Zimbabwe katika jitihada za kuzuia kuenea mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu
(last modified Mon, 23 Oct 2023 12:40:50 GMT )
Oct 23, 2023 12:40 UTC
  • Zimbabwe katika jitihada za kuzuia kuenea mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu

Serikali ya Zimbabwe imetangaza kuchukua hatua za kudhibiti kuenea ugonjwa wa kipindupindu nchini humo ambapoo hadi sasa watu 5,000 wamepata maambukizi tangu mwezi Februari mwaka huu.

Zimbabwe inafanya kila iwezalo ili kuzuia kuenea kwa mlipuko wa kipindupindu, huku serikali ya nchi hiyo ikitangaza hatua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huo. Hali ya wasiwasi imetanda juu ya uwezekano wa kukaririwa mlipuko kama ule wa mwaka 2008 huko Zimbabwe  ambao ulipelekea kutangazwa dharura ya kitaifa.  

Hadi sasa maambukizi kadhaa ya ugonjwa wa kipindupindu yameripotiwa   katika majimbo yote 10 ya Zimbabwe, huku kukiwa na ongezeko la kutisha zaidi katika majimbo ya kusini-mashariki ya Masvingo na Manicaland. Serikali ya Zimbabwe imetangaza kuwa kipindupindu kimeuwa watu zaidi ya 100 na kuambukiza wengine 5,000 nchini humo tangu mwezi Februari mwaka huu. 

Mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu Zimbabwe 

Tayari serikali ya Harare imetangaza hatua kadhaa za kuzuia kuenea maambukizi ikiwa ni pamoja na kuzuia safari katika maeneo yaliyoathirika, kupunguza idadi ya watu mazikoni hadi 50 na kuzuia watu kusalimiana kwa kupeana mikono au kugawa chakula katika maeneo ya mikutano, sherehe n.k.