Kikosi cha EAC nchini Kongo DR chaongezwa muda wa kuhudumu
(last modified Wed, 06 Sep 2023 10:34:39 GMT )
Sep 06, 2023 10:34 UTC
  • Kikosi cha EAC nchini Kongo DR chaongezwa muda wa kuhudumu

Jumuiya ya Afrika Mashariki imekiongeza muda wa kuhudumu kikosi cha kikanda cha jumuiya hiyo (EACRF), chenye jukumu la kukomesha mapigano na kuzima uasi huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Viongozi wa EAC kwa kauli moja jana Jumanne katika mkutano wao huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya, waliafikiana kukiongeza muda wa miezi mitatu Kikosi hicho cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF).

Taarifa iliyotolewa mwishoni mwa Mkutano wa 22 wa Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki imesema, kikosi hicho cha kikanda ambacho muda wake ulikuwa unamalizika Septemba 8, sasa kitasalia mashariki mwa DRC hadi Disemba 8.

Taarifa hiyo imeishukuru Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwa kuchangia dola milioni 2 kwenye mfuko wa kufadhili shuguli za Kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Kongo DR (EACRF).

Kikosi hicho cha kikanda ambacho kilitumwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mara ya kwanza mnamo Novemba mwaka jana, kinashirikiana na wanajeshi wa Kongo katika kukabiliana na harakati za magenge ya waasi kama M23, yanayopambana na jeshi la Kongo FARDC mashariki wa DRC.

Wanajeshi wa EAC nchini DRC

Muda huo umerefushwa katika hali ambayo, Kinshasa imewahi kuyalaumu majeshi hayo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) kwamba hayajafanikiwa ipasavyo kukomesha machafuko katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi, huko nyuma alivituhumu vikosi hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ikiwemo kukabiliana na makundi yenye silaha.

Tags