Chama cha DA cha Afrika Kusini chajiondoa kwenye mazungumzo ya kitaifa
Chama cha Democratic Alliance cha nchini Afrika Kusini kimejiondoa kwenye mazungumzo ya kitaifa hata hivyo hakijajitoa katika serikali ya mseto baada ya Rais wanchi hiyo Cyril Ramaphosa kumfuta kazi Naibu Waziri wake mmoja. Haya yameelezwa na kiongozi wa chama hicho John Steenhuisen.
Mazungumzo hayo ya kitaifa ni mchakato ulioanzishwa na Rais Ramaphosa ili kuiunganisha nchi hiyo baada ya uchaguzi wa mwaka jana, ambapo chama chake cha African National Congress (ANC) kilipoteza wingi wa wabunge wake kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miongo mitatu, hivyo kulazimika kuungana na chama cha DA kuunda serikali.
Vyama hivyo viwili vimekuwa vikitofautiana pakubwa kimawazo na kuhitilafiana mwaka jana kufuatia chama cha DA kukituhumu chama cha ANC kwa kuendesha mambo kinyume na maslahi yake na bila mashauriano hitajika.
Kiongozi wa Democratic Allliacne Steenhuisen amesema kuwa chama hicho "kiko katika mchakato wa kupoteza imani katika uwezo wake wa kuwa kiongozi si wa ANC, bali wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hitilafu zimeibuka kati ya vyama hivi viwili vya Afrika Kusini baada ya Rais Cyril Ramaphosa wiki hii kumfuta kazi Andrew Whitfield Naibu Waziri wa Biashara kwa kufanya ziara nchini Marekani bila ridhaa ya mamlaka husika.