Sep 16, 2023 10:54 UTC
  • Sheikh Ponda: Wanawake Waislamu Tanzania washiriki katika masuala ya kitaifa

Katibu wa Shura ya Maimamu nchini Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda amewataka wanawake wa Kiislamu nchini humo washiriki katika masuala ya kitaifa ikiwemo masuala ya maendeleo na uongozi na kutahadharisha kuwa kutofanya hivyo kunatoa nafasi kwa watu wengine kushiriki kwa niaba yao.

Sheikh Ponda ametoa wito huo leo Jumamosi katika kongamano la Baraza Kuu la Wanawake wa Kiislamu Tanzania lililofanyika jijini Dar es Salaam.

"Nawashauri mshiriki katika masuala ya maendeleo ya nchi, tumeelezwa kuwa rekodi zetu hazionyeshi kama tunashiriki katika mambo yanayotuhusu. Wanawake wa Kiislamu hawaonekani kushiriki katika masuala ya nchi", ameeleza Katibu huyo wa Shura ya Maimamu na kuongeza kuwa hiyo ni sababu ya mambo yao nchini kuganda kwa namna moja au mbalimbali na kwamba kutoshiriki maana yake ni kutoa nafasi kwa watu wengine washiriki kwa niaba yao.

Wanawake Waislamu Tanzania wakiwa katika hafla ya Maulidi ya Mtume SAW

Sheikh Ponda ametanabahisha kuwa, kutokuwepo ushiriki wa kutosha wa wanawake wa Kiislamu katika masuala ya kitaifa ikiwemo vikao vya maamuzi kunasababisha maslahi yao kutolindwa.

Aidha, Katibu wa Shura ya Maimamu nchini Tanzania amesema, kushiriki katika masuala ya uongozi sio dhambi.

"Tunaposhiriki masuala ya nchi, unajitetea mwenyewe; na usiposhiriki unamuachia mtu mwingine kwenye nafasi ile ya maamuzi. Tunapofanya mikutano ya kitaifa mnatakiwa mshiriki", amesisitiza Sheikh Ponda.../

 

Tags