Russia yatahadharisha kuhusu uingiliaji kijeshi huko Niger
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetahadharisha kuhusu hatua yoyote ya kuingia kijeshi nchini Niger.
Oleg Ozerov Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia katika Masuala ya Afrika ambaye pia ni mkuu wa Sekretarieti ya Jukwaa la Ubia kati ya Russia na Afrika ametahadharisha kuwa, uingiliaji wowote wa kijeshi wa nchi ajinabi katika masuala ya ndani ya Niger utakuwa na taathira hasi.
Jumuiya ya ECOWAS Jumatano iliyopita ilitangaza kuwa ipo tayari kuingilia kijeshi huko Niger; hata hivyo imesisitiza kuwa uingiliaji kijeshi ni chaguo la mwisho kwa ajili ya kile ilichokitaja kuwa "kurejesha demokrasia nchini humo".
Kikosi cha askari wa Gadi ya Rais wa Niger Jumatano Julai 26 kilimfunga ndani ya ikulu kiongozi wa nchi hiyo Muhammad Bazoum na kisha kumuondoa madarakani. Siku mbili baadaye, yaani Ijumaa ya tarehe 28 Julai, wanajeshi waliofanya mapinduzi wa Niger walimtangaza Jenerali Abdulrahman Tichiani kuwa Mkuu wa Baraza la Mpito la nchi hiyo.
Niger ina ukubwa wa kilomita mraba milioni 1.3, na akthari ya karibu watu milioni 25 na laki nne wa nchi hiyo ni Waislamu.