Somaliland yapuuzilia mbali pendekezo la Rais wa Uganda kuhusu mazungumzo ya amani
Serikali ya Somaliland imetangaza kuwa, haina mpango wowote ulewa kufanya mazungumzo kuhusu kujadili suala la amani na umoja na serikali ya Somalia.
Taarifa hiyo inatolewa baada ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni kutangaza hivi karibuni kwamba, yuko tayari kuwa mpatanishi kati ya eneo hilo ambalo limejitenga na serikali ya shirikisho ya Somalia.
Hivi karibuni Rais Yoweri Museveni, alinukuliwa akisema kuwa, amekubali kuchukua nafasi ya mratibu wa amani kati ya pande hizo mbili baada ya kukutana na mjumbe wa serikali ya Somaliland jijini Entebbe Uganda.
Wakati wa mazungumzo hayo, Rais Museveni alisema haungi mkono mpango wa eneo la Somaliland kujitenga akisema haukuwa uamuzi bora.
Katika taarifa yake Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Somaliland imesema, mazungumzo ya aina yoyote na serikali ya Mogadishu, hayatajadili suala la umoja bali yanapaswa kujadili namna pande hizo mbili zinaweza kusonga mbele kila moja kwa njia tofauti.

Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa, Jamhuri ya Somaliland kwa mara nyingine tena inasisitiza na kuuthibitisha Umoja wa Afrika na jumuiya nyingine za kimataifa kwamba, haina mpango wa kufanya mazungumzo ya kujadili umoja na Somalia.
Somaliland ilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Somalia mwaka 1991 na tangu wakati huo imekuwa ikitafuta njia za kutambuliwa kimataifa bila mafanikio.
Mazungumzo kati ya pande hizo mbili yamekuwa yakiendelea kwa miaka na kujikita zaidi katika suala la usimamizi wa anga na harakati za kuvuka mpaka na vilevile hitajio la Somaliland ya kutambuliwa kama nchi huru.
Hata hivyo hadi sasa hakuna hatyua ya maana iliyopigwa katika mazungumzo hayo.