Oct 20, 2022 08:48 UTC
  • BBC, karne moja ya huduma na uaminifu kwa serikali ya Uingereza

"Tom Mills, mwanasosholojia na mwandishi wa Kiingereza, anasema katika kitabu "The BBC: Myth of a Public Service" kwamba BBC daima imekuwa ikisema hewallah na imekuwa hadimu mtiifu kwa wale walio madarakani..."

Hii leo, tukiwa katika zama za mawasiliano, nguvu ya vyombo vya habari inaonekana  na kuhisika zaidi kuliko wakati wowote mwingine. Pamoja na hayo karne moja iliyopita, wakati Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) lilipoanza kufanya kazi na kupeperushi matangazo yake kupitia kituo kimoja cha redio mnamo Oktoba 18, 1922, ni watu wachache sana waliotabiri mabadiliko makubwa kama haya yanayoshuhudiwa sasa katika sekta ya vyombo vya habari. Umuhimu wa vyombo vya mawasiliano ya umma ulidhihiri zaidi kadiri muda ulivyopita na kutokana na maendeleo ya teknolojia ya vyombo vya habari na mbinu za kuzalisha na kutuma ujumbe, na katika uwanja huo BBC ilifanya jitihada za kutobaki nyuma ya washindani wake. Kwa sababu hiyo, miaka kumi baadaye, Shirika la Utangaza la Uingereza, BBC, lilianzisha kitengo cha matangazo ya ng'ambo ambacho kazi yake kuu ilikuwa kupeleka mbele malengo ya sera ya kigeni ya serikali ya Uingereza, ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa imepoteza nguvu zake za kikoloni wakati huo. Nafasi na majukumu ya BBC yalipanuliwa na kuimarishwa zaidi ndani na nje ya Uingereza baada ya kuzuka kwa Vita vya Pili vya Dunia. Redio zilizokuwa zikirusha matangazo chini ya shirika hilo la utangazaji kwa kutumia lugha kadhaa, zilikuwa na jukumu la kuelekeza maoni ya umma kwa maslahi wa nchi Waitifaki, hasa Uingereza, na kuandika habari za maendeleo na kusonga mbele kwao. Nafasi yenye ushawishi ya chombo hicho cha habari katika Vita vya Pili vya Dunia kama mkono wa kuume wa serikali ya London, iliifanya Uingereza iipe kipaumbele maalumu BBC kwa kupanua zaidi shughuli zake baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Kwa utaratibu huo, idadi ya redio, muda wa utangazaji na aina mbalimbali za vipindi vya redio vya BBC viliongezwa. Pia, vituo vya televisheni vya BBC vilianzishwa hatua kwa hatua na kuanza kutangaza na kurusha matangazo na vipindi mbalimbali. BBC ilianza mapema sana kutumia mtandao wa intaneti kwa ajili ya kupigia debe na kueneza zaidi matangazo yake. Kwa njia hiyo, Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC kwa sasa linasambaza na kuwatwisha watu maoni yake katika pembe mbalimbali za dunia kwa kutumia zana tatu za vyombo vya habari, yaani redio, televisheni na mtandao wa intaneti.

Inasemekana kuwa, BBC ndio kituo kikubwa zaidi cha habari duniani katika nyanja mbalimbali, na inarusha matangazo na vipindi vyake katika lugha zaidi ya 40. Shirika hilo lina waandishi wa habari zaidi ya 200 na wafanyikazi rasmi na wasio rasmi elfu 35. Vifaa na zana za kisasa ambazo zinazotumiwa na BBC nchini Uingereza na sehemu mbalimbali za dunia vimeongeza uwezo wa taasisi hiyo ya kupasha habari katika kuongoza na kuelekeza fikra na maoni ya umma. Hata hivyo inatupasa kuelewa kwamba, rasilimali muhimu zaidi ya chombo chochote cha habari ni imani ya watu kwa chombo hicho. Ni kwa sababu hiyo, ndiyo maana BBC daima imekuwa ikisisitiza kwamba haipendelei wala kuegamia upande wowote na kwamba inatangaza ukweli mtupu, na inafanya jitihada za kuwakinaisha wasikiliza na watazamaji wake katika uwanja huo. Hata hivyo imekabiliana na vizingiti viwili muhimu katika kuthibitisha madai hayo na kwamba ni chombo huru na kisichopendelea upande wowote. Mosi ni kwamba, BBC inategemea bajeti ya serikali ya Uingereza, na pili ni kwamba matangazo ya chombo hicho yanapaswa kulingana na mikakati na stratijia iliyotangazwa na serikali ya London. Mambo haya mawili yanabatilisha na kutia doa madai ya BBC ya kutopendelea upande wowote katika matangazo yake, na kwa sababu hiyo, imekuwa ikijaribu kujitetea au kukanusha shutuma za kufanya kazi kwa upendeleo. Lakini inavyoonekana ni kuwa, kulingana na uhalisia wa mambo, ni muhali kuweza kukanusha utegemezi wa BBC kwa serikali ya Uingereza katika masuala ya kiutawala na kifedha. Aidha, katika ripoti ya British House of Lords kipindi cha ubunge cha 2005-2006, ilielezwa kuwa: “Makubaliano ya vyombo vya habari kati ya BBC na Wizara ya Mambo ya Nje yanaamua malengo ya kimkakati ya BBC World Service. Makubaliano hayo yanaiwajibisha BBC World Service kwamba vipindi na matangazo yake na vipaumbele vyake vya kihabari vitayarishwe kulingana na mkataba wake na Wizara ya Mambo ya Nje." 

"Tom Mills, mwanasosholojia na mwandishi wa Kiingereza wa kitabu "The BBC: Myth of a Public Service" anatoa vielelezo na ushahdi wa kuthibitisha kwamba BBC si chombo huru wala kisichopendele upande wowote cha habari. Anasema katika kitabu hicho kwamba: "BBC daima imekuwa ikisema hewallah na imekuwa hadimu mtiifu kwa wale walio madarakani..." Zaidi ni kwamba, shirika hilo la utangazaji limeonyesha kwa vitendo kwamba maslahi ya serikali ya Uingereza ni mstari wake mwekundu usioonekana kwa macho. Hivyo tunaweza kusema kuwa, misimamo ya BBC kuhusu matukio mbalimbali ni kielelezo cha sera za serikali ya Uingereza. BBC pia inafanya harakati katika masuala ya kitamaduni na kijamii na inajaribu kuuweka mtindo wa maisha wa Kimagharibi katika nafasi ya utamaduni wa kitaifa na asili wa watu wa nchi mbalimbali. Kwa hiyo, watu wanaoacha mila, desturi na imani zao na kufuata utamaduni wa kigeni wa Magharibi, wataendana vyema na mielekeo ya BBC. Matunda ya kitamaduni yanayozalishwa na chombo hicho cha habari yanaonekana miongoni mwa baadhi ya wafanyakazi wake kwa kadiri kwamba, kila mara, kumekuwa kukifichuliwa habari na kashfa za ufisadi wao wa kimaadili na mahusiano haramu ya ngono. Miongoni mwa mifano muhimu ya ukweli huo ni kesi "Jimmy Savile" aliyekuwa mtangazaji maarufu wa BBC, ambaye ripoti ya kushangaza iliyotolewa mwaka mmoja baada ya kifo chake mnamo 2011, ilifichua kuwa alikuwa amewanyanyasa kingono watu 600 katika kipindi cha miaka 50. Jimmy Savile alikuwa mtangazaji mkubwa na mashuhuri wa BBC na mwendeshaji wa vipindi maarufu kama Top of the Pops and Jim'll Fix It.

Jimmy Savile aliyekuwa watangazaji maarufu wa BBC

Viongozi wa serikali ya Uingereza walikuwa wakipora rasilimali za Iran kwa muda mrefu kwa kutumia ushawishi wao na kuingilia masuala ya ndani ya Iran. Shirika la BBC pia linatilia maanani sana Iran, na lilizindua redio yake ya lugha ya Kiajemi (Kifarsi) mwanzoni mwa Vita vya Pili Dunia, mnamo Desemba 29, 1940. Wakati huo, lengo la BBC lilikuwa kukwamisha mpinzani wake yaani Ujerumani, kushawishi maoni ya umma ndani ya Iran na kuhalalisha uvamizi wa Uingereza dhidi ya nchi yao. Sera za propaganda dhidi ya Iran za redio hiyo inayokaribia kufungwa, zingali zinaendelea hadi sasa.

Wakati wa harakati za kutaifisha sekta ya mafuta iliyokuwa ikidhibitiwa na madola ya kigeni nchini Iran, BBC ilichukua msimamo wa kuipinga harakati hiyo, kiasi kwamba kabla ya mapinduzi na kuondolewa madarakani serikali ya Dk. Mossadeq, ilitangaza uunga mkono Marekani na Uingereza kwa mapinduzi hayo.

Wakati wa kilele cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, BBC ilijaribu kujionyesha kuwa haina upande wowote, lakini wakati huo huo ilikuwa ikitangaza habari mbaya na za kukatisha tamaa kuhusu mapinduzi hayo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi wa Iran, chombo hicho daima kimekuwa kikipuuza maendeleo ya Iran ya Kiislamu, na kinyume chake, kinakuza nukta dhaifu na kuwakatisha tamaa wananchi kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mnamo Januari 14, 2009, yaani karibu miezi mitano kabla ya uchaguzi wa 10 wa Rais wa Irani, ilianzishwa televisheni ya BBC ya lugha ya Kifarsi ili kuathiri zaidi jamii ya Irani. Baada ya uchaguzi huo na kutokana na madai ya udanganyifu yaliyotolewa na mmoja wa wagombea, kulijitokeza machafuko ambayo yaliendelea kwa muda, na televisheni mpya ya BBC ilichukua jukumu muhimu katika kuzidisha na kuendeleza machafuko hayo, bila kujali madai yake ya siku zote eti ya kutoegemea upande wowote. Televisheni hiyo ya lugha ya Kifarsi ya BBC iliachana na madai hayo waziwazi katika machafuko mengine nchini Iran na kuunga mkono ghasia dhidi ya serikali, ikiwa ni pamoja na uungaji mkono wake kwa wafanyaghasia wanaotangaza waziwazi kuwa lengo lao ni kuipindua Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika hali kama hizi, BBC hueleza mtazamo na misimamo yake kupitia maneno ya eti wataalamu wake au vyanzo visivyojulikana. Kwa upande mwingine, chombo hicho cha habari cha Uingereza, kama vilivyo vyombo vya habari vya nchi nyingine za kibeberu, kinajaribu kueneza utamaduni mbovu wa Kimagharibi kwa kutumia anwani na majina ya kuvutia na eti mitindo ya kisasa, na kwa njia hiyo kuharibu na kupotosha maadili ya kidini, kitaifa na utambulisho wa watu katika mataifa mengine kama Irani katika kalibu ya vipindi, tamthilia, filamu na matangazo ya aina mbalimbali.

Kwa ujumla ni kwamba, japokuwa Shirika la Utangazaji la BBC, katika kipindi cha karne moja ya shughuli zake, limepewa himaya kubwa ya kifedha na kiufundi na kuweza kufikisha matangazo yake ya kipropaganda katika maeneo mengi ya dunia, lakini ushahidi, nyaraka na utendaji wake vinathibitisha kuwa taasisi hiyo haitoi habari na taarifa za kuaminika kwa wasikilizaji wake na haizingatii kanuni za kutoegemea upande wowote na uaminifu, kwa sababu kabla ya jambo lolote jingine BBC huzingatia na kuweka mbele maslahi ya serikali ya kikoloni ya Uingereza.

Tags