Afrika Kusini yaandaa mkutano wa kimataifa dhidi ya ubaguzi wa rangi wa Israel
Mkutano wa Kimataifa dhidi ya Ubaguzi wa Rangi wa Israel huko Palestina ulitazamiwa kuanza leo Ijumaa katika Jiji la Johannesburg nchini Afrika Kusini na utaendelea na kazi zake hadi tarehe 12 Mei mwaka huu.
Huu ni mkutano wa kwanza wa kimataifa unaotaka kuanzishwa vuguvugu la kimataifa la kusambaratisha mfumo wa ukoloni na ubaguzi wa rangi wa Israel, na unahudhuriwa na zaidi ya viongozi 200 wa kidini, kisiasa na wa wakuu wa makundi na vyama kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Mkutano huo unafanyika huku Israel ikiendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Palestina wa Ukanda wa Gaza tangu tarehe saba Oktoba mwaka jana, ambayo hadi sasa yameua raia karibu 35,000 wa Kipalestina, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake, pamoja na kujeruhiwa takriban wengine 79,000.
Mkutano huo ulipangwa kufunguliwa kwa hotuba ya Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Naledi Pandor, ambaye katika taarifa za awali alilaani hujuma ya Israel dhidi ya Gaza, na kutishia kuwatia mbaroni raia wa nchi yake wanaohudumu katika jeshi la utawala huo ghasibu iwapo watarejea nchini humo.
Katika muktadha huu, rais wa mkutano huo, Frank Chikane amesema - katika ujumbe wake kwenye tovuti ya mkutano kwamba: "Watu wa Palestina wanakabiliwa na mashambulizi ya mauaji ya kimbari ya utawala wa kibaguzi wa Israel kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea."
Amendika kuwa: Mkutano wa kimataifa wa kupinga ubaguzi wa rangi unakusudiwa kuangalia kwa kina janga la Palestina na kwa pamoja kuandaa mikakati ya kukomesha mauaji ya halaiki huko Gaza, kusitisha uvamizi wa miongo kadhaa wa ardhi ya Palestina na kuwaacha Wapalestina watumie haki yao ya kujitawala.
Chikane alisema - katika mahojiano ya awali na televisheni ya Al Jazeera ya Qatar - kwamba "ninachokiona Palestina ni kibaya zaidi kuliko sera ya ubaguzi wa rangi iliyokuwa ikitawala Afrika Kusini. Utawala wa Israel unafanya mambo mabaya zaidi dhidi ya Wapalestina kuliko yaliyoshuhudiwa katika kipindi cha utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini."
Taarifa iliyotolewa na kamati ya uongozi ya mkutano huo imesema, mkutano huu unalenga kuhamasisha harakati ya kimataifa ya kupinga ubaguzi wa rangi ili kuiwajibisha Israel kwa uhalifu wa ubaguzi wa rangi inaoufanya dhidi ya Wapalestina, na kufanya kazi ya kuutokomeza utawala wa kibaguzi wa Israel kutoka Mto Jordan hadi Bahari ya Mediterania.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, Afrika Kusini ambayo ilipitia kipindi kigumu cha mateso na manyanyaso ya utawala wa makaburu weupe, imekuwa mstari wa mbele kuwatetea Wapalestina wanaouawa kikatili wa Ukanda wa Gaza.