Sep 26, 2023 10:32 UTC
  • Kusalimu amri Ufaransa mbele ya takwa la Niger

Hatimaye, baada ya wiki kadha za vuta nikuvute, Ufaransa imesalimu amri mbele ya takwa la Niger na kutangaza kwamba, balozi wa Ufaransa nchini Niger, Sylvian Itte, atarejea Paris katika saa chache zijazo.

Tangazo la Ufaransa linasema pia kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo nao wataondoka Niger ifikapo mwishoni wa mwaka huu.

Sambamba na kutangazwa kwa habari hii, Baraza la Kijeshi la Niger katika taarifa yake limeeleza kuwa, kuondolewa kwa wanajeshi wa Ufaransa na balozi wa Ufaransa nchini Niger ni wakati wa kihistoria kwa nchi hiyo na kutangaza katika taarifa yake kwamba leo tunaadhimisha enzi mpya katika njia ya uhuru na mamlaka ya kujitawala Niger.

Baraza la kijeshi la Niger lilikuwa limeitaka Ufaransa kuondoa wanajeshi wake kutoka Niger ifikapo Septemba 3. Baraza hilo pia lilitishia kwamba vinginevyo baada ya tarehe hii, makamanda wa kijeshi wa Ufaransa watawajibika kwa matukio yoyote yatakayotokea.

Tarehe 26 Julai 2023, gadi ya rais wa Niger ilifanya mapinduzi dhidi ya rais wa nchi hiyo, Mohamed Bazoum, na mkuu wa walinzi wa rais wa Niger, Abdelrahman Tiani, akajitangaza kuwa kiongozi mpya na mkuu wa baraza la mpito. Moja ya matakwa ya awali ya Baraza la Kijeshi la Niger ni kuondolewa kwa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo na kukomeshwa uingiliaji kati wa Paris nchini humo, ombi ambalo lilipingwa na Ufaransa na wafuasi wake.

 

Mamlaka za Ufaransa, haswa katika muongo mmoja uliopita, zimetuma vikosi vyao vya kijeshi katika nchi mbalimbali za bara hilo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na makundi ya kigaidi yaliyoko barani Afrika. Kwa muda mrefu, licha ya madai ya Paris, vikosi hivi vimesababisha kutoridhika kwa nchi za Kiafrika, na watu wa nchi hizi wamekuwa wakitaka kuondoka wanajeshi wa Ufaransa katika nchi zao. Kama ilivyoshuhudiwa katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita ambapo mapinduzi katika nchi za Mali, Burkina Faso na Niger yalikaribishwa kwa mikono miwili na wananchi watu wa mataifa hayo wamekaribisha mabadiliko ya kisiasa katika nchi zao kwa kauli mbiu ya kifo kwa Ufaransa.

Ingawa wanajeshi wa Ufaransa hatimaye waliondoka Mali na Burkina Faso, Paris ilitarajia kudumisha uwepo wake wa kijeshi nchini Niger. Maafisa wa serikali ya Ufaransa walitangaza tangu kuanza kwa mabadiliko ya serikali nchini Niger kwamba watahakikisha balozi wao anabakia mjini Niamey. Vyombo vya habari vya Ulaya pia vilionya kwa uwazi kwamba, mamlaka ya Ufaransa inaweza kutumia njia za kijeshi kumrudisha Mohammad Bazoum madarakani.

Lakini matakwa ya wananchi na kusimama kidete Baraza la Kijeshi la Niger kulisababisha Ufaransa kujiondoa kwenye nafasi yake ya awali. Sambamba na tangazo la kufungwa kwa anga ya Niger kwa ndege za Ufaransa, Paris ilimwita nyumbani balozi wake nchini Niger na kutangaza kumalizika kwa uhusiano wa kijeshi na nchi hii.

Katika kuhalalisha uamuzi huu, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema: Niger si nchi tena inayotaka kupambana na ugaidi.

Wanajeshi waandamizi wa Niger waliomuandoa madarakani kwa mapinduzi Rais Muhammad Bazoum

 

Ufaransa inaondoa vikosi vyake kutoka Niger huku nchi nyingine za Afrika zikiwa haziko tayari kukubali uwepo wa vikosi vya kigeni kwa muda mrefu. Sambamba matukio ya kimataifa, kuongezeka kwa kiwango cha elimu na ufahamu wa wananchi na kuingia madarakani kizazi kipya cha viongozi, wananchi wa Afrika hawako tayari tena kufuata siasa za Ufaransa au mataifa mengine ya Magharibi.

Ahmad Abdallah, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na suala hili kwamba: Ingawa vita vya ushawishi katika bara la Afrika vinaendelea kati ya mataifa makubwa, lakini mazingira ya sasa ni fursa kwa nchi za Kiafrika kuchora kigezo chao kwa uhuru zaidi.

Inaonekana mchakato wa kutafuta mamlaka ya kujitawala katika nchi za Kiafrika utaendelea ambapo hitilisho lake ni kuondoka Ufaransa na nchi zingine za magharibi kutoka kwa nchi za bara la Afrika.

Tags