Onyo la Russia kwa Israel: Msithubutu kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran
(last modified 2024-10-18T02:52:27+00:00 )
Oct 18, 2024 02:52 UTC
  • Onyo la Russia kwa Israel: Msithubutu kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran

Russia imeuonya vikali utawala haramu wa Israel na kuutaka usijaribu hata kufikiria kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran.

Shirika la habari la TASS limemnukuu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Ryabkov akisema, Moscow inaionya Israel isijaribu kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran.

"Tumeonya mara kwa mara na tunaendelea kuonya...tunaionya (Israel) dhidi ya hata kutafakari uwezekano wa kupiga vituo vya nyuklia vya (Iran) na miundombinu ya nyuklia," Ryabkov amenukuliwa akisema hayo na TASS.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza kuwa, kushambuliwa vituo vya nyuklia vya Iran kutazusha janga kubwa, mbali na ukweli kwamba hatua hiyo itakuwa imekiuka sheria na kanuni zote zilizopo katika eneo, za kudhamini usalama wa nyuklia.

Baada ya Iran kufanya operesheni ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel iliyopewa jina la Ahadi ya Kweli 2 mnamo Oktoba Mosi, utawala wa Kizayuni umekuwa ukibwabwaja na kutishia kuwa utashambulia vituo vya nyuklia vya Iran.

Hata hivyo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) linasisitiza kuwa, Operesheni ya Ahadi ya Kweli 2 lilikuwa onyo tu; na kama Israel itakosea na kuthubutu kufanya uvamizi, utakabiliwa na jibu kali zaidi.

Tags