Dunia yakumbuka siku ya ubaguzi wa rangi
Wapenzi wasikilizaji wiki hii tarehe 21 Machi ilikuwa ni siku ya kutokomeza ubaguzi wa rangi duniani. Siku hii hukumbukwa kwa mnasaba wa mauaji ya waandamanaji wazalendo Waafrikadhidi ya ubaguzi wa rangi, mjini Sharpeville, Afrika Kusini, tarehe 21, Machi, mwaka 1960. Katika tukio hilo, waandamanaji wapatao 60 walipigwa risasi na kuuawa na polisi wa utawala wa makabaru waliokuwa wakitawala nchi hiyo. Karibuni......@
Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi ni fursa ya kusistiza kuhusu ahadi za kuundwa dunia yenye uadilifu na usawa na isiyo na chuki na taasubi. Mwanadamu anapaswa kupata somo na ibra kutoka katika historia na uharibifu uliotokana na ubaguzi wa rangi ili kwa njia hiyo ajifunze kuhusu kutokomeza ubaguzi na kujifunza kuishi na wanaadamu wa rangi mbali mbali kwa heshima. Hii ni kwa sababu amani ya kudumu haitawezekana isipokuwa kwa kuzingatia msingi wa usawa na haki za watu wote pasina kubagua kwa msingi wa rangi ya ngozi, kaumu au kabila, jinsia, dini, hadhi ya kijamii n.k
Wiki hii siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi imekumbukwa kukiwa na chagamoto na mafanikio kuhusu Taarifa ya Durban.
Ni miaka 15 sasa, baada ya taarifa ya kihistoria kupitishwa katika Kongamano la Kimataifa Dhidi ya Ubaguzi wa Rangi kupitishwa huko Durban, Afrika Kusini mwaka 2001. Kongamano hilo lilijadili vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni yaani Xenophobia n.k.
Baada ya kusambaratika Shirikisho la Sovieti na kumalizika vita baridi baina ya madola mawili makubwa duniani yaani Shirikisho la Sovieti na Marekani, kuliimarika harakati za kutetea haki za binadamu na kupinga ubaguzi wa rangi. Kulifanyika vikao kama vile Kikao cha Vienna cha Haki za Binadamu mwaka 1993 na Kikao cha Copenhagen cha Haki za Kijamii. Pamoja na hayo tulishuhudia kuongezeka ubaguzi wa rangi na chuki kote duniani na ni kwa msingi huo ndio Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likaamua kuitisha mkutano kujadili tatizo hilo. Mnamo 12 Desemba mwaka 1997, Baraza Kuu la Umoja wa Mataia lilipitisha azimio nambari 52/111 kuhusu kuandaliwa mkutano wa kimataifa dhidi ya ubaguzi wa rangi, na chuki dhidi ya wageni. Mkutano huo ulipangwa kufanyika Durban Afrika Kusini mwaka 2001. Mkutano huo ulihudhuriwa na nchi 163 na takribani mashirika yasiyo ya kiserikali, NGO 3500. Ajenda kuu ya kikao hicho ilikuwa ni kujadili na kuchunguza sababu za ubaguzi wa rangi mamboleo na chuki dhidi ya raia wa kigeni, kuwatambua waathirika, kuchukua hatua za kuzuia kuibuka tatizo hili na kutoa msaada wa kukabiliana na ubaguzi na chuki sambamba na kuwepo na hatua za kuwalipa fidia waathirika wa maovu hayo.
Ubaguzi wa rangi ni kitendo cha kuthamini au kutenga binadamu kwa misingi ya rangi za ngozi. Ubaguzi wa rangi ulikuwa maarufu sana katika nchi kama Afrika Kusini kwa jina la "apartheid" na Marekani kwa jina la "segregation" ambapo huko Waafrika walikandamizwa kutokana na rangi yao katika kupata huduma mbalimbali za kijamii na kimaendeleo. Wakati wa ukoloni, rangi ilitumika kama msingi wa utoaji huduma muhimu mfano: shule, matibabu na haki nyingine za kibinadamu. Rangi nyeusi ilipewa hadhi ya chini zaidi. Iwapo mtu au watu, kundi au serikali itakuwa na dhana kuwa kundi maalumu la watu ni bora kuliko wengine kwa ajili ya kuwa na rangi au kuwa katika kaumu maalumu, basi huo huwa ni ubaguzi wa rangi. Ingawa ubaguzi na ukosefu wa uadilifu ni mambo ambayo yana historia ndefu katika historia ya jamii ya mwanadamu, lakini ubaguzi wa rangi na kudau kaumu moja kuwa bora zaidi ya nyingine ni mambo ambayo yalitiliwa mkazo zaodo wakati wa ukoloni wa madola ya magharibi. Ubepari wa zama za Renaissance barani Ulaya na kujirundikia utajiri tabaka moja katika jamii ambalo pia lilipata suhula zote bora ndio uliokuwa mwanzao wa ubaguzi wa rangi katika karne za hivi karibuni.
@@@@
Tokea wakati wakoloni wa Ulaya walipoingia barani Afrika, hatima ya watu wa bara hilo ilikuwa sawa na ya wakaazi asili wa bara Amerika au maeneo mengine yaliyokoloniwa duniani. Maeno hayo yaliyokoloniwa yalishuhudia utumwa na dhulma kubwa iliyotendwa na wakoloni. Katika bara Afrika, wakoloni Wazungu kutoka Ulaya, kwa himaya ya serikali zao, waliwapokonya wazalendo Waafrika haki zao na kuwatumia kama watumwa wao katika migodi na kazi nyingine ngumu. Ingawa kwa mapambano, nchi za Afrika zimepata uhuru ikiwemo Afrika Kusini nchi ambayo ilipata masaibu makubwa zaidi kabla ya kuangushwa utawala wa ubaguzi wa rangi au Apertheid, lakini leo tungali tunashuhudia ukoloni mambo leo barani Afrika. Utajiri mkubwa wa Afrika hasa madini yangali yanaporwana madola ya kibeberu.
Katika zama za ukoloni, Marekani ilikuwa ikishirikiana na waitifake wake wa Ulaya kukandamizwa mwamko wa Waafrika wazalendo na hata kuingilia kijeshikatika baadhi yanchi.
Frantz Omar Fanon katika kitabu chake kuhusu ubaguzi wa rangi anasema: 'Ukoloni wa nchi za Magharibi ulitegemea mafanikio ya nchi hizo kiteknolojia kukoloni maeneo mengine. Wamagharibi waliamini kuwa, kutokana na mafanikio yao basi walikuwa ni kaumu bora zaidi ya wengine. Huu ndio uliokuwa mwanzo wa ukoloni na ubaguzi wa rangi wa nchi za Magharibi."
Taasubi ya kirangi ni itikadi ya kusikitisha ambayo imemsababishia mwanadamu matatizo mengi.
Leo katika karne ya 21, pamojana ustawi mkubwa wa kielimu na kiteknolojia,mwanadamu angali anakumbwa na matatizo ya ubaguziz wa rangi.
Mwaka 2015, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alitoa wito kwa nchi zote duniani kupambana na ubaguzi wa rangi na zipate ibara na funzo kutoka katika historia. Katika ujumbe wake mwaka wa 2016 kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alibainisha wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la ubaguzi na ghasia inayohusiana na chuki za kibaguzi duniani kote. Aliongeza kuwa mzozo na mivutano dhidi ya vikundi vya watu walio wachache imeongezeka, akimulika hasa ghasia, chuki na mashambulizi dhidi ya wahamiaji, wakimbizi na Waislamu duniani.
Leo pia tunashuhudia ubaguzi mkubwa wanaotendewa Wapalestina mikononi mwa utawala wa kibaguzi wa Israel. Utawala haramu wa Israel una malengo ya kishetani ya kuteka kikamilifu ardhizote za Wapalestina.
Halikadhalikam ingawa Marekani inadai kuwa ni mtetezi wa demokrasia duniani lakini ukwelini kwamba jamii ya Marekani ni dhihirisho kamili ya ubaguzi wa rangi na kaumi. John Robertson, mtaalamu wa kijamii wa Marekani, anafafanua hali ya Wamarekani weusi au wenye asili ya Afrikana kusema: 'Ubaguzi Marekani una muundo rasmi katika majimbo yote. Aghalabu ya Wamarekani weusi wanaishi katika mitaa yao maalumu. Ni vigumu kuona Wamarekani weusi wakiwa wanapanda vyeo vya juu kisiasa au jeshini. Zaidi ya yote hayo kuna ubaguzi mkubwa wa kiuchumi. Hali ya kiuchumi ya Wamarekani Waafrika ni mbaya zaidi ya Wazungu"
Katika upande mwingine Waislamu nchini Marekani nao hivi sasa wanakabiliwa na ubaguzi mkubwa sana hasa baada ya matukio ya Septemba 11 mwaka 2011. Waislamu nchini Marekani wanasema kuongezeka hujuma na mashambulizi dhidi ya Waislamu nchini humo kumejiri kufuatia matamshi ya wanasiasa hasa Donald Trump, anayewania kuteuliwa na chama cha Republican kugombea urais nchini Marekani ambaye amekuwa akitoa matamshi makali dhidi ya Waislamu. Kwa ujumla kumeshuhudiwa kuongezeka chuki dhidi ya Waislamu kote duniani kutokana na sera za nchi za Magharibi za kuuchafulia jina Uislamu na Waislamu.
@@@
Dini Tukufu ya Kiislamu inatoa muongo mzuri sana kuhusu suala la wanadamu kuwa ni wenye kutoka kabila, kaumu au rangi mbali mbali. Uislamu unatazama suala hilo kama mazingira ya maumbile ambayo yako aina mbali mbali. Qur'ani Tukufu imezungumzia kuhusu mwanadamu kuwa na lugha na rangi mbali mbali na kusema hiyo ni dalili ya adhama ya Mwenyezi Mungu katika uwezo wake wa kuumba. Katika Surat Al H'ujuraat, aya ya 13 ya Qur'ani Tukufu tunasoma hivi: "Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari."