufanikiwa kutoa kigezo kikubwa cha kujitolea na kuuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu na wakati huo huo kuacha hamasa kubwa katika nyoyo za wapenda haki na wachukia dhulma kote ulimwenguni.

Kumwagwa damu ya Imam Hussein AS kulileta uhai katika miili iliyoganda na akaleta umoja kwa ajili ya kuhuisha haki na kuangamiza dhulma. Kwa muktadha huo, Imam Hussein akawa mwanzo wa kisa kirefu ambacho hadi leo kimezishughulisha nyoyo na kimekuwa kikiwalingania watu wote ukweli na haki.

Endapo tutasema kuwa, Imam Hussein AS ni wa Waislamu tu, tutakuwa tumekosea. Kile ambacho tunakishuhudia katika Arubaini ya Imam Hussein AS ambapo watu kutoka Afrika, Ulaya, Asia na kwingineko Waislamu wa madhehebu mbalimbali na hata wasiokuwa Waislamu ni ishara ya wazi kwamba, Imam Hussein AS sio wa Waislamu tu bali ni wa dini na kaumu zote. Kibanda na Husseiniya ya Wakristo inayojuliakana kwa jina la "Issa bin Maryam" ambayo hutoa huduma kwa wafanyaziara katika njia ya kuelekea Karbala ni mfano mwingine wa wazi kuhusiana na jambo hilo. Mfano mwingine ni wafanyakazi wa Shirika la Trim ambao ni mabudha wa China.

Mabudha hawa wanaofanya kazi katika shirika hilo la Trim nchini Iraq, husimamisha kazi zao kwa siku kadhaa na kuweka vibanda maalumu vya kutoa huduma bure kama maji ya kunywa, chai, matunda na kadhalika kwa mazuwaar wanaotembea kwa miguu kuelekea Karbala. Aidha huandaa huduma za kuchaji simu wafanyaziara hao ili waweze kufanya mawasiliano.

Mkurugenzi wa Shirika la Trim anasema: Imam Hussein AS alikuwa shakhsia mkubwa mno. Sisi tunamfahamu Hussein ni nani na tunaelewa pia nini kilimpata. Kwa hakika sisi tunajiona ni familia moja na hawa mazuwwar na tunaonyesha kwamba, tuko pamoja nao."

 

Kwa hakika hii ni mifano midogo na michache tu ya maashiki na wapenzi wa Imam Hussein kutoka pembe mbalimbali duniani ambao hata sio Waislamu. Hili ni fukuto la mapenzi kwa Imam Hussein AS katika ulimwengu huu tata na kila mtu anayehisi joto na fukuto la mapenzi haya huvutwa.

Diana Tranko ambaye amezaliwa na kukulia katika familia ya Kikristo katika jimbo la Texas nchini Marekani alisilimu hivi karibuni. Diana ambaye alivutiwa mno na shakhsia ya Imam Hussein AS anasema: Harakati na irada ya Imam Hussein ilikuwa ni kwa ajili ya kuhuisha haki na ukweli. Alijitolea kila kitu ili dini na utu wa mwanadamu vibakie. Katika hili kuna engo ya kifrikra na kiakili ya ajabu. Sababu kuu iliyonifanya nisilimu na kuwa Mwislamu ilikuwa hii. Kwa maoni yangu, Imam Hussein ni shakhsia wa kimataifa."

Kwa hakika mjadala kuhusu Karbala na tukio la Ashura si jambo la Waislamu wa madhehebu ya Shia tu. Huba na mapenzi kwa Imam Hussein AS ni mhimili wa umoja wa Waislamu.  Imam Hussein na kuuawa kwake shahidi kwa dhulma kulizuia upotofu mkubwa mno uliokuwa ukifanywa katika sira ya Bwana Mtume SAW na dini ya Mwenyezi Mungu. Imam Hussein AS alifuta kwa damu yake vumbi lililokuwa limeingia katika itikadi za Uislamu.

Marhumu Ayatullah Sayyid Ridha Sadr anaandika katika kitabu cha "Kiongozi wa Mashahidi" kwamba: Kuuawa shahidi Imam Hussein AS, kulidhamini umoja wa Uislamu.

Kama harakati ya Imam Hussein AS mwaka 61 Hijria na karne nyingi baada yake ilipelekea kutokea umoja baina ya waislamu, kwa nini hii leo harakati hii na nguvu hii haitumiwi katika njia ya kuleta umoja miongoni mwa Waislamu? Bila shaka ni mahapa pake hapa kutaja jina la Imam Mussa Sadr, aliyekuwa kiongozi wa Mashia nchini Lebanon. Imam Mussa Sadr, alikuwa akiwaalika katika majlisi za Muharram maulama na wanafikra wa Kisuni na hata Wakristo na kubainisha kuhusiana na shakhsia ya Imam Hussein AS pamoja na malengo yake yaliyopeleke a hadi Karbala Iraq. Mbinu hii ya Imam Mussa Sadr ilionyesha juu ya fikra yake kwamba, Imam Hussein ni zaidi ya madhehebu na kundi fulani la Waislamu.

Aidha Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria nae alikuwa akifanya hivyo pia na kufanikiwa kuwafahamisha watu wengi kuhusiana na Imam Hussein AS katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Hii leo kama wafuasi wa dini za mbinguni na dini ya tawhidi, watamfanya Imam Hussein AS kuwa kigezo na ruwaza yao njema kwa ajili ya kuhuisha utu, ubinadamu na maadili mema na hivyo kuungana katika hilo, bila shaka watafanikiwa kufikia malengo yao aali.

اَلسَّلامُ عَلَیْکَ یا اَبا عَبْدِاللّهِ وَ عَلَى الاْرْواحِ الَّتى حَلَّتْ بِفِنآئِکَ عَلَیْکَ مِنّى سَلامُ اللّهِ اَبَداً ما بَقیتُ وَ بَقِىَ اللَّیْلُ وَ النَّهارُ وَلا جَعَلَهُ اللّهُ اخِرَالْعَهْدِ مِنّى لِزِیارَتِکُمْ اَلسَّلامُ عَلَى الْحُسَیْنِ وَ عَلى عَلِىِّ بْنِ الْحُسَیْنِ وَ عَلى اَوْلادِ الْحُسَیْنِ وَ عَلى اَصْحابِ الْحُسَیْنِ

Wassalamu Aayakum Warahmatullahi Wabarakaatuh….

 

 

Tags